Msindo: Huyu Tshabalala mtu kwelikweli

Muktasari:

  • Msindo ni miongoni mwa mabeki wenye asisti nyingi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa nazo tatu, huku moja akitoa dhidi ya Simba

Kufanya mazoezi bila kuchoka na kujifunza kwa waliofanikiwa ni miongoni mwa mambo ambayo yamemfanya Pascal Msindo mwenye umri miaka 20 kuwa bora kiasi cha kutumika mara kwa mara kwa sasa kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC mbele ya Msenegali Cheikh Sidibe.

Msindo ambaye ni miongoni mwa mabeki wenye asisti nyingi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa nazo tatu, huku moja akitoa dhidi ya Simba amefichua hayo kwenye mahojiano maalumu ambayo alifanya na Mwananchi siku chache kabla ya mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, hivi karibuni.

Beki huyo wa kushoto anasema haikuwa kazi nyepesi kwake kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa Sidibe (24) ambaye alijiunga na matajiri hao wa Chamazi akitokea Teungueth FC kama mrithi wa Bruce Kangwa ambaye umri ulimtupa mkono.

"Kila kocha amekuwa na mambo ambayo huhitaji mchezaji kuwa nayo kwenye mfumo wake, nilijipa muda kwanza wa kujua nini ambacho kocha alikuwa akihitaji kutoka kwa mabeki wake wa pembeni. Nilianza kufanyia kazi hayo taratibu huku nikijisukuma mwenyewe kwa kufanya zaidi," anasema.

Beki huyo anasema: "Niliamini njia pekee ya kumshawishi mwalimu ni kufanya vizuri kwenye uwanja wa mazoezi huku nikisubiri wakati wangu ambao ataona nipo tayari kuanza kutumika kwa bahati nzuri haikuchukua muda kwakweli na tangu hapo nimekuwa nikipata nafasi."

Msindo alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Azam FC ambacho kilianza dhidi ya Simba akicheza na Lusajo Mwaikenda, Yannick Bangala na Yeison Fuentes kwenye ukuta wa timu hiyo huku golini akisimama Mohamed Mustafa aliyesajiliwa kutoka Al-Merrikh SC ya Sudan.

Yeyote freshi

Beki huyo anasema Azam FC ni miongoni mwa timu zilizokamilika, hivyo kila mchezaji huwa tayari kimchezo na mwenye njaa ya namba kama ilivyo kwenye vikosi vya Simba na Yanga.

"Ni ngumu kusema kwamba mchezaji fulani ndiye mwenye uhakika wa namba kwenye kikosi chetu, hutegemea na nani yupo tayari zaidi kimchezo lakini pia kingine ambacho huamua nani anaweza kuanza ni mpango wa mwalimu katika mchezo husika, sisi kama wachezaji jukumu letu huwa ni kuipambania timu tu," anasema.

"Kuna muda mwalimu anaweza kuamua kuanza na fulani na mechi inayofuata akafanya mabadiliko, kwetu kama wachezaji kila mmoja amekuwa akipambana kuwa tayari na jukumu ambalo atapewa. Nimekuwa nikifurahia hilo."

JKT noma
Msindo anasema mechi ngumu msimu huu kwenye ligi ilikuwa Desemba, mwaka jana dhidi ya JKT Tanzania, huku akieleza sababu ni namna ambavyo maafande hao walivyocheza kwa nguvu, hivyo iliwawia vigumu kupata ushindi kwenye mchezo huo uliochezwa Azam Complex.

"Ile ilikuwa mechi ngumu sana kwetu, walijua namna ya kutuzuia lakini tulipambana na kupata ushindi, nakumbuka tulianza kwa kuwatangulia na mimi ndiye niliyetoa asisti ya bao kwa Bajana, wakasawazisha ila katika dakika za mwishoni kabisa tukapata bao la ushindi," anasema.

Tshabalala acheni
Miongoni mwa wachezaji ambao Msindo anakubali kazi yao na amekuwa akijifunza kutoka kwao ni pamoja na Mohammed Hussein wa Simba ambaye amekuwa bora kwenye kikosi hicho hadi upande wa timu ya taifa la Tanzania 'Taifa Stars' kwa miaka mingi.

"Huwa napenda sana kujifunza kwa watu ambao wametangulia, vipo vitu vingi ambavyo vimekuwa msaada kwangu kutoka kwao, napenda kuwa bora katika kushambulia na kuzuia na ndivyo beki wa kisasa anatakiwa kucheza," anasema beki huyo.  

"Tshabalala amekuwa mfano mzuri wa kuigwa naamini wapo wachezaji wengi wachanga ambao wamekuwa wakimchukulia kama mfano hata upande wa nidhamu kiukweli yupo vizuri, nampongeza sana kwenye hilo."

Dabo anachomweleza

"Nashukuru Mungu nimekuwa nikipata nafasi ya kufanya mazungumzo na kocha (Dabo) kwa lengo la kujifunza zaidi. Amekuwa akinieleza mambo mengi kama mchezaji kijana ambayo natakiwa kuyazingatia kwa sababu malengo yangu ni kufika mbali natamani kupiga hatua zaidi," anasema.

"Kucheza soka la kulipwa Ulaya ni miongoni mwa malengo yangu. Najua kwamba sio kazi nyepesi natakiwa kuonyesha zaidi."


Alikotoka

“Napenda mpira tangu mdogo nilicheza sana mtaani na shule ya msingi. Pia pale Lupanga Sekondari kabla ya mwalimu Juma Michu kugundua kipaji changu na kunipeleka Moro Kids ambako nilipata misingi bora ya kucheza soka.

“Kwa wakati huo wazazi wangu walikuwa hawaniamini, ilikuwa vigumu kuniruhusu nikacheze mpira lakini nilipambana na kupata sapoti ya mwalimu Juma kuwashawishi wazazi kuwa mpira ni kazi kama kazi nyingine ndipo wakaniamini na kuanza kunisapoti,” anasema Msindo, mzaliwa wa Morogoro aliyelelewa katika kituo cha kukuza vipaji cha Moro Kids.

Azam walimfuata Moro

“Azam walikuwa na safari zao za mikoani kutafuta vipaji na walipokuja Morogoro nikaonyesha kiwango bora nikiwa na Moro Kids, uwezo wangu uliwavutia, baada ya hapo nikaambiwa nijiandae kuja Dar.

“Nilifanya taratibu zote na wazazi wakaniruhusu hivyo nikajiunga Azam nikiwa mwenye furaha sana kwani niliona naenda sehemu ambayo itanisaidia sana kutimiza malengo yangu,” anasema Msindo.

“Kiukweli maisha ya Azam ni mazuri kwani yananifanya nijifunze kila uchao pia yananijenga kuwa bora zaidi kutokana na miundombinu ambayo ipo hapa.”