MTU WA PWANI: Azam ilikikosa inachokipata kwa Zaka Zakazi

Muktasari:

KUNA mwanadamu mmoja pale Azam FC huwa hawapi nafasi ya kupumua mashabiki wa Simba na Yanga na hata wasemaji wa klabu hizo kwa nyakati tofauti.

KUNA mwanadamu mmoja pale Azam FC huwa hawapi nafasi ya kupumua mashabiki wa Simba na Yanga na hata wasemaji wa klabu hizo kwa nyakati tofauti.

Anaitwa Thabit Zakaria maarufu kama Zaka Zakazi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo.

Kuna wakati aliwahi kuwa gumzo kutokana na alivyokuwa akirushiana tambo na kejeli na aliyewahi kuwa Msemaji wa Simba wakati huo ambaye katimkia upande wa pili, yaani Haji Manara.

Pia kwa muda tofauti amewahi kuwa kwenye vita ya maneno na Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ingawa sio vita inayoumiza kwani nje ya majukumu yao hao jamaa ni marafiki wakubwa.

Siku chache zilizopita mabosi wa Azam FC waliamua kuonyesha jeuri yao ya fedha mbele ya vigogo vya soka nchini Yanga na Simba kwa kuamua kulinunua na kulileta hapa nchini basi la kifahari aina ya Scania Irizar ambalo litakuwa linatumiwa na timu yao katika safari mbalimbali.

Ni basi la kifahari kweli ambalo thamani yake ni zaidi ya Sh900 Milioni, fedha ambayo ingeweza kutengeneza uwanja wa soka kama ule wa Gwambina Stadium kule Misungwi mkoani Mwanza.

Sasa alichokifanya Zaka Zakazi ni aliratibu msafara wa baadhi ya maofisa wa klabu hiyo akiwemo yeye mwenyewe kwenda hadi Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia kwa ajili ya kulipokea basi hilo

Na haikuishia kulipokea tu bali pia basi hilo lilitembezwa taratibu katika miji mbalimbali ya njiani na kuruhusu watu kupiga nalo picha ambazo nyingi zilisambaa katika mitandao ya kijamii ya vyombo mbalimbali vya habari na pia watu binafsi.

Kusambaa huko kwa picha za basi la Azam kukaibua mijadala mingi ya watu mbalimbali, wengine wakizungumzia thamani yake, matumizi yake na baadhi hasa mashabiki wa Simba na Yanga wakawa wanaibeza timu hiyo kwa kununua basi la thamani kubwa na kuwaringishia huku ikiwa haifanyi vizuri na mashindano mengine ambayo imekuwa ikishiriki.

Lakini wapo ambao wamesimama upande wa Azam na kuipongeza kwa kununua basi hilo na kisha kulitembeza huku likipambwa kwa sifa nyingi kwa vile ilikuwa inakuza hadhi na thamani ya klabu hiyo.

Haya yote ni matokeo ya ubunifu wa idara ya habari na mawasiliano ya Azam chini ya Zaka Zakazi ambaye tangu alipojiunga na klabu hiyo, kuna hatua kubwa imepiga katika masuala ya habari na mawasiliano.

Anachokifanya Zaka Zakazi ni kitu ambacho klabu ya Azam ilikuwa inakikosa kwa muda mrefu katika medani ya soka hapa nchini na kujikuta kila kukicha inaachwa mbali na Yanga na Simba.

Azam walikuwa wanakosa mtu wa kuifanya izungumzwe na ijadiliwe na wapenzi, mashabiki na wadau wa mpira wa miguu hapa nchini.

Chapa ya Azam ilijikuta ina unyonge mbele ya vigogo hivyo na ilikosa ushawishi wa kujadiliwa kwa mazuri ambayo imekuwa ikiyafanya na mara kwa mara mijadala michache ambayo ilikuwa inaihusu ni ile yenye taswira hasi ambayo haiipi sura nzuri nembo ya klabu hiyo.

Lakini, Zaka Zakazi amesimama imara na kuitetea Azam pasipo kujali mashambulizi, tambo au kejeli kutoka kwa watu wa Simba na Yanga ambao daima wanaamini timu zao zinapaswa kusemwa kwa mazuri na hakuna nyingine inayostahili kusifiwa na sifa mbaya ndizo zinapaswa kwenda kwa timu zisizo zao.

Kwa muda mrefu, Azam walihitaji mtu wa aina ya Zaka Zakazi ambaye yuko tayari kujitoa mhanga na kupambana na vilivyo na Simba na Yanga katika kuifanya ‘brand’ ya Azam inakuwa mjadala mkubwa katika nchi.

Utamaduni wa soka letu unahitaji watu aina ya Zaka Zakazi ili waifanye klabu izungumzwe jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linasaidia kuvutia wadhamini.

Kuzuka kwa mijadala ya mapokezi ya basi na uzungushwaji wake katika miji mbalimbali hadi linafika pale Azam Complex Chamazi, ni dalili za muelekeo wa mafanikio ya Azam katika harakati za kuipandisha thamani yake.

Chapa isiyojadiliwa na kujulikana haiwezi kukua na kupata heshima na thamani stahiki. Zaka Zakazi taratibu anaanza kuwatimizia ndoto waliyokuwa wakiiota kwa muda mrefu. Ile ya kuwa habari kubwa ya mara kwa mara katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.