MR LIVERPOOL: Nyakati nyingine unakubali wapinzani wazuri

WAKATI timu zinapokuja Anfield kwa ajili ya mechi za marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, jambo moja la kuangalia kujua kama kuna kitu au hakuna ni namna mechi inavyoanza.

Kama Liverpool ikianza vyema na kupata bao la mapema tena kama kuna mashabiki wa kutosha uwanjani, unajua kwamba hapo sasa shughuli ipo. Nimeona mechi za namna hii zaidi ya 10 katika kushabikia kwangu klabu hii. Ndiyo sababu, wakati nikiandika safu hii wiki iliyopita nilisema kwamba kama Liverpool itaanza vyema dhidi ya Real Madrid na kupata bao la mapema, mechi itakuwa ngumu kwa miamba hiyo ya Hispania.

Wakati Mohamed Salah alipokosa bao la wazi mwanzoni kabisa mwa mechi, halafu Thibaut Courtois akaokoa mchomo wa James Milner na kisha Gini Wijnaldum akapaisha shuti lake katika mazingira ambayo kulenga goli ilikuwa rahisi kuliko kupaisha, nikajua kwamba siku haikuwa yetu.

Kuna kitu katika mpira huwa hakina maelezo. Kuna siku unajua kwamba mambo hayatakuwa sawa.

Nakumbuka kuna mechi ambayo kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, aliwahi kusema kwamba alifahamu mapema kuwa atapoteza mechi kwa sababu hata harufu ya majani ya kiwanjani hayakuwa yakinukia ipasavyo.

Viko vitu katika soka ambavyo haviwezi kuelezeka kwa maneno ya kawaida, lakini kwa wanaojua wanajua.

Baada ya mechi dhidi ya Madrid juzi Jumatano, Jurgen Klopp, kocha wa Liverpool alisema bao alilikosa Salah mwanzoni mwa mechi katika hali ya kawaida angeweza kufunga akiwa amefumba macho.

Real Madrid ni timu yenye uzoefu mkubwa sana wa mechi. Nahodha wake, Karim Benzema, amecheza mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko jumla ya mechi ambazo Alisson Becker, Trent Alexander Arnold, Andrew Robertson, Ozan Kabak, Nathaniel Philips na Fabinho wamecheza kwenye mashindano hayo. Unawatazama Luka Modric, Casemiro na Toni Kroos na unaona unatazama watu ambao wamecheza mechi zote kubwa unazozifahamu; ile El Classico, Fainali za Kombe la Dunia, Fainali za UEFA na mechi kubwa zote unazozijua.

Kama zimebaki dakika 20 au 30 kabla mechi haijamalizika, wanajua tu nini wanastahili kufanya. Kama mnacheza kwa kasi wanajua namna ya kupoza mambo. Kama mnacheza taratibu wanajua namna ya kuongeza kasi. Wanajua dakika ngapi zitaongezwa mwishoni mwa mechi kabla hata kibao hakijanyanyuka. Wanajua miguu yao inaweza kukimbia wapi na wapi na wapi hawawezi kwenda.

Nilikuwa namtazama Modric na Kroos na sikumbuki ni mara ngapi walikimbia kuingia kwenye eneo la hatari la Liverpool. Wao walikuwa wanajiweka katika maeneo ambako endapo mpira utaporwa na wao kupasiwa, watapiga pasi moja au mbili za hatari kwa adui. Wala hawahitaji kukimbia huku na kule kama Wijnaldum. Wala hawahitaji kupiga makwanja kama Milner. Na wala hawahitaji kuangalia pembeni saa zote kama Fabinho.

Wanajua tu wako wapi na wanafahamu wanatakiwa kuwa wapi wakati fulani.

Liverpool imeishia katika hatua ya robo fainali msimu huu kwa sababu ya namna walivyocheza mechi ya kwanza kule Madrid. Kama wangecheza mechi ya kwanza kama walivyocheza mechi ya pili, huenda matokeo yangekuwa tofauti.

Nataka kuamini kwamba Real Madrid wamecheza na Liverpool katika wakati mzuri. Nilikuwa natazama takwimu za Liverpool kabla ya mechi ya juzi na nikaona kwamba katika mechi walizocheza Anfield mwaka huu wa 2021, wamepiga golini mashuti zaidi ya 120, lakini wamefunga magoli matatu tu.

Huu ni wastani wa kufunga magoli mawili katika kila mashuti 100 yanayopigwa langoni kwa adui. Si ajabu kwamba Salah anakosa magoli ambayo kwa kawaida angefunga akiwa kafumba macho na Gini anakosa magoli ambayo kufunga ni rahisi kuliko kukosa.

Na Bobby Firmino masikini. Bado ni mchezaji muhimu lakini nadhani kuna kitu hakiko sawa kichwani kwake. Anakosa magoli ya wazi na anafanya vitu ambavyo kwa kawaida si vyake. Firmino anapoteza pasi zaidi ya tano kwenye mechi moja?

Liverpool inawezeja kucheza mechi kubwa kama ya juzi pasipo Firmino kupiga hata pasi mpenyezo moja?

Sadio Mane ndiye mchezaji ambaye ananisikitisha zaidi sasa hivi. Kila anachofanya anakifanya anakifanya kuwa kigumu zaidi. Raha pekee niliyo nayo ni kwamba nafahamu kwamba mpira anaujua na kama unaujua, unaujua tu. Pamoja na yote, wakati mwingine tunatakiwa kunyanyua mikono juu na kusema dhidi ya Madrid katika mechi zote mbili, hatukuwa bora zaidi yao. Wamestahili kusonga mbele, tumestahili kuishi tulipoishia.


Imeandikwa na Ezekiel Kamwaga