MZEE WA UPUPU: Samatta hatutendei haki

MZEE WA UPUPU: Samatta hatutendei haki

NCHINI Ethiopia watoto wengi, kama siyo wote, wana ndoto siku moja kuwa wanariadha wakubwa duniani. Iwe jijini Addis Ababa, Bahr Dar, Adama, Awassa, Hawassa na hata Dire Dawa.

Asubuhi na mapema utakutana nao barabarani wanakimbia wakifanya mazoezi. Unajua kwanini? Sababu ni moja tu, KENENISA BEKELE. Ni nani huyu?

Kenenisa Bekele ni mwanariadha raia wa Ethiopia mshindi mara mbili wa medali ya dhahabu ya Olimpiki kwa mbio ndefu za mita 5000 na 10000. Alishikilia rekodi ya dunia ya mbio za mita 5,000 kuanzia mwaka 2004 hadi 2020.

Na pia alishika rekodi ya dunia ya mita 10,000 kuanzia mwaka 2005 hadi 2020. Alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 na 10,000 kwenye Olimpiki ya Beijing 2008.

Lakini kabla ya hapo alishinda medali ya dhahabu ya mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki ya Athens mwaka 2004. Pia alishinda medali ya fedha kwenye mbio za mita 5000. Kwa jumla, Bekele ameshinda katika mashindano 26 yenye hadhi ya dunia.

Mafanikio haya yakamfanya kuwa maarufu sana nchini kwao kwani vyombo vya habari vyote, vya nje na ndani vililipamba jina lake kila wakati. Lakini kama unadhani hiyo ndiyo inawafanya watoto watamani kuwa wanariadha, basi bado hujapata picha kamili.

Kenenisa Bekele aliyageuza mafanikio haya ya medali na mataji kuwa kitu cha kujivunia nyumbani kwao kwa kufanya uwekezaji mkubwa. Katikati ya Jiji la Addis Ababa, kwenye Mtaa wa Cameroon katika kitongoji cha kifahari cha Bole Medhanialem Cathedral, Bekele amejenga hoteli kubwa ya kifahari ya ghorofa nane.

Hoteli hiyo iliyofunguliwa 2013, ilijengwa kwa gharama ya Birr 200 milioni za Ethiopia sawa na zaidi ya Sh800 bilioni za Tanzania. Ni hoteli hii na uwekezaji mwingine mwingi alioufanya ndiyo unaowatia kichaa watoto wengi wa Kiethiopia kutaka kuwa wanariadha.

Kila mtoto anaamini kupitia kukimbia kama Bekele anaweza kubutua kombolela kwa familia yake na kuikomboa.

Hiki ndicho kitu anachotunyima Mbwana Samatta. Huyu ndiye nyota wetu wa soka aliyefanikiwa zaidi katika historia ya nchi hii. Alifanikiwa Afrika na akaenda kufanikiwa Ulaya akicheza hadi kwenye ligi maarufu zaidi duniani, EPL.

Kwa kufanya hivyo, Samatta amekuwa mfano mzuri sana kwa watoto wetu wanatamani kuwa wanasoka wakubwa. Lakini hiyo pekee haitoshi kuwafanya wakeshe viwanjani kutamani kuwa Samatta.

Mbwana alitakiwa atufanyie jambo kubwa sana la uwekezaji litakalokuwa mfano kwa kila mtoto, kama Kenenisa Bekele. Afungue mradi mmoja mkubwa ambao utamuingizia pesa yeye binafsi na kumfanya kuyatawala maisha baada ya kustaafu soka, lakini pia utakuwa mfano kwa watoto wetu.

Samatta anatakiwa akirudi nchini kupumzika baada ya misukosuko ya msimu huko Ulaya, Tanzania ijue nyota wake mkubwa wa soka amerudi.

Samatta anatakiwa atingishe kama Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’ anavyotingisha kwenye Bongofleva.

Diamond anayaweka wazi mafanikio yake kiasi cha kuwafanya watoto wengi watamani kuwa wanamuziki. Wanatamani kuwa kama yeye. Samatta atufanyie hivyo. Kwanza itasaidia kuinua uchumi wa nchi, wake mwenyewe na kuamsha ari ya watoto kutamani kuwa wanasoka wakubwa.

Mwenye namba ya Samatta, amshtue.