NYUMA YA PAZIA: Mendy, mzalendo au muoga mwenye majuto?

Muktasari:

EDOUARD Mendy mapema wiki hii alisafiri kutoka Uwanja wa Heathrow jijini London hadi Uwanja wa Ndege wa Leopold Sedar Senghor jijini Dakar ‘nchini kwao’ Senegal kucheza pambano dhidi ya Namibia.

EDOUARD Mendy mapema wiki hii alisafiri kutoka Uwanja wa Heathrow jijini London hadi Uwanja wa Ndege wa Leopold Sedar Senghor jijini Dakar ‘nchini kwao’ Senegal kucheza pambano dhidi ya Namibia.

‘Nchini kwao’ kama ilivyowekwa inamaanisha tofauti. Mendy alizaliwa Ufaransa miaka 29 iliyopita. Amekulia Ufaransa. Amelelewa Ufaransa. Katika soka hakuwahi kugusa timu yoyote Senegal.

Safari yake katika wikiendi hii ya mechi za kimataifa ingeweza kuwa tofauti. Baada ya pambano dhidi ya Southampton pale London, Mendy angeweza kusafiri kutoka London kwenda katika kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa pale Paris na kisha kuibukia katika Uwanja wa Ndege wa Brussels kwa pambano kati ya Ubelgiji dhidi ya Ufaransa juzi. Haikuwezekana.

Mendy ni mmoja kati ya vijana wengi wa Kiafrika waliozaliwa Ulaya ambao hawakuwahi kujua kwamba maisha yangeweza kubadilika njiani. Kwa sasa ni kipa mwenye hadhi ya kuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ufaransa.

Ukimtazama katika lango la Chelsea jinsi anavyojaa, jinsi anavyopangua michomo ya hatari, jinsi anavyosambaza mipira kwa mabeki wake, Mendy anabakia kuwa mmoja kati ya makipa wa kisasa zaidi katika soka la kileo.

Msimu uliopita alichaguliwa kuwa kipa bora wa Ulaya baada ya kulilinda lango la Chelsea na kutwaa ubingwa wa Ulaya. Ilikuwa mbele ya hao kina Manuel Neuer. Lakini pia ilikuwa mbele ya kipa namba moja wa Ufaransa, Hugo Lloris ambaye pia ni nahodha wa kikosi hiki. Hata hivyo Mendy alichagua kucheza Senegal katika taifa ambalo mama yake ametoka. Kabla ya hapo alitamani kucheza katika kikosi cha Guinea Bissau ambacho baba yake ametoka. Yeye mwenyewe amezaliwa Ufaransa.

Ina maana Mendy angeweza kucheza Ufaransa, Senegal au Guinea Bissau. Alichagua kucheza Senegal. Kisa? Kunaweza kuwa na sababu mbili. Kwanza kabisa ni uoga wa kusubiri na kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Ufaransa. Lakini pia inawezekana amelelewa katika makuzi ya Kiafrika zaidi na kisha akajiona Mwafrika ambaye hastahili

kukaa katika lango la wazungu wakati anasubiriwa kudakia timu ya nyumbani. Sababu hizi mbili zinawafanya baadhi ya wachezaji wa Afrika kujutia uamuzi wao mbele ya safari.

Mastaa hawa hawawezi kututamkia lakini nahisi wanaweza kuwa wanajuta au hawajuti. Kwa mfano, Kalidou Koulibaly wa Napoli ni mmoja kati ya walinzi imara barani Ulaya ambaye amezaliwa Ufaransa lakini aliamua kucheza nyumbani Senegal na sasa anamlinda Mendy.

Kila nikiwatazama kina Raphael Varane na wenzake katika safu ya ulinzi ya Ufaransa sioni kwanini Koulibaly asingeweza kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa. Hata kama asingecheza basi angeitwa tu na si ajabu leo angekuwa mmoja kati ya wachezaji wa Ufaransa ambao wamewahi kutwaa Kombe la Dunia pale Russia 2018.

Vipi kuhusu Riyad Mahrez? Alichagua kucheza Algeria licha ya kuzaliwa Ufaransa. Ina maana Mahrez angeshindwa kucheza mbele ya kina Thomas Lemar? Sidhani. Nadhani moja kati ya sababu hizo mbili nilizozitaja ilimkimbiza Mahrez kuiwakilisha Algeria badala ya Ufaransa. Vipi kuhusu Pierre-Emerick Aubameyang? Huyu naye ni mmojawapo. Nadhani angeweza kucheza kikosi cha Ufaransa alikozaliwa lakini akaamua kucheza Gabon ambayo haikuwahi kushiriki hata Kombe la Dunia.

Kuna wachezaji wengi wa Kiafrika walioamua kuchukua uamuzi huo ambao ni mzuri na wa kizalendo kwa sisi Waafrika, lakini katika mioyo yao huwa unaacha maswali baadaye kutokana na mwenendo wa kusuasua wa mataifa ambayo waliamua kuyawakilisha kwa sababu ya asili za wazazi wao.

Ni kama hapo nyuma ambapo Zinedine Zidane aliamua kutoa uoga na kuamua kucheza katika kikosi cha Ufaransa badala ya Algeria ambako wazazi wake walitoka kabla ya kuamua kuzamia Ufaransa. Ni kama tu ilivyo sasa ambapo Hakim Ziyechi alipoamua kuichezea Morocco badala ya Uholanzi ambako amezaliwa. Wapo wengi wa wachezaji wa namna hii na katika kundi hili kwa sasa anaingia Mendy. Sioni kama Lloris wa sasa ana uwezo kuliko Mendy. Kama Lloris angeendelea kucheza mbele ya Mendy ni kwa sababu ya tabia ya kocha Didier Deschamps ambaye anapenda kuwaamini wachezaji anaowajua yeye pengine kuliko wenye viwango halisi. Na labda pia rangi yake ingeweza kumuweka benchi. Sio kitu kizuri kukizungumza hadharani lakini ubaguzi bado upo katika soka.

Hata hivyo ni faraja kwetu kumuona Mendy aking’ara katika lango la Chelsea akiwa kipa ambaye anaiwakilisha Afrika. Sijawahi kumuona kipa mweusi Afrika ambaye amewahi kutamba katika klabu kubwa za Ulaya kiasi hata cha kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Eneo la lango katika klabu kubwa ni la wazungu tu. Sitaki umhesabie Bruce Grobbelaar katika kundi hili. Huyu ni mzungu ambaye alizaliwa jijini Durban - Afrika Kusini na walowezi wa Kiingereza waliozamia Zimbabwe kwa ajili ya kusaka ardhi. Vinginevyo klabu kubwa kama Chelsea, Arsenal, Manchester United, Real Madrid, Barcelona, Juventus, AC Milan na wengineo hawajawahi kuwa na makipa weusi wanaocheza katika timu za taifa za Afrika. eneo hilo ni la wazungu tu.

Tuliwahi kuwa na makipa bora kutoka Afrika lakini waliishia kucheza timu za viwango vya Real Sociedad, Nice au Athletic Bilbao. Cameroon ndio ilikuwa inatuletea makipa wa namna hii kina Jose Antonio Bell, Thobian Nkono na Jaqcues Sang’oo. Hata hivyo hawakuwahi kutwaa ubingwa wa Ulaya mahala katika kiwango ambacho Mendy amefikia. Kipa pekee ambaye anajivuta katika anga za Mendy ni Andre Onana anayedaka Ajax Amsterdam ya Uholanzi lakini mpaka sasa nashangaa kuona hasogei. Alianza kung’ara mapema kabla ya Mendy wakati alipoifikisha Ajax nusu fainali za Ulaya miaka michache iliyopita lakini naona nyota yake imefifia. Ikumbukwe pia kwamba tunaweza kujivunia Mendy kwa sababu pale Chelsea alikwenda kumuweka benchi kipa ambaye aliaminika atakwenda kuwa kipa namba moja wa Hispania, Kepa Arizabalaga.