MZEE WA UPUPU: Mpira unavyowaunganisha Wazambia

ZAMBIA ni moja kati ya nchi zenye matatizo makubwa sana ya mawasiliano miongoni mwa wananchi wake. Ikiwa na mikoa kumi tu, Zambia ina makabila zaidi ya 70 huku ikiwa haina lugha moja inayounganisha taifa zima.

Badala yake kuna makabila saba ambayo yamepewa hadhi ya kuwa lugha za taifa na yanatumika kufundishia shuleni katika maeneo husika. Makabila hayo ni Bemba, Nyanja, Tonga, Lozi, Lunda, Luvale na Kaonde.

Kiingereza ndiyo lugha kuu ya taifa, lakini kwa bahati mbaya, siyo watu wote wanaokijua zaidi ya wasomi na watu wa mijini kwa namna moja au nyingine.

Hii ni kwa sababu kabla ya kujua Kiingereza ukubwani watoto huanza kujua makabila yao katika mikoa husika.

Wakati wa kampeni za urais zilizomalizika hivi karibuni kuna baadhi ya maeneo ilibidi wagombea watumie wakalimani kufikisha ujumbe wao. Mgawanyiko huu umeligawa taifa vipandevipande na kuwafanya watu wasiwe wamoja kama kaulimbiu yao inavyotaka taifa liwe ‘One Zambia, One Nation’ yaani Zambia moja, taifa moja.

Kwa hiyo ili kuwaunganisha watu na kuwafanya wajihisi kitu kimoja, serikali imekuwa ikiutumia mpira kama silaha kuu miaka na mikaka. Mpira unawasahaulisha Wazambia tofauti zao za lugha na makabila na kujikuta wakizungumza lugha moja ambayo ni mpira.

Chipolopolo kama timu ya taifa ndiyo kinara namba moja katika kuwaunganisha Wazambia kama taifa. Na hii ni tangu enzi za mwasisi wa taifa hilo.

Wahenga watakumbuka Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Hayati Dk Kenneth Kaunda alivyokuwa karibu na mpira kiasi kwamba hata timu ya taifa iliitwa KK Eleven.

Ili kupata timu imara ya taifa, ni lazima uwe na ligi imara ya taifa. Serikali kuu na taasisi zake, imesimama mstari wa mbele kuhakikisha kunakuwa na ligi bora itakayozalisha wachezaji bora kwa ajili ya timu bora ya taifa.

Wakati Tanzania ina uwanja mmoja tu mkubwa ule wa Benjamin Mkapa, Zambia wanavyo viwili kama hivyo; Heroes wa Lusaka na Levy Mwanawasa uliopo Ndola.

Mradi wa Uwanja wa Heroes ni sawa na wetu wa Mkapa, yaani ulijengwa pembeni ya uwanja wa Uhuru- na wao hivyohivyo.

Na kupitia taasisi zake, serikali imekuwa ikimiliki timu kadhaa au ikizidhamini moja kwa moja kuanzia Ligi Kuu hadi madaraja mengine ya chini. Kwa mfano katika timu 18 zilizoshiriki Ligi Kuu msimu uliopita timu 16 zilikuwa zikimilikiwa au zikidhaminiwa moja kwa moja na taasisi za umma.

Zesco United ni timu ya Shirika la Umeme Zambia ambalo ni sawa na Tanesco kwa Tanzania. Zanaco ni timu ya Benki ya Taifa ya Biashara nchini humo, sawa na NBC nchini Tanzania. Ilianzishwa 1978 na imeshinda Ligi Kuu mara saba.

Red Arrows - hii ni timu ya Jeshi la Anga la Zambia sawa na Airwing kwa hapa Tanzania. Kabwe Warriors timu ya wananchi inayodhaminiwa moja kwa moja na Shirika la Reli Zambia. Ipo pia Green Eagles timu ya Jeshi la Kujenga Taifa Zambia (Zambia National Service), kama ilivyo kwa JKT hapa nchini.

Kuna timu ya Prison Leopards - timu ya Jeshi la Magereza kama ilivyo Tanzania Prisons hapa nchini. Ipo Nkwazi FC timu ya wananchi inayodhaminiwa moja kwa moja na Jeshi la Polisi Zambia, ilhali Green Buffaloes ni timu ya kikosi cha ardhini cha Jeshi la Zambia .

Vilevile kuna timu ya Power Dynamos ambayo ni timu ya Shirika la Taifa la Umeme Migodini, huku Forest Rangers ikiwa ni timu ya Mamlaka ya Taifa ya Misitu Zambia, ambapo Nkana FC ni ya mgodi wa shaba wa Mopani.

Nyingine ni Young Green Eagles iliyoanza kama akademi ya Green Eagles baadaye ikasimama yenyewe, lakini bado ni timu ya Jeshi la Kujenga Taifa, huku Napsa Stars ikiwa ni timu ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii kama NSSF hapa Tanzania.

Ipo Lumwana ambayo ni timu ya Mgodi wa Shaba wa Lumwana na Indeni FC inadhaminiwa moja kwa moja na kampuni ya taifa ya kusafisha mafuta ghafi kama iliyo Tiper ya Tanzania. Ni timu tatu tu; Lusaka Dynamos, Kitwe United na Buildcon FC ndizo hazikuwa zikimilikiwa na taasisi za umma au kudhaminiwa.

Taasisi hizi za umma huwekeza vya kutosha kwenye mpira kiasi cha kuzifanya timu kuwa imara vya kutosha. Hadi Bunge la Zambia lilikuwa na timu ambayo ilishiriki Ligi Kuu ambayo ilishuka daraja msimu wa 2019/20 na sasa iko Daraja la Kwanza.

Japokuwa Zambia hakuna timu zenye uwezo wa kifedha kulinganisha na klabu tatu za Tanzania Simba, Yanga na Azam zinapokuwa kwenye ubora wao, lakini hakuna timu zenye njaa kama zile za Tanzania zinazofuata baada ya zile tatu kubwa.

Ili kuelewa zaidi hapa, nitumie mfano ufuatao. Kuna kijiji kimoja kina watu watatu wana magari na kingine hakina hata mtu mmoja ana gari, lakini wote wana pikipiki. Ni kijiji kipi kina unafuu wa usafiri?

Sasa vijiji hivi ni sawa na Tanzania na Zambia. Tanzania kuna timu tatu kubwa zenye pesa nyingi sawa na yale magari, na Zambia ni kile kijiji ambacho hakina gari lakini kila mwanakijiji ana pikipiki.