MPAPASO WA MASAU BWIRE: Waamuzi, kuna tatizo gani?

MPAPASO leo umejielekeza kwa waamuzi wa soka namna wanavyozitafsiri sheria na malalamiko ya wadau kuhusu uamuzi wao.

Kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wapenzi, mashabiki na wadau wa mpira wa miguu nchini wakionyesha masikitiko kwa baadhi ya waamuzi kushindwa kuzitafsiri sheria 17 za soka.

Vitendo na matukio kwa baadhi ya waamuzi yanayoleta uamuzi wa utata katika baadhi ya michezo wanayochezesha imezua malalamiko na lawama kwamba wana makusudi ya kuzionea na kuzibeba baadhi ya klabu. Hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi wa klabu, wachezaji, mashabiki, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu nchini kukosa imani na matumaini ya kushinda mchezo kutokana na maandalizi na kuamini kwamba ushindi utatokana na matakwa ya uamuzi wa waamuzi wa mchezo husika.

Wadau wakikosa imani na idara nyeti ya waamuzi katika mpira wa miguu ni hatari kubwa katika maendeleo ya mpira wenyewe na athari zake ni kubwa, tena athari hasi. Msisimko wa mpira wa miguu utapungua, ushindani wa kweli utakosekana, maendeleo ya mpira wa miguu nchini kwa ujumla yatazidi kudorora na kushuka pakubwa.

Mengi yamezungumzwa na wadau kutokana na kasoro na upungufu unaovuka ule wa kibinadamu unaofanywa na baadhi ya waamuzi katika uamuzi wao. Wapo wanaodai wanapenyezewa kitu kidogo ili watoe upendeleo, huku wengine wakisema ni uwezo mdogo wa baadhi ya waamuzi wanaovurunda. Wengine wanadai baadhi ya waamuzi wamekuwa wakitoa uamuzi usio sahihi kutokana na mapenzi na ushabiki wao hasa kwa klabu za Simba na Yanga.

Wapo wanaodai ni kwa sababu ya michezo ya kubahatisha waamuzi nao siku hizi wanabeti au waliobeti na wenye michezo hiyo ya kubeti wanaweza kuwashawishi kusaidia kufanikisha matokeo mazuri upande waliobetia. Ni vigumu kuamini moja kwa moja hayo yasemwayo, lakini kutokana na matukio yanayotokea na kulalamikiwa na wengi, lazima kwa kiasi fulani tuamini kwamba inawezekana au nini hasa kinasababisha uhuni huo kufanyika kwenye mpira wetu. Ujue klabu zinatumia gharama kubwa katika maandalizi na kujiandaa kwa ajili ya ushindi na inapotokea mtu mmoja au wawili katika uamuzi wao wakapindisha ukweli inauma na inavunja nguvu na kukatisha tamaa. Upendeleo katika soka ni adui wa haki wote tuupinge kwa nguvu zote.

Kinachonisikitisha na kunihuzunisha zaidi ni pale ninaposhuhudia baadhi ya waamuzi walioaminiwa wenye beji za Fifa wao kuwa ndio wanakuwa vinara wa kuvurunda na kuadhibiwa. Tanzania tunao waamuzi watano wenye beji za Fifa na wasaidizi saba ambao pia wana beji hiyo ya Fifa. Waamuzi watano wenye beji za Fifa ni Heri Sasii, Ramadhan Kayoko, Ahmed Arajiga, Tatu Malogo na Frolentina Zabroni ilhali waamuzi wasaidizi ni Frank Komba, Sudi Lila, Mohammed Mkono, Fredinand Chacha, Kassim Mpanga, Janet Balama na Glory Tesha. Katika waamuzi hao watano wa Fifa mpaka sasa tayari wawili wamefungiwa kila mmoja miezi sita kwa kuvurunda na kuonyesha upungufu mkubwa katika uamuzi wao huku mwamuzi msaidizi mmoja alifikishwa katika kamati ya maadili na kupewa onyo.

Waliofungiwa ni Arajiga na Frolentina ambao waliharibu na kushindwa kuzitafsiri vizuri sheria 17 za soka katika baadhi ya michezo waliyochezesha.

Arajiga mchezo wa awali alioharibu na kulalamikiwa na wengi ulikuwa kati ya Azam na Yanga ambapo alidaiwa kuipa Yanga penalti ambayo haikuwa sahihi, na ambayo pia mpigaji hakuweza kufunga. Lakini pia katika mchezo huohuo ilidaiwa aliruhusu Yanga kucheza mpira uliokuwa umetoka nje na kufunga bao na kufanya umalizike kwa sare ya 2-2. Pia mwamuzi msaidizi Komba alipewa onyo kwa uamuzi wake kwenye mchezo huo.

Mechi nyingine aliyovurunda Arajiga, mwamuzi bora msimu wa Ligi Kuu 2021/22 ni kati ya Tanzania Prisons na Simba. Anadaiwa kuikataa penalti halali ya Simba, lakini akaruhusu Simba kucheza mpira ambao tayari ulikuwa umetoka nje ukasababisha bao na kufanya mpira huo umalizike kwa sare ya bao 1-1. Lakini Sasii amelalamikiwa na Watanzania wengi kwa madai ya kuwapa Azam penalti dhidi ya Ruvu Shooting ambayo haikustahili. Bado wadau wanasubiri Kamati ya saa 72 itasema nini kutokana na tukio hilo. Ni wakati kwa baadhi ya waamuzi wanaokiuka sheria kwa kuzitafsiri ndivyo sivyo kuacha tabia hiyo. Watende haki kwa klabu zote washindi wapatikane kwa uwezo na siyo kubebwa na wao. Pia TFF na Bodi ya Ligi wachukue hatua na kutoa adhabu kali kwa waamuzi wanaofanya vitendo vya upendeleo na uonevu.