Mei ya Dabi lolote litatokea

Muktasari:

HABARI ya mjini kwa sasa upande wa michezo ni mechi ya leo Jumamosi jioni ya watani wa jadi, Simba na Yanga pale kwa Mkapa jijini Dar es Salaam.

HABARI ya mjini kwa sasa upande wa michezo ni mechi ya leo Jumamosi jioni ya watani wa jadi, Simba na Yanga pale kwa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Hii ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambapo mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1. Bao hilo lilifungwa na Michael Sarpong upande wa Yanga wakati Simba lilitupiwa kimiani na Joash Onyango.

Mechi za watani zina mvuto wa kipekee. Mara nyingi zinatumia muda mwingi wa watu kuzijadili. Tambo zinakuwa haziishi mtaani na zimewagawa Watanzania katika makundi mawili. Mwanaspoti linakuletea rekodi ya michezo ya Mei kwa timu hizo tangu zilipoanza kukutana mara ya kwanza na mara ya mwisho ilikuwa Mei 18, 2013.


MEI 19, 1985 (Yanga1-1Simba)

Mchezo uliopigwa Mei 19, 1985 ilikuwa Jumapili, mashabiki wa klabu hizo waliondoka uwanjani wakiwa hawana cha kutambiana baada ya dakika 90 kumalizika kwa kufungana bao 1-1.

Bao la Wanajangwani lilifungwa na Omar Hussein katika dakika ya sita, huku lile la kusawazisha la Wanamsimbazi lilitupiwa katika dakika ya 30 na Mohammed Bob Chopa.


MEI 21, 1989 (Yanga 0-0 Simba)

Mwaka 1989, Mei 21, Yanga ndio walikuwa wenyeji wa mchezo huo, ambapo ulimalizika kwa suluhu.


MEI 26, 1990 (Simba 1-0 YanGA)

Mei 26, 1990 Simba ilikuwa mwenyeji wa mtani wake wa jadi, Yanga katika mchezo huo uliopigwa Jumamosi, ambapo mashabiki wa Simba walitoka na kicheko baada ya timu yao kushinda kwa bao 1-0 kupitia kwa Mavumbi Omari katika dakika ya sita.


MEI 18, 1991 (Yanga 1-0 Simba)

Yanga iliichapa Simba bao 1-0, Mei 18, 1991 kupitia kwa Said Sued ‘Scud’ alilolitupia vyavuni katika dakika ya saba na kuwafanya mashabiki wao kutamba mtaani, huku wapinzani wao wakilala mapema.


MEI 1, 1999 (Yanga3-1 Simba)

Mei Mosi, 1999 ilikuwa ngumu kwa Simba baada ya kipigo cha Yanga cha mabao 3-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na Idd Moshi dakika 59, Kalimangonga Ongala dakika 64 na Salvatory Edward dakika 70, huku lile la kufutia machozi la Simba likifungwa na Juma Amir dakika 12.


MEI 6, 2012 (Simba5-0 Yanga)

Mei 6, 2012 Simba iliichakaza Yanga na kuichapa mabao 5-0 Uwanja wa Benjamini Mkapa (zamani ukiitwa Taifa). Mabao hayo yalifungwa na Emmanuel Okwi katika dakika ya 1, 65, Patrick Mafisango penalti dakika ya 58, Juma Kaseja penalti dakika 69 na Felix Sunzu kwa penalti dakika 74.


MEI 18, 2013 (Yanga2-0 Simba)

Mei 18, 2013 mashabiki wa Yanga waliondoka na vicheko uwanjani baada ya timu yao kuichapa Simba mabao 2-0. Mabao hayo yalifungwa na mastaa wao wa kigeni Didier Kavumbagu dakika 5 na Hamis Kiiza dakika 62.

Katika mechi ambazo zilichezwa Mei, siku ya Jumamosi, Yanga imeshinda mechi tatu na Simba moja wakati mechi zilizopigwa siku ya Jumapili, Simba ilishinda moja na kutoshana nguvu mara mbili.