NYUMA YA PAZIA: Ronaldo hajahofia mlango wa kikao Old Trafford

Sunday September 26 2021
RONALDO PIC
By Edo Kumwembe

UNAFUNGUA mlango wa kuingia kikaoni. Meza kubwa amekaa Muhammad Ali, kushoto kwake kuna George Foreman, kulia kuna Mike ‘Iron’ Tyson na kwa mbali unamuona Joe Frazier ‘Smoking Joe’ ambaye ananong’onezana kitu na Lennox Lewis. Unatafakari mara mbili namna ya kuingia katika kikao.

Unajijua kwamba wewe ni bondia mchanga. Huruhusiwi katika kikao hiki. Unasalimia, unageuka nyuma na kuondoka zako taratibu na kwa heshima kubwa. Hali hiyo haipo katika klabu inayoitwa Manchester United kwa sasa. Maisha yameenda kasi.

Zamani ukienda katika kikao cha Manchester United unafungua mlango unakuta Sir Alex Ferguson anaongea. Wanaosikiliza ni Roy Keane ambaye ambaye amekaa naye karibu. Kando kuna David Beckham na Paul Scholes wanatetea jambo. Halafu nyuma yao kuna Dwight Yorke na Andy Cole. Hapo ni lazima ufungue mlango na kuondoka zako. Kama hutaondoka basi utajikuta umekaa kinyonge tu. Hata hivyo maisha hayakuwa hivi wakati Bruno Fernandes alipotua Manchester United, Januari mwaka jana. Aliingia katika kikao na moja kwa moja akaanza kupiga kelele.

Bruno alipoingia alijikuta mkubwa moja kwa moja. Amheshimu nani? Marcus Rashford? Hajawahi hata kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England. Anthony Martial? Hapana. Anacheza anavyojisikia. Leo anafunga, kesho anaondoka uwanjani msafi kama vile alikuwa hachezi mechi. Bruno alicheza miezi michache tu, lakini akawa mchezaji bora wa msimu wa United. Kuanzia Januari mpaka Mei ilimtosha kuwa mkubwa ndani ya klabu na pia nje. Ndivyo yalivyo maisha ya Manchester United katika miaka ya siku hizi.

Leo Manchester United wanamuimba Cristiano Ronaldo katika umri wa miaka 36. Anastahili kuimbwa. Huu ulikuwa umri ambao Ronaldo angeweza kufungua mlango wa kikao cha Manchester United na kujikuta akitishika.Kama angefungua mlango wa kikao na kumkuta Keane, Scholes, Giggs, Beckham, Dwight, Cole na wengineo angeweza kutishika. Angeweza kutafakari maamuzi yake ya kurudi katika klabu hii. Sio ajabu asingehitajika uwanjani.Lakini pambano la kwanza tu la

Ronaldo dhidi ya Newcastle United amecheza dakika zote 90. Usisahau kwamba alifunga. Kufunga kunadhihirisha Ronaldo bado wamo. Katika pambano lile bila ya Ronaldo maisha yangekuwa magumu kwa United.

Advertisement

Kucheza dakika 90 kulimaanisha mambo mawili kama sio matatu. Ole Gunnar Solskjaer hakuwaamini sana watu waliokuwa katika benchi ambao wangeweza kucheza katika nafasi ya Ronaldo licha ya Ronaldo kuwa na umri wa miaka 36 na wao kuwa vijana. Kama katika benchi angekuwepo mchezaji mwenye ubora wa Giggs si ajabu Solskjaer angemtoa Ronaldo dakika ya 70 ya mchezo. Lakini pia Ronaldo alikuwa anaonyesha machale ambayo wachezaji wengine wa United wasingeweza kuonyesha. Tangu afike Ronaldo anaonekana anafunga mabao rahisi. Hapana, sio rahisi. Ni mabao magumu. Kitendo cha kujua kipa anaweza kuudondosha mpira na eneo la kukaa ni kitu muhimu katika soka. Mara ngapi makipa wanadondosha mpira na hakuna kinachotokea. Mara ngapi uwanja unatapika kwa kelele baada ya mpira kujikatizia katika boksi la adui, lakini tusione mtu wa kuukwamisha katika nyavu. Ronaldo amevuna uzoefu wa miaka 18 sasa kuweza kujua maeneo ya kukaa na yale mabao sio rahisi.

Majuzi tu kulikuwa na mechi ya Carabao pale Old Trafford na Ronaldo alikuwa jukwaani. Tulishuhudia jinsi ambavyo watoto wa Solskjaer walishindwa kurudisha bao la mapema la West Ham. Haya unaweza kuyaona mambo ya kawaida kama Ronaldo akikaa jukwaani. Akiwa ndani ya uwanja anaweza kukugeuzia kuwa mabao.

Ninachotabiri ni kwamba Ronaldo ataibeba Manchester United msimu huu, lakini sidhani kama mabao yake yataweza kuipa ubingwa Manchester United. United ya leo ina wachezaji wachache wenye ubora wa hali ya juu.

Bahati mbaya pia hata wale wenye ubora bado wanakosa mwendelezo wa ubora. Ni tofauti na ilivyo kwa Manchester City au Liverpool. Hapohapo nina wasiwasi hata Ronaldo mwenyewe anaweza kuchoka mbele ya safari.

Ni kweli ni mchezaji ambaye yuko fiti, lakini muda umefika sasa wa namna ya kumtumia Ronaldo. Kwanza mwenyewe kwa muda mrefu amejua jinsi ya kujitumia na ndio maana ameendelea kubakia katika kiwango kizuri.

Kwa sasa Ronaldo anavizia zaidi pengine kuliko kupiga zile chenga zake za ‘baiskeli’ kama alivyokuwa wakati akiwa na umri wa miaka 18. Huu ni mfano mzuri wa namna ya kujua kujitumia kadri ya umri unavyokwenda.

Lakini bado inahitajika namna ambavyo Solskjaer atajua kumtumia Ronaldo kwa ajili ya kumuweka fiti muda mrefu wa msimu. Mfano mzuri ni namna alivyomweka nje katika pambano la Carabao majuzi dhidi ya West Ham.

Lakini pia atapaswa kumuacha nje katika mechi kadhaa za Ligi Kuu. Tofauti ya Italia na Ligi Kuu ya England ni kwamba EPL ina matumizi makubwa ya nguvu kuliko Ligi Kuu ya Italia. Ronaldo akicheza kila wikiendi na kwa dakika zote 90 kuna uwezekano akafika Januari akiwa hoi.

Ligi ya Italia ilikuwa salama kwa afya yake. Tatizo kubwa ni kwamba Solskjaer atajikuta akitamani kumtumia Ronaldo kila mara kutokana na ubovu wa kina Martial. Hatakuwa na jinsi. Wakati mwingine hatutakuwa na lawama kwake. Tazama jinsi ambavyo Lionel Messi ametafuta kichaka sahihi cha kujificha. Amekwenda PSG ambayo kuna Neymar, Angel Di Maria, Kylian Mbappe, Marco Verrati na wengineo. Kule ataweza kujificha na kupumzika.

Ronaldo kama angekuwa anacheza Liverpool au Manchester City angeweza kusaka kijiwe kizuri zaidi ya kujificha lakini kwa United hii, tena inayofundishwa na Solskjaer nina hofu kwamba mambo mawili yanaweza kutokea.

Kuna uwezo wa Ronaldo kufunga mabao mengi ya bure ambayo hayakuwa na msaada sana kwa timu yake mwishoni mwa msimu, lakini kuna uwezekano mkubwa wa Ronaldo mwenyewe kujichosha zaidi kabla ya kufika mwishoni mwa msimu.

Advertisement