Mnyama alivyopenya CAF

HOROYA AC ya Guinea walichapika haswa juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa pale Temeke. Walipigika hasa. Unapoona kiungo wa chini, Sadio Kanoute akiondoka uwanjani na mabao mawili ujue wapinzani walikuwa katika maisha magumu. Na kweli. Horoya walipigika haswa na hawatakuja kusahau.

Simba waliingia uwanjani kusaka ushindi wa aina yoyote ile, lakini wakajikuta wakiingia katika historia ya soka la Afrika kuwa miongoni mwa timu zilizofunga mabao mengi katika pambano moja la michuano ya Ligi ya Mabingwa katika hatua ya makundi. 7-0.

Hakuna haja ya kurudia kuelezea kilichotokea juzi Temeke. Kila kitu kilikuwa upande wa Simba. Walitawala mechi na kubeba kila takwimu kuanzia katika kumiliki mpira, kupiga mashuti mengi, kufunga mabao mengi, kupiga kona nyingi. Kila kitu walimiliki katika siku ambayo kwa mara nyingine tena Clatous Chama alikuwa katika ubora wake na aliondoka na mabao matatu.

Kilichotokea hakikutegemewa. Simba walikuwa na nafasi ya kushinda na kutinga robo fainali lakini hakuna aliyetegemea wangeondoka na ushindi walioupata. Ilikuwa kama vile mashabiki waliofurika Kwa Mkapa walikuwa wanatazama marudio ya pambano la Liverpool dhidi ya Manchester United wiki mbili zilizopita pale Anfield. Sasa Simba watakwenda Casablanca - Morocco kucheza pambano la mwisho dhidi ya Raja Casablanca wakiwa watalii tu. Watatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mohamed V wakiwa watalii wa safari ndefu ya Afrika Kaskazini wakiwa tayari wamepita. Haikutazamiwa kwa namna ambavyo walilianza kundi.

Kuanzia Ulaya mpaka Afrika ni nadra sana kwa timu kupoteza michezo miwili ya kwanza halafu ikafanikiwa kuvuka katika kundi. Zaidi ya yote ni licha ya kupoteza mechi hizo, lakini wamefanikiwa kupita huku wakiwa na mechi moja mkononi. Inashangaza na haitokei mara nyingi katika soka.

Mechi muhimu ambayo iliivusha Simba ilikuwa ugenini dhidi ya Vipers pale Kampala. Pale ndipo Simba walianza roho ngumu kwenda robo fainali. Lakini zaidi walisaidiwa na Horoya kucheza mechi mbili na Raja ambazo walipoteza. Horoya ndio walionekana kuwa tishio kwa Simba.

Sasa Simba inaweza kupangiwa timu yoyote jeuri katika hatua inayofuata. Ushindi wa juzi umeacha maswali kama ambavyo dhidi ya Vipers Kwa Mkapa uliacha maswali. Walikuwa katika kiwango cha kawaida wakati walipowafunga Vipers kiasi kulikuwa na mkanganyiko wa hisia kutoka kwa mashabiki wa Simba na wale wengine wanaopenda soka.

Simba haikuonekana kama timu ambayo ingeweza kuwa na makali katika siku za usoni. Hata mashabiki wake walionekana kuwa na hofu. Juzi wameupiga mwingi, lakini tunaachiwa maswali kama wapo katika ubora wa kupambana na wababe wa soka la Afrika kina Esperance, Mamelodi, Wydad Casablanca na wengineo.

Tuichukue mechi ya lini kama angalizo? Dhidi ya Vipers ambayo walishinda kwa tabu au Horoya ambayo wameshinda kwa kishindo? Binafsi naichukua ya Vipers. Simba wawe makini na pambano lijalo huku wakilitumia la Vipers kama mfano. Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anahitaji kuitengeneza kuwa makini.

Kuna tatizo la ukabaji wa pamoja wakati timu haina mpira. Hakuna nidhamu kubwa watu wa mbele. Ukiwapanga Chama, Saido Ntibazonkiza na Pape Sakho mara nyingi timu inakosa balansi na kunakuwa na mzigo mkubwa kwa viungo wengine pamoja na safu ya ulinzi.

Licha ya ushindi mnono wa juzi, ningemsihi Robertinho aichezeshe timu kama vibonde (underdogs) kama wakipangiwa na klabu kubwa. Vinginevyo maisha yatakuwa magumu kama ilivyokuwa dhidi ya Raja na Simba hawakucheza kwa nidhamu wakajikuta wanaadhibiwa.

Kwa Horoya ilikuwa rahisi kwa Simba kufanya kila walichotaka uwanjani kwa sababu wapinzani wao walionekana kuwa dhaifu na hawakuwa na mipango madhubuti. Hata katika pambano la kwanza kule Conakry, Simba hawakustahili kupoteza pointi tatu kama kina John Bocco wangekuwa makini.

Lakini sasa wanaenda kukutana na timu kali zaidi. Wanaweza kulitumia pambano la marudiano dhidi ya Raja pale Casablanca kama mfano wa namna wanavyoweza kucheza na timu kubwa katika hatua inayofuata. Pambano hili dhidi ya Raja ugenini ni kipimo tosha cha aina ya mechi mbili wanazotarajia kucheza hatua inayofuata.

Sijawahi kumuamini Robertinho katika kuichezesha timu kwa namna ya kujihami kwa usahihi. Kama akifanikiwa kuichezesha timu kwa mbinu hizo Simba inaweza kusogea mbali. Ni vile tu mpaka sasa hatujui ni mpinzani gani atapangiwa katika pambano lijalo. Hata hivyo halitazamiwi kuwa pambano rahisi.

Vyovyote itakavyokuwa, kilichonifurahisha kuhusu Simba ni namna ambavyo wameanza kuifanya hatua ya robo fainali kama mazoea. Wakati naandika makala hii Yanga walikuwa hawajacheza pambano lao dhidi ya US Monastir ya Tunisia pale pale Temeke, lakini kama na wao wakifuzu kwenda hatua ya robo fainali itakuwa jambo la kupendeza kwa soka la Tanzania.

Mazoea ya kwenda robo fainali mara kwa mara ndio ambayo yatatengeneza nafasi nzuri ya kwenda hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza baada ya miaka 49. Mara ya mwisho timu ya Tanzania kucheza nusu fainali ya michuano hii ilikuwa mwaka 1974 wakati Simba walipocheza nusu fainali na Mehalla Al Kubra ya Misri. Haijawahi kujirudia.

Hata hivyo hauwezi kuiwaza nusu fainali au fainali kama haufiki robo fainali mara kwa mara. Ni kama suala la kuwaza kufuzu kucheza kombe la dunia wakati unashindwa kufuzu kwenda michuano ya mataifa ya Afrika. Ni udanganyifu wa akili. Simba wanachofanya kwa sasa ni sahihi zaidi bila ya kujali aina ya kikosi ambacho wanacho. Inatengeneza uimara wa akili hata kwa wachezaji wapya wanaoingia kikosini kila mwaka.

Kila la heri kwa Mnyama. Timu pekee ambayo naihofia zaidi katika michuano hii ni Mamelodi Sundowns. Kama wakiiepuka katika hatua inayofuata basi litakuwa jambo jema. Nilikuwa nawaangalia walivyokuwa wakiiteketeza Al Ahly wiki moja iliyopita. Mamelodi ni ndoto inayotisha. Ni kama vile walikuwa wanacheza michuano tofauti na hii ambayo Simba wanashiriki.