Nchimbi: Nimerudi kivingine, acheni miguu iongee

HAKUNA ambaye hamkumbuki mshambuliaji Ditram Nchimbi kutokana na usajili wake kutoka Polisi Tanzania kwenda Yanga na ilitokana na kuonyesha ubora pindi timu hizo zilipokutana kwenye misimu miwili nyuma akiifunga Yanga mabao matatu.
Nchimbi alikuwa Polisi kwa mkopo akitokea Azam FC ambayo ilimsajili akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na klabu ya Njombe Mji.
Mshambuliaji huyo alikuwa kimya kwa muda mrefu, huku kukiwa hakuna mtu aliyekuwa anajua alikuwa wapi, lakini Mwanaspoti limemuibua mafichoni kuanzia usajili wa kwenda Fountain Gate. Twende pamoja.


AZAM ILIMKAUSHIA
Nchimbi alisajiliwa na Azam 2018 akizipotezea ofa za Yanga na KMC, na kutua Chamazi ambako kulikuwa na mastaa kama Donald Ngoma na wengineo ambao waliongeza ushindani kikosini.
Mshambuliaji huyo anasema licha ya kujiunga na Azam alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na  kutocheza mechi ya Ligi Kuu jambo ambalo lilimlazimu kutoka kwa mkopo.
"Nilitoka kwa mkopo kwenda Polisi na kwangu ilikuwa furaha kwa kuwa tayari nilishaona kocha hana mpango na mimi, acha nikapambane mwenyewe. Mwisho yeye ndiye aliniita kwenye timu ya Taifa na nikalisaidia Taifa langu," anasema Nchimbi.
"Maisha ya Azam hayakuwa mazuri kwa sababu sikutimiza malengo kwa timu na hata mimi mwenyewe. Nilicheza tu Kombe la Kagame, sikucheza mechi yoyote ya ligi."
Nchimbi anaongeza kuwa: "Kutocheza mechi ya ligi ilinitia sana hasira na nilipopata nafasi ya kutoka kwa mkopo nilipania kufanya vizuri ili nisogelee malengo yangu."


YANGA KITAMBO SANA
Baada ya kwenda kwa mkopo Polisi Tanzania, Nchimbi alianza kuwika na kuhitajika tena na klabu ya Yanga (2019) na yeye mwenyewe anaweka wazi hakushangaa aliposikia timu hiyo inamuhitaji kwani mara kadhaa walikuwa wanashindwana kwenye maslahi.
Nchimbi anasema tangu akiwa yupo Mbeya City alikuwa anapigiwa hesabu na Yanga na hata alipokuwa kwenye timu ya Njombe Mji bado timu hiyo iliendelea kumtafuta.
"Haikunishangaza na ndiyo maana walipoleta ofa niliwaambia Azam kuna ofa naomba mmalizane na Yanga nataka kwenda huko na ofa yao ilikuwa kubwa tofauti na ile ambayo nilitoka Njombe Mji, japo ya Azam ndiyo ilikuwa ya kubwa kwa mara ya kwanza kwangu tangu nianze soka ila ilipokuja ya Yanga ilikuwa mara tatu ya Azam," anasema Nchimbi na kuongeza;
"Muda ulikuwa sahihi kwakuwa nilifika wakati sahihi na nikaingia kwenye mfumo, maisha yalikuwa safi na changamoto zilikuwepo na sehemu yoyote zipo ila pale wananchi siku zote wanataka matokeo,  kuna muda timu haipati matokeo vile wanavyotaka basi hapo utafurahi."


YANGA YAMBADILISHA KILA KITU
Bila kupepesa macho Nchimbi anaweka wazi usajili wake na maisha akiwa Yanga yalibadilisha kila kitu kwake na kumfanya awe mtu wa tofauti kwani maslahi yake yaliboresheka.
"Maisha yangu yalibadilika siku moja kaka hapo nielewe vizuri kabisa yani kila kitu kinabadilika moja kwa moja hadi sasa, Nchimbi wa Majimaji siyo yule aliyepita Yanga kwa sababu kimaisha nimebadilika, kuna vitu nilikuwa sina ila kwa usajili ule nilivipata,"anasema Nchimbi na kuongeza;
"Kuna mafunzo mengi niliyapata nikiwa pale kwa sababu kuna wachezaji wa nchi tofauti, kubwa zaidi unatakiwa uishi na watu vizuri kwani kwenye maisha ya mpira kuna kukutana tena."
Nchimbi anasema hata upande wa timu alizopita yeye kama mchezaji kulikuwa na tofauti kubwa Azam na Yanga kwa sababu hizo ni timu kubwa kwenye soka la Bongo.
"Kuna utofauti mkubwa kati ya timu za zamani nilizopita na Azam na Yanga, hawa wawili ni wakubwa na hata pesa yao ya usajili ipo tofauti, hela niliyopata Azam ilikuwa ni mara nne na timu zangu za zamani na hela ya Yanga ni mara tatu ya hela ya Azam."


GUNDU LA MABAO
Nchimbi bila kupepesa macho anasema alikuwa hayupo sawa wakati vyombo vya habari vinaandika kutokufunga kwake mwaka mzima lakini kama mchezaji alijipambania na kuwa sawa.
"Kipindi Media (Vyombo vya Habari), vinaniandama kwamba sifungi unafika mwaka na kusahau kama naisaidia timu yangu kwa njia nyingine kama kutoa pasi na watu wanafunga, sitakuja kusahau ila ndiyo maisha yalipita na mengine yanaendelea," anasema Nchimbi.
Nchimbi aliwataka wachezaji hasa wazawa ambao bado wapo Yanga wasijisahau kwa sababu wapo kwa ajili ya kuitumikia Yanga na ni taasisi kubwa hivyo wajitoe muda wote.
"Yanga wenyewe wanaita ni taasisi kubwa na ndiyo maana ina neno Daima mbele nyuma mwiko, kikubwa wazingatie sana bidii wasitoke kwenye njia ambayo iliwafanya wasajiliwe Yanga."


ISHU YA GEITA
Nchimbi baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga alisajiliwa na Geita Gold kwa mwaka mmoja lakini mchezaji huyo hakuonekana sana huku kukiwa na taarifa mbalimbali.
Mshambuliaji huyo anaweka wazi alipata msiba lakini wakati huo huo alikuwa na maumivu ya ugoko kwa hiyo alipomaliza msiba alienda kufanya vipimo vya picha (xray) na kutakiwa kupumzika kwa wiki tatu hadi nne.
"Nikatuma taarifa kwa uongozi lakini mwisho wa siku ikachukuliwa tofauti, muda wa kurudi kazini ulipofika kuomba nauli sikutumiwa na wala simu zangu hazikupokelewa," anasema Nchimbi na kuongeza;
"Mwisho walifunga mshahara wangu nikaona acha nikae kimya sikutaka iwe shida acha nipumzike na mkataba ukiisha nitaanza moja, nashukuru Mungu nikapona nikawa sawa kabisa."


MIGUU ITAONGEA
Mshambuliaji huyu anasema kwa sasa akili yake ipo upande wa Fountain Gate na anataka kuhakikisha anaisaidia ili iweze kupanda Ligi Kuu kwenye msimu ujao na ameweka wazi inawezekana kutokana na usajili uliofanywa.
"Nimeona nianze huku ili nipate nafasi ya kucheza zaidi kisha msimu ujao imani yangu inaniambia nitakuwa kwenye Ligi Kuu, nipo hapa kutimiza malengo ya timu yangu,"anasema Nchimbi na kuongeza;
"Kila kitu kinawezekana na zilikuwepo timu nyingi za Ligi Kuu zilionyesha nia ya kunisajili lakini mimi mwenyewe niliamua kuanza huku kwa sababu niliona ni sehemu sahihi kwangu."
Nchimbi amesaini mkataba wa miezi sita tu kuitumikia timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship