Ninja alifanya hiki baada ya kupigwa benchi

UVUMILIVU, nidhamu na kujituma vimemnufaisha beki wa kati waYanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuanza kucheza kikosi cha kwanza, licha ya kusalia mechi chache za kumaliza msimu huu.

Ninja alijunga na Yanga kwa mara ya kwanza msimu wa 2017/2019, baadae alipata dili la kuichezea MFK Vyškov ambayo ilimpeleka kwa mkopo wa miezi sita LA Galaxy inayocheza Ligi kuu ya Marekani na baada ya kumalizika mkataba huo alirejea Tanzania.

Ninja hakuendelea kuitumikia MFK Vyskov, alivunja mkataba wa miaka mitatu na kurejea kuitumikia timu yake ya zamani (Yanga), hapo ndipo ilipoanzia changamoto ya kukaa benchi chini ya Zlatko Krmpotic na Cedric Kaze, akishuhudia wenzake wakicheza.

Aliyekuwa kaimu kocha mkuu, Juma Mwambusi ndiye alifufua matumaini ya Ninja ambapo katika mechi tatu alizokiongoza kikosi hicho, akipata alama saba dhidi ya KMC (bao 1-1), Biashara (1-0) na Gwambina FC (mabao 3-1), alimuanzisha kikosi cha kwanza, akicheza dakika 90 na hata baada ya kocha mpya Nasreddine Nabi kuanza majukumu yake ameendelea kumtumia kikosi cha kwanza.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na Ninja, akasimulia alivyopambana kujikwamua na jinamizi la kukaa benchi wakati mwingine kukaa jukwaani hadi kuaminiwa kucheza mechi mzunguko wa pili.

“Ukimuona mchezaji katika timu yoyote, yupo kwa ajili ya kazi, ndio maana hakuna anayeweza kujisikia vizuri kama anakosa nafasi, ingawa lazima kila mmjoa atangulize maslahi ya timu, suala la kiwango linakuja kuonekana kupitia utendaji kazi wako,” anasema.

Anasema kukaa kwake benchi, liligeuka somo la kujua makocha waliopita Yanga msimu huu wanahitaji nini kutoka kwake, aliongeza bidii kuhakikisha haambulii patupu msimu huu.

“2019/20 haukuwa mzuri kwangu kutoka na covid 19 iliyosababisha nirejee nchini, timu nyingi ziliyumba kiuchumi na nilikuwa sijacheza mechi nyingi, baada ya kujiunga na Yanga nikakutana na mabeki ambao walikuwa wameishaamiwa na isingekuwa rahisi kupangua safu ya ulinzi, ila sikukata taamaa nikaamua kupambana.”


ALIWEKA DHAMIRA

Anasema aliweka dhamira ya kuamini ukifika muda wake wa kucheza atacheza na kwamba aliamua kuipambania hilo, akiweka mbele uvumilivu wa kujifunza dhidi ya wale wanaoanza na makocha kile wanachokifundisha.

“Katika soka bila uvumilivu mchezaji huwezi kufika popote, nilitia bidii katika mazoezi, niliangalia wenzangu wana kitu gani na mimi nifanye nini, nikaanza kucheza chini ya kocha Mwambusi na huyo mpya amenipanga pia katika mechi na Azam na Prisons ya Kombe la Shirikisho la Azam,”anasema.


NIDHAMU

Nje na uvumilivu Ninja anasema bila nidhamu mchezaji hawezi kufika popote katika mafanikio ya kipaji chake, kwamba licha ya kwamba alikosa namba lakini haikumfanya awe mvivu wa kufika kwa wakati katika mazoezi na kuyafanya yake binafsi.

“Nilijituma kama vile nacheza kikosi cha kwanza bila kujali kama sichezi hilo kocha Mwambusi alikuwa akilifuatilia, niliwahi sehemu za mazoezi, nashukuru Mungu nimeaanza kucheza lakini wote tupo kwa ajili ya kuijenga Simba,” anasema.

Anaeleza malengo yake katika mechi zilizosalia kwamba anatamani mchango wake uache alama, hasa anatamani kuona Yanga inachukua ubingwa kitu ambacho wanakitamani mashabiki baada ya kukikosa kwa muda wa miaka mitatu. Ninja anaamini kwamba Yanga ina uwezo wa kufanya vizuri msimu huu kwavile bado wana michezo mingi mkono na takwimu zinawapa nafasi mbele ya washindani wao katika nafasi za juu kwenye msimamo. Amesisitiza kwamba haamini kwenye kukata tamaa bali kwa morali iliyopo ndani ya kikosi ana uhakika kwamba watapata kitu msimu huu. Washindani wakubwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu kimahesabu ni Yanga, Simba na Azam ingawa lolote linaweza kutokea.