NIONAVYO: Mbio za unbeaten zimeisha zimebaki zile za Ubingwa Ligi Kuu

WALIOSEMA duniani wawili wawili hawakukosea. Msemo huu una maana kwamba duniani kuna watu au matukio hufanana au kuelekeana kwa namna fulani. Hivyo ndivyo wamekuwa wakijinadi baadhi ya wapenzi wa Young Africans SC kufuatia kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa Ihefu FC ilichopata timu yao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara hivyo kukata mnyororo wa michezo 49 (Unbeaten) ya ligi bila kufungwa.

Unbeaten neno la Kiingereza likimaanisha kutokupoteza au kutofungwa limekuwa neno maarufu katika ulimwengu wa soka hapa Tanzania kwa siku za karibuni. Unbeaten imekuwa redioni, kwenye mitandao hata vijiwe vya kahawa.

Rekodi kama hiyo iliwekwa na klabu ya Arsenal ya London katika Ligi Kuu ya England ikianza Mei 7, 2003 na kukoma Oktoba 16, 2004 katika takwimu zinazoelekeana na za Yanga. Hapa chini ni baadhi ya vitu vinavyofanana au kuelekeana na hata kutofautiana katika rekodi hizi:

Kuna mambo mengi na hata takwimu nyingine ambazo zinatofautisha timu hizi hasa kwa sababu timu hizi zilicheza ligi tofauti lakini kinachozifananisha zaidi ni kwamba timu hizi zilijikuta zinagota katika mchezo wa 49 wa ligi.

Rekodi hiyo ya kutofungwa (unbeaten) ya Yanga katika siku za karibuni ilikuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki huku baadhi wakiomba iendelee mpaka kusikojulikana na wengine wakitamani ikiwezekana ifutwe au ikome mara moja. Ni jambo unalolitegemea katika ligi yenye uhasimu mkubwa lakini pia kwa sasa ni ligi yenye ushindani mkubwa. Hilo linajidhihirisha kwa Yanga inayoongoza ligi yenye timu 16 kufungwa na Ihefu inayoshika mkia katika ligi hiyo.

Laiti kama ubishi kuhusu unbeaten ungehamishiwa katika ushindani uwanjani naamini katika miaka michache tungepata timu nyingine yenye rekodi kama hiyo au hata Young Africans wenyewe wangeweza kuanza safari ya kushindana na rekodi yao.Ndiyo, rekodi haivunjwi kwa kumwombea adui njaa, rekodi zinavunjwa kwa kuweka rekodi bora zaidi.

Naamini, ligi ya unbeaten ilijipenyeza tu katika Ligi Kuu lakini haikuwa mashindano rasmi hivyo timu zinatakiwa kuelekeza macho katika kujiboresha kiushindani na bila shaka takwimu bora zitapatikana na rekodi zitawekwa.Mwisho wa siku anatafutwa bingwa wa Ligi Kuu (NBCPL) bila kujali ni beaten (amepoteza) au unbeaten (hajapoteza).