Nyuma ya pazia Simba, Yanga kukipiga Kigoma

SOTE tunafahamu kuwa leo Jumapili Julai 25, ni siku muhimu kwa wadau wa mchezo wa soka nchini na hata walio nje ya nchi kwa sababu watakuwa wakifuatilia kila kinachoendelea mjini Kigoma ambapo Simba na Yanga zitakutana katika mechi ya fainali ya Kombe la Azam Sports Federation msimu huu.

Mechi hiyo inayokutanisha watani wa jadi siku zote imekuwa ndio kubwa kuliko nyingine nchini kutokana na historia ya timu hizo, ambapo kila timu huchukulia mechi dhidi ya mtani kuwa fainali hata kama itakuwa ya ligi au kombe.

Safari hii mara ya kwanza timu hizo mbili kongwe nchini zinakutana katika Mkoa wa Kigoma na mechi kuchezwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, hivyo kuweka historia ya watani hao kukutana mkoani humo kwa mara ya kwanza tena katika mchezo wa fainali.

Hatua hii inaongeza ushindani unaovutia sio tu kwa upande wa mashabiki, bali hata kwa benchi la ufundi na wachezaji pia ambapo kila mtu hutamani kuweka rekodi mpya kukumbukwa na vizazi vijavyo. Timu hizo zimekwishawahi kukutana kwenye mechi zilizochezwa katika mikoa mbalimbali kama vile Mwanza (Uwanja wa CCM Kirumba), Arusha (Sheikh Amri Abeid), Morogoro (Jamhuri) na Dodoma (Jamhuri), lakini kwa Kigoma mechi inayozikutanisha timu hizo haijawahi kuchezwa, hivyo kuwa ndio mara ya kwanza.

Hatua hii imesababisha kuwa na hamasa kubwa kwa wadau wa klabu hizi waliopo katika mkoa huo na mikoa jirani, hivyo kuonyesha uhitaji wa matukio kama haya kusambazwa katika mikoa mingine, na miaka ijayo hata katika wilaya mbalimbali.

Kitendo cha mechi kama hizi kuchezwa katika viwanja mbalimbali ni miongoni mwa mikakati ambayo hupangwa na kutumika kwa malengo ya kuusambaza mchezo wa soka maeneo tofauti, lakini pia kupitia umaarufu wa mechi hiyo klabu husika hupata nafasi ya kutengeneza mashabiki na wafuatiliaji wapya katika maeneo au mikao hiyo.

Ndio maana tunakumbuka 2017 wababe wa Ligi Kuu Hispania (La Liga), Real Madrid na Barcelona waliwahi kukutana mjini Miami nchini Marekani kwenye International Championship Cup iliyoandaliwa na kampuni ya Heineken na timu hizo kuweka rekodi kuwa mara ya pili kukutana katika mechi ya watani wa jadi nje ya Hispania.

Lakini, kwa kukutana tu zilifanikiwa kuongeza idadi kubwa ya mashabiki nchini Marekani ambao iliziwavutia hadi kuanza kupanga mikakati ya baadhi ya mechi za La Liga kuchezwa nchini humo kwa lengo la kibiashara na kutengeneza wapenzi wapya.

Hali hiyohiyo ilianza kuonekana hata katika mechi hii ya watani wa jani nchini kwani ukifuatilia mijadala kwenye mitandao ya kijamii na hata vijiwe mbalimbali vya soka utagundua kuwa tangu siku ya kwanza Simba na Yanga ziliposhinda katika mechi za nusu fainali, mambo yalichangamka zaidi.

Utagundua kuwa Mkoa wa Kigoma umekuwa ukitajwa na kuzungumzwa sana katika vyombo mbalimbali vya habari hadi kuwafanya mashabiki wa klabu hizi kutengeneza kauli ya “Tukutane Kigoma.”

Hivyo katika jicho la biashara hali ya kutajwa kwa mkoa au sehemu fulani na kuzungumziwa kwa mazuri mara kwa mara katika vyombo vya habari ni moja kati ya vitu vinavyotakiwa sana kibiashara, kwani kutajwa huko ndiko huongeza umaarufu wa bidhaa au huduma kama tunavyoona kampuni mbalimbali za biashara zikitumia fedha nyingi kutangaza bidhaa zao katika vyombo vya habari. Kitendo cha kupeleka mechi hiyo mkoani Kigoma kina manufaa makubwa kibiashara kwa mkoa husika kutangaza fursa zake na kuvutia wawekezaji au watalii kupitia mchezo wa soka, lakini pia kuzinufaisha klabu zenyewe kwa kutengeneza mashabiki na wapenzi wapya wa timu hizo, hivyo kufikiria kuwa na utaratibu kama huo kwa siku zijazo.

Leo naishia hapa huku nikisubiri mrejesho kutoka kwako.


IMEANDIKWA NA ALI MAYAY