MTU WA MASHABIKI: Mzee Mpili kawajaza mkajaa mazima

Muktasari:

SITAKI kuamini mnachoamini. Nilipita hapo kwenye Kijiwe cha Kahawa juzi nikabishana na nyie sana,nikaona mnanipotezea muda nikasepa zangu.

SITAKI kuamini mnachoamini. Nilipita hapo kwenye Kijiwe cha Kahawa juzi nikabishana na nyie sana,nikaona mnanipotezea muda nikasepa zangu.

Yanga haikushinda kwa sababu ya Mzee Mpili. Mi nawashangaa sana na nitaendelea kuwashangaa kama mtakuja Kigoma mkimfikiria yule mzee. Ni mjanja mjanja tu yule, yaani kawajaza kidogo tu wote mkajaa. Kilichotokea kwenye ile mechi pale kwa Mkapa ni kwamba wachezaji wa Yanga walikataa unyonge. Wakapambana kulinda heshima yao ndani ya uwanja. Hilo tu. Basi. Hakuna maajabu ya mzee naniliu wala nini...

Lakini amewapa Yanga fundisho kwamba wanahitaji mtu fulani wa kuwajenga mashabiki wao kisaikolojia waipambanie klabu yao nje ya uwanja. Wajitoe kwaajili ya kuishangilia timu yao katika hali zote siyo wakati wa ushindi tu. Wawe nyuma ya viongozi na wachezaji wao muda wote. Wajazane viwanjani kushangilia timu yao, wanunue jezi, walipie kadi. Wachangie maendeleo ya klabu yao badala ya kubishana na Simba mitandaoni tu kutwa. Yanga ya sasa haina mtu wa hamasa au kuwajaza watu upepo wa kishabiki kama Mzee Mpili.

Lakini isifike mahali tukapuuzia juhudi wa kocha na wachezaji tukaanza kufikiria vitu vya ajabuajabu. Tuheshimu kazi za watu na tuache soka lichezwe uwanjani.

Simba nao wameamini kwamba Mzee Mpili ndiye aliyeicheza ile mechi waliyolala bao 1-0, jana nimeona wazee kibao pale stendi hata hawajavaa barakoa wanaenda Kigoma kupambana na Mzee Mpili. Dah! Kweli, tumefikia huku? Yaani leo hii wazee ni bora kuliko Bocco, Mugalu, Yacouba au Mauya? Tujifikirie, tuache hizi aibu. Ushabiki wa mitaani uishie jukwaani. Tusibeze kazi za wengine. Mi’ sidhani kama wachezaji wanajisikia vizuri wanavyoona kila sehemu wakitukuzwa wazee. Soka letu lilishavuka kwenye upuuzi huo. Twende na kasi ya mabadiliko, wahamasishaji wawepo lakini wasipuuze juhudi wa wachezaji wanaovuja jasho usiku na mchana mazoezini. Twendeni Kigoma tukaangalie mpira. Tusiwekeze akili zetu kwenye hizo imani ambazo hazitusaidii kufika popote. Miaka ya nyuma hizo ishu zilikuwepo kibao lakini zilisaidia nini zaidi ya kuliwa pesa tu? Mbona si Simba wala Yanga ambazo ziliwahi kubeba Kombe la Afrika au hata timu zetu za Taifa?

Jumapili tutulie tuangalie fainali. Mimi mwenyewe nina tiketi yangu, kesho ntakuwa kwenye treni. Tutaona mpira mkubwa sana Jumapili. Hao viungo watachapana sana viatu na ndio watakaoamua hii gemu kwavile tayari makocha wote waliona kilichotokea katika mchezo uliopita hakuna masihara tena safasi hii. Utapigwa mwingi sana pale kati.

Lakini naona kila dalili Simba ikianza na mastraika watatu huku Nabi akikomaa staili yake ile ile ya mmoja. Ingawa uwanja ni mdogo lakini kutakuwa na ladha ya aina yake ambayo pengine haijaonekana kwenye dabi za hivikaribuni. Vyombo vya usalama na mamlaka za soka ziweke mazingira mashabiki waone mpira bila bugudha. Mtanikuta jukwaa la mzunguko.