MZEE WA UPUPU: Tujiandae na fainali ijayo Azam Shirikisho

Msimu wa soka Tanzania umemalizika kwa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports mjini Kigoma. Tangu 2017, fainali ya mashindano haya imekuwa ikizinguka katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikianza na Dodoma, Arusha, Lindi, Rukwa na sasa ilipigwa Kigoma.

Ni wazo zuri kuipeleka fainali hii katika mikoa mbalimbali kwa sababu inasaidia kuufanyia promosheni mpira. Lakini pia inaiunganisha zaidi nchi kwani maingiliano baina ya mikoa na mikoa yanakuwa makubwa wakati wa fainali hizi, kama ambavyo imeshuhudiwa katika miaka yote.

Lakini, faida hizi zinakuja kwa gharama kubwa ya mchezo mzuri...haipaswi kuwa hivyo. Mara zote tunapofikiria jambo lolote kuhusu mpira, swali la kwanza kujiuliza ni ‘tunausaidia mpira?’

Kuipeleka fainali kubwa kama hii katika mkoa kama Kigoma ambao haukujiandaa, ni kuuhujumu mpira badala ya kuusaidia.

Kigoma ni kama haikujiandaa. Timu zinazocheza fainali zinakosaje uwanja wa mazoezi? Yaani ukiacha Uwanja wa Lake Tanganyika ambao ndiyo ulikuwa unaandaliwa kwa fainali, Kigoma haikujiandaa na jambo lingine lolote.

Ni kama mkoa haukuwa na viongozi wa soka ambao wanalijua soka. Samahani kwa hilo. Yaani inapofikia wakati mkoa unakosa uwanja wa mazoezi, unajiuza ‘hapa kuna mpira kweli?’

Uwanja pekee ambao uliokuwepo na wanafainali walifanyia mazoezi pamoja haukuwa na hiyo hadhi. Shida sana. Hapo hatuusaidii mpira, tunauhujumu. Tunaisaidia zaidi siasa kuliko mpira.

Viongozi wa TFF wanahesabu fainali kuchezwa katika mikoa mbalimbali ni mafanikio kwao, lakini mpira haufanikiwi. Tabu ambazo waliocheza nusu fainali Tabora na Songea, na hawa waliocheza fainali Kigoma walikutana nazo, hazielezeki.

Fainali ya mashindano makubwa kama haya hutakiwa kufanyika kwenye uwanja mzuri katika mji uliojipanga. Fainali zote za mashindano haya, ukiacha ile ya kwanza 2016 zimefanyika kwenye viwanja vibovu na miji ambayo haikujiandaa.

Na anayesababisha yote haya ni TFF, waandaaji wa mashindano. Kwanini wasitangaze sasa mji ambao fainali ijayo itafanyika? Wanaweza kutangaza hata fainali za miaka mitatu ijayo na kazi ikabaki kwa wanaojiandaa tu.

Kombe la Dunia wanafanya hivyo, Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) wanafanya hivyo na hata Ligi ya Mabingwa Ulaya wanafanya hivyo. Hao ni watu ambao viwanja vyao viko tayari muda wote. Wanaweza kuamshana usiku wa manane kwamba kesho ni fainali, na wakapata viwanja zaidi ya 100 ambavyo viko tayari.

Lakini bado wanatoa muda wa mwandaaji wa fainali kujiandaa vizuri. Hii ni kwa sababu fainali siyo tu zile dakika 90 za kuupiga mateke mpira ndani ya uwanja, ni mzunguko wote wa maisha wakati wa kipindi husika.

Tangaza kabisa sasa kwamba fainali ya 2022 itafanyika mkoa fulani na masharti ni lazima kuwe na uwanja wenye sehemu nzuri ya kimataifa ya kuchezea. Lazima kuwe na viwanja vya mazoezi angalau viwili kwa ajili ya hizo timu.

Kuwe na miundombinu mizuri ya kukarimu wageni. Kigoma ilizidiwa, hoteli hazikutosha. Fanya hivyo kwa fainali tatu zijazo, 2022, 2023 na 2024.

Baada ya fainali ya msimu ujao, tanganza tena fainali ya 2025. Hii itasaidia mikoa kujipanga na fainali kupata heshima inayostahili ya kimpira, siyo ya kisiasa.

Ni hizi sababu za kisiasa ndizo zinazosababisha mashindano ya Kagame kufanyika hapa nchini. Viongozi wa TFF wamepambana kuhakikisha mashindano haya yanakuja Tanzania kwa sababu Azam TV wameahidi pesa nzuri.

Azam TV hawataki kuona mashindano yanafanyika nchini bila timu za nyumbani kushiriki. Na hawataki kutoa mzigo mkubwa kama yatafanyika nje ya Tanzania. Hicho ndicho kilichowatoa roho wakuu wa Karume, lakini hawaangalii sababu za kimpira kwamba sisi Tanzania wachezaji wetu hawajapumzika.

Msimu wa soka ndiyo tumeumaliza Julai 25, halafu Agosti Mosi, Kagame inaanza, maana yake timu hazijapumzika kabisa. Septemba 10 mashindano ya CAF na baadaye Ligi Kuu inarejea.

Hapo tunataka kuzilinda nafasi zetu NNE za CAF kwa timu zetu kufika mbali.

Zitafikaje kama wachezaji hawajapewa muda wa kupumzika? Lakini kwa kuwa viongozi wanazikumbatia sababu zinazoleta mashindano haya siyo za kimpira, basi yanakuja tu.

Ni kweli kwamba Kombe la Kagame ni muhimu kwa maendeleo yetu ya kisoka katika huu ukanda, lakini tujiangalie sisi kwanza. Tusitafute ufahari wa mshumaa kwa kujiangamiza wenyewe.

Haitakuwa ajabu kuona timu zikitumia U-20 kwenye mashindano haya ili kuwalinda nyota wao kwa ajili ya msimu ujao. Kwa hiyo Kagame Cup inaweza ikashuhudia wachezaji wenye majina madogo, hivyo kuyapoozesha.

Na hii ni kuharabu mashindano yenyewe, ni bora tu yasingefanyika. Ingeeleweka zaidi kuliko hii lipua lipua ya kisiasa. Inaonyesha ni namna gani hatujiandai na mambo yetu. Kila siku sisi ni watu wa kukurupuka tu. Na hii ni Afrika nzima, siyo Tanzania tu.

Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake yalipangwa kufanyika kuanzia Julai 17. Mashindano ambayo yalipangwa kufanyika kikanda, kanda Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yalitakiwa kufanyika Nairobi.

Wakati timu zikijiandaa na zingine zikiwa tayari zimewasili Nairobi, ikatoka taarifa kwamba yameahirishwa hadi itakapopangwa tena. Mashindano haya yaliahirishwa siku tatu kabla hayajaanza.

Unajua kisa ni nini? Kumbe baada ya uchaguzi mkuu wa CAF ulioleta viongozi wapya kina Motsepe maisha yakabadilika. Kina Motsepe wakaja na fagio la kuondoa watu wote walioonekana ni chembechembe za utawala wa Ahmad Ahmad.

Hii ikamhusu hata mtu wa CAF aliyekuwa akiratibu mashindano haya. Kwa hiyo watu wapya wakawa hawajui waanzie wapi.

Na kwa kuwa fungu la kuendesha mashindano haya lilitakiwa kutoka CAF, likashindwa kutoka kwa sababu walioingia hawakujua waanzie wapi. Kuja kutahamaki mashindano haya hapa. Tunafanyaje? Tuahirishe kwanza tujipange.

Unaweza ukashangaa kwa CAF kuwa katika hali hii, lakini nani anaunda shirikisho hilo? Ni hawahawa viongozi ambao wanashindwa kujipanga vizuri kuandaa fainali moja tu ya ASFC. Ni hawa viongozi ambao wanakurupuka kuandaa Kagame Cup. Kwa hiyo tarajia madudu mengi tu huko CAF, kama yanayotokea hapa.