MZEE WA UPUPU: Zambia wanafunga VAR, sisi tunaongeza posho za waratibu

MWAKA 2018, CAF ilianzisha kituo cha usimamizi wa mechi ndani ya ofisi zake za makao makuu jijini Cairo, Misri.

Kituo hicho kinachoitwa MATCH COMMAND CENTER, hufanya kazi kama moyo wa mtiririko wa taarifa za mechi za mashindano yote ya CAF.

Kituo hiki kimefungwa kwa teknolojia ya hali ya juu na hutumika kama kiungo kati ya CAF wenyewe na wasimamizi wa mechi zao zote, wakiwemo warusha matangazo, watu wa usalama, na hadi idara zao za masoko.

Kutokana na hili, CAF wakaongeza watu wawili kwenye kila mchezo ili kurahisisha mawasiliano.

Watu hao ni mratibu mkuu wa mchezo (General Coordinator) na ofisa habari wa mchezo.

Shirikisho la soka hapa nchini, TFF, na Bodi ya Ligi, TPLB, wakaiga moja ya nafasi hizi kama zilivyo kwa CAF...nafasi ya mratibu mkuu wa mchezo!

Kwenye kila mchezo huwa na huyu mtu wa kuitwa mratibu wa mechi ambaye anatoka makao makuu kwa sababu ndiyo waliopata mafunzo ya CAF.

Mtu huyu anapewa heshima kubwa kuliko hata mwamuzi wa mchezo.

Chukulia mchezo unafanyika Mwanza, mratibu atatoka Dar es Salaam na atasafirishwa kwa ndege na kulipiwa kila kitu huku akipewa laki sita kwa siku kama posho.

Mwamuzi wa kati atapanda basi, tena kwa nauli yake halafu atarudishiwa baadaye.

Kisha atapewa shilingi laki tatu na nusu kwa safari nzima.

Na huyo ni mwamuzi wa kati, lakini mwamuzi msaidizi ni pungufu ya hapo.

Hivi nani aliwaambia wasimamizi wa soka letu kwamba mpira wetu haiwezi kufanikiwa bila mratibu wa mechi...na anaratibu nini hasa?

CAF wamemuweka huyo mtu kutokana na mfumo wao sasa wa kujiendesha ikiwemo kile kituo kikuu cha usimamizi wa mechi...TFF na Bodi ya ligi hawana.

Sasa huyo mratibu analeta maajabu gani...anaripoti kwa nani?

Wakati TFF na Bodi ya Ligi wakitengeneza nafasi hizi za mchongo kwa wakuu wao pale Karume, wenzetu Zambia wanafunga VAR katika kila kiwanja ili kutoa haki.

Wenzetu wanaita vitu ambavyo vitaleta manufaa ya moja kwa moja kwenye mpira, sisi tunaiga vitu ambavyo vinaongeza gharama isiyo na maana yoyote.

Mpira wa Zambia unaingiza pesa ndogo zaidi kulinganisha na Tanzania, lakini wenzetu wanafanya mambo makubwa zaidi kuliko sisi.

Ligi ya Zambia inaonyeshwa na DSTV kwa mkataba wa dola milioni moja kwa mwaka.

Ligi ya Tanzania inaonyeshwa na Azam TV kwa mkataba wa dola milioni kumi kwa mwaka.

Yaani ligi ya Tanzania imeiacha mbali sana kwa mapato ligi ya Zambia, lakini wao wanaweka VAR, sisi tunaongeza posho kwa waratibu.

Kupanga ni kuchagua, wenzetu wamechagua maendeleo sisi tumechagua kupeana posho.

Hivi kati ya mratibu wa mechi na VAR ni nini kinaleta maendeleo kwenye mpira?

Wenzetu Zambia licha ya fedha ndogo wanayoingiza kwenye mpira, lakini wanaitumia vizuri sana kwa ajili ya maendeleo...sisi tunaoingiza fedha nyingi tunaishia kuzitafuna kiujanja ujanja tu.

Na hii ndiyo tofauti ya sisi na wenzetu wanaotuzidi. Ni katika kuchagua vipaumbele vya uwekezaji.

Tunawekeza kwenye nini katika wakati gani...ndiyo shida yetu!

Sisi tunaweza kupoteza muda kuhangaika na vitu vya kawaida sana na kuacha vitu vya msingi ambavyo vingeweza kutuvusha hapa tulipo.

Hebu angalia uchaguzi wa wachezaji wa timu ya taifa.

Himid Mao, kiungo anayecheza ligi ngumu ya Misri huku akipata namba, anaachwa na kuchukuliwa Mzamiru Yasini ambaye hapati namba kwenye timu yake ya Tanzania.

Tunatafuta ushindi kwenye mechi ngumu, anaingia Nickson Kibabage kama winga huku Idd Nado ambaye ni mzawa aliyefanya vizuri zaidi kwenye ligi yetu msimu uliopita, akiachwa benchi.

Tumerogwa sisi...siyo bure!