Muda wowote wanatua....

Mpole: Watajua hawajui

IMEBAKIA mizunguko minne kabla ya Ligi Kuu Bara kumalizika, huku baadhi ya timu zikianza maandalizi ya msimu ujao hasa usajili.

Kuna baadhi ya nyota kutoka ndani na nje ya nchi wamezivutia baadhi ya timu na wameonyesha nia ya kuwataka ikiwemo kufanya nao mazungumzo kwa usiri mkubwa.

Miongoni mwa timu zilizoanza maandalizi ya msimu ujao ni vinara wa ligi, Yanga ambao wameonekana kuanza kwa kasi usajili kwa kulitumia benchi la ufundi, huku wakiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Usajili, Injinia Hersi Said.

Simba na Azam sio kama wapo kimya nao kila mmoja kwa njia yake ameanza mipango ya kuboresha kikosi chake kwa kuingia sokoni kufuatilia baadhi ya wachezaji waliovutiwa nao na tayari kuna tetesi za kuwanasa baadhi ya nyota hao.

Hawa hapa ni miongoni mwa nyota wanaohusishwa na timu mbalimbali nchini.

Miongoni mwa nyota hao wanaohusishwa na Simba na Yanga wapo winga wa Asec Mimosas, Stephano Aziz Ki na winga wa USGN, Victorien Adebaryo.


Stephano Aziz Ki

Simba na Yanga walikuwa wanamuwania winga kutoka Asec Mimosas, Stephano Aziz Ki, lakini inadaiwa Yanga wamefanikiwa kumpa mkataba wa miaka miwili na kinachosubiriwa ni kumtangaza.

Hivi karibuni wakati Yanga ikipambana na dili hilo, ilielezwa kwamba Simba nao wameingia kwa kasi huku wakipandisha dau lake, lakini masharti aliyotoa mchezaji huyo ndiyo yalikuwa kikwazo kumpata.


George Mpole

Huyu ni straika wa Geita Gold mwenye mabao 15 hadi sasa moja zaidi ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele (kabla ya mchezo wa jana wa Yanga dhidi ya Cpastal Union) na hadi juzi ilidaiwa kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili Msimbazi huku Yanga wakielezwa kuwa na mipango naye.

Mpole lilikuwa ni chaguo la aliyekuwa kocha wa Simba, Pablo Franco ambaye ametimuliwa, lakini bado mabosi wa Simba waliona inafaa mshambuliaji huyo kuongezwa kikosini, hivyo kuamua kumpa mkataba kama inavyodaiwa.

Inaelezwa mmoja wa vigogo wa juu Simba anavutiwa na uwezo wa Mpole kwenye kufunga mabao na anataka awepo kikosini msimu ujao.


Azizi Andambwile

Matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam FC wameulizia uwezekano wa kupatikana kwa kiungo mkabaji Andambwile anayekipiga Mbeya City na amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya timu hiyo msimu huu.

Andambwile mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na mshambuliaji amekuwa katika kiwango bora muda wote kwenye mechi za Mbeya City, na amefanya hivyo hata katika michezo mikubwa dhidi ya Simba, Yanga na Azam msimu huu.

Mbali na timu hizo, mchezaji huyo pia amewashawishi mabosi wa Singida Big Stars (zamani DTB) ambao wamepanda kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ambao wameonyesha nia ya kumsajili.

Ubora aliouonyesha Andambwile umewavutia mabosi wa Azam na huenda mwisho wa msimu huu asiwepo katika kikosi cha Mbeya City na akaonekana katika mitaa ya Chamazi, Jangwani au Msimbazi.


Cleophas Mkandala

Kocha Pablo kabla ya kutimuliwa aliandaa ripoti yake kwa mabosi wa Simba ambayo ndani yake aliweka jina la Mkandala kwa ajili ya kumsajili msimu ujao, hivyo halitakuwa jambo la kushangaza jina la kiungo huyo wa Dodoma Jiji kuwepo kutokana na kuvutiwa naye.

Mkandala alilivutia benchi la ufundi Simba kutokana na uhitaji wa kiungo mwenye uwezo wa kushambulia. Hata kama watasajili nyota wa kigeni, ila Mkandala atakuwa miongoni mwa wapya kutokana na kuvutiwa kwa aina yake na uchezaji wa kushambulia, kuanzisha mashambulizi, kufunga mabao na kukaba kwake.


Dickson Mhilu

Beki huyu wa kulia wa Kagera Sugar mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu, hivyo atakuwa mchezaji huru, lakini ni miongoni mwa nyota wanaotajwa kuondoka kwenye timu hiyo. Kumekuwapo na ushawishi mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Kagera Sugar ili kumbakiza misimu mingine miwili, ingawa inadaiwa mwenyewe amegoma kwani anataka kupata changamoto mpya.

Inaelezwa sababu kubwa inayompa ari ya kujiamini Mhilu ni uwepo wa dili lenye maslahi mazuri mezani kwake kuhitajika na Namungo FC ilioonyesha nia ya kumtaka kabla ya mzunguko wa kwanza kumalizika.

Kama mambo yatakwenda vizuri, basi Mhilu anaweza kuwa miongoni mwa nyota wa kwanza kusajiliwa Namungo inayopambana kumaliza katika nafasi za juu msimu huu kwenye msimamo wa ligi.