NYUMA YA PAZIA: Msela Rooney, chupa mpya mvinyo ni ule ule

Tuesday August 03 2021
RONEY PIC
By Edo Kumwembe

JOHANNESBURG pale Afrika Kusini ndipo nilipowahi kusikia kisanga kimoja cha nje ya uwanja cha Sir Alex Ferguson. Wakati huo alikuwa Kocha wa Manchester United. Alipita katika taa nyekundu za barabarani na Polisi wa Kikaburu wakaanza kumfukuza.

Walipomsimamisha akasingizia kwamba alikuwa amebanwa na haja na akalazimisha kuwahi kwa haraka ndio maana akavuka katika taa nyekundu kinyume na sheria. Kichekesho cha aina yake. Walimuachia. Nadhani kwa sababu alikuwa Sir Alex Ferguson.

Arsene Wenger? Sijawahi kusikia kituko chake chochote kile nje ya uwanja. Siwezi kumsingizia. Jose Mourinho? Ana vituko vingi ndani ya uwanja na katika mikutano yake na waandishi wa habari. Fabio Capello? Sijawahi kusikia.

Louis Van Gaal? Hana vituko vya nje. Anacho cha uwanja wa mazoezi tu akiwa na Bayern Munich. Alishusha nguo zake mbele wachezaji wa Bayern na kumuonyesha staa wa Italia, Luca Toni kwamba yeye ni mwanaume hasa na angeweza kumfanya chochote kile.

Tuna makocha wengi wa zamani na hawa wa kisasa, lakini hawana vituko vya nje ya uwanja. Hata hawa wa sasa kina Pep Guardiola, Mauricio Pochettino, Antonio Conte na wengineo wana mikasa yao ya mazoezini lakini si kama huu wa kocha wetu mpya wa Derby Count. Anaitwa Wayne Rooney. Umewahi kulisikia hili jina mahala?.

Ndiye yeye mwenyewe. Wayne Rooney staa wa zamani wa Manchester United. Kwa sasa ni kocha mkuu pale Derby Count. Rooney anakuwa ingizo jipya kwa makocha wapya wa kizazi hiki. Kizazi kinachokuja baada ya kina Pep Guardiola.

Advertisement

Kuna Mikel Arteta, Steven Gerrard, Frank Lampard, Joey Barton, Andrea Pirlo na wengineo. Tunadhani hawa ndio wanakuja kuchukua nafasi za kina Pep na Pochettino lakini tayari Rooney ameshamwaga kituko kipya akiwa kama kocha.

Wiki iliyopita Rooney alipigwa picha akiwa amelewa na kulala katika kiti cha chumba alichokuwa na warembo watatu. Warembo walikuwa wanamchezea kama mdoli huku akiwa amelewa. Ilishangaza sana lakini tukio lake lilikuwa kama vile mvinyo wa zamani katika chupa mpya.

Rooney tuliyemfahamu akiwa kama kocha alikuwa na tabia hizi hizi. Tabia za ovyo nje ya uwanja. Mlevi na mkorofi nje ya uwanja lakini ndani ya uwanja alikuwa na kipaji kikubwa. Huku ndani ya uwanja ndipo ambapo Wayne alitunyamazisha.

Nje ya uwanja Waingereza walipenda Rooney awe kama David Beckham. Walipenda awe mstaarabu na baba mzuri wa familia kama David Beckham. Baada ya Waingereza kumtengeneza Beckham akawa jina kubwa nje ya uwanja dunia nzima walitamani Rooney achukue nafasi hiyo.

Tatizo kubwa ni kwamba Rooney ni msela aliyekulia Croxteth pale Liverpool. Usela haujawahi kumtoka kichwani. Nilidhani kwamba baada ya kuachana na jezi uwanjani na kuanza kuvaa suti nje ya uwanja labda angebadilisha tabia.

Hiki ndicho alichotakiwa kufanya. Rooney anapaswa kuwa mfano. Anapaswa kubadilisha tabia zake lakini hiki kimeanza kuonekana kuwa kitu kigumu kwake. Ndani ya msimu wake wa kwanza tu kama kocha kamili tayari ameshaharibu.

Ameharibu tena kwa mkwewe Coleen na watoto, halafu akaharibu taswira ya timu yake. Waingereza wanalia, Rooney atabadilika lini? Ndivyo alivyo. Ninachojiuliza katika kiti chake cha ukocha ni kwamba kama yeye ataendeleza utovu wa nidhamu wachezaji wake itakuwaje?

Ni kweli kwamba kina Ferguson walikuwa binadamu wa kawaida tu lakini walipambana sana kuficha tabia zao mbovu za nje ya uwanja. Rooney ndani ya msimu mmoja tu ameendeleza tabia zake zile zile za zamani wakati anacheza. Sijui safari yake itakuwaje mbele ya safari.

Lakini subiri kwanza. Kuna hili jambo hapa ambalo limenichekesha sana. Baada ya kutoka katika mkasa wake wa kupigwa picha akiwa amelala amelewa, kesho yake Rooney akarudi katika uwanja wa mazoezi na kumuumiza mchezaji wake, Jason Knight.

Alimuumizaje? Alijishikirisha katika mazoezi kama kocha mchezaji kuonyesha mfano lakini wakarukiana na Knight katika staili ya tackling akamuumiza kifundo cha mguu. Nadhani alijisahau akadhani yeye ni mchezaji.

Mara nyingi makocha wamekuwa wakisisitiza kwamba wachezaji wasiingiane kwa nguvu wakiwa mazoezini lakini yeye ndiye kwanza akaonyesha mfano mbovu kwa kushindwa kumkwepa mchezaji wake mazoezini.

Huyu ndiye Rooney halisi ambaye anashindwa kuficha makali yake kwa mara nyingine tena akiwa kama kocha. Atafika kweli? Ni jambo la kujiuliza. Wenzake kina Lampard na Gerrard mpaka sasa hawajatupa kisanga hata kimoja.

Gerrard wakati akiwa na Liverpool naye alikuwa na visanga vyake vya pombe lakini huko Scotland mpaka sasa tunaona kimya. Anahitaji uvumilivu wa kazi yake mpya. Hii ni kazi tofauti kulinganisha na ile ya mwanzo. Inahitaji utulivu wa akili zaidi.

Wakati akiwa Manchester United watu wa saikolojia wa Manchester United walimtengenezea Rooney begi (punching bag) ambalo watu wa mchezo wa ndondi huwa wanawafungia mabondia kwa ajili ya kulipiga ngumi kama sehemu ya mazoezi.

Walimfungia punching bag na kumpa maagizo kwamba awe analipiga ngumi mara nyingi awezavyo kwa ajili ya kupunguza hasira zake. Nadhani akiwa kama kocha huu ndio wakati mwafaka kwake kufunga begi hilo kwa ajili ya kupunguza hasira. Kama anaweza kumrukia mchezaji wake bila ya kumkwepa vipi kwa makocha wengine ambao atapambana nao katika ule mstari wa nje ya uwanja kando ya mwamuzi wa akiba.

Vinginevyo kila la kheri kwake. Yeye na wengineo ndio kizazi kipya cha makocha. Mbaya zaidi ni kwamba Rooney alikuwa mchezaji mzuri uwanjani. Kwangu ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kumuona Ligi Kuu ya England.

Kuna hisia kwamba wachezaji wengi bora huwa hawageuki kuwa makocha mazuri. Wengi wanasubiri kuona mchezaji kama yeye atakuwa kocha wa aina gani. Atafeli kama Diego Maradona au atafaulu kama Johan Cruyff.

Advertisement