Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England zinavyobadilika kila wiki
![Ubingwa Pict](/resource/blob/4856740/1fc1b7f15a1726b97af74ed97265de57/ubingwa-pict-data.jpg)
Muktasari:
- Liverpool imekusanya pointi 35 katika mechi 14, inashikilia usukani wa ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND: POINTI nane zinazitofautisha timu nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Liverpool imekusanya pointi 35 katika mechi 14, inashikilia usukani wa ligi hiyo.
Chini yake, ipo Chelsea na pointi 31 ilizovuna kwenye mechi 15. Pointi nne zinawatofautisha wababe hao wa Stamford Bridge na vinara.
Kisha inafuatia Arsenal kwenye namba tatu na pointi zao 29 walizovuna kwenye mechi 15. Miamba hiyo ya Emirates ipo nyuma kwa pointi sita kuwafikia Liverpool kileleni.
Nne bora inakamilishwa na mabingwa watetezi, Manchester City wenye pointi 27 katika mechi 15, pointi nane nyuma ya vijana wa Arne Slot.
Hata hivyo, pengo hilo la pointi linaweza kuwa kubwa zaidi endapo kama Liverpool itashinda kiporo chake baada ya mchezo wao dhidi ya Everton kwenye Marseyside derby kuahirishwa kwa sababu za hali ya hewa.
Vita ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England inaonekana kuchukua sura mpya kila wiki.
Mara ya mwisho Ligi Kuu England iliposimama kukwepa mechi za kimataifa katikati ya Oktoba, ilionekana kama mbio za timu tatu, ambapo pointi moja tu iliwatofautisha vinara Liverpool na Man City na Arsenal.
Lakini, wachezaji waliporejea kutoka kuziwakilisha nchi zao kwenye mechi za kimataifa, mambo yamekuwa tofauti kabisa kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England.
Arsenal ilikosa ushindi kwenye mechi nne za Ligi Kuu na Man City ikakumbana na vipigo mfululizo kutoka kwa Bournemouth na Brighton, wakati huo Liverpool yenyewe ikiendelea kukusanya pointi kwa ushindi.
Wakaichapa Aston Villa kuweka pengo la pointi kufikia tano, huku Chelsea na Arsenal zilikuwa nyuma kwa pointi nne zaidi baada ya sare ya 1-1.
Hiyo ina maana gani kwenye mchakamchaka wa mbio za ubingwa? Baada ya mwanzoni kuonekana kama ni vita ya Liverpool, Arsenal na Man City, lakini sasa Chelsea imeibuka na kuonekana kuingia kwenye mbio hizo.
Mwanzo bora wa kocha Slot huko kwenye kikosi cha Liverpool umeduwaza wengi. Kikosi chake kilivuna pointi 28 kati ya 33 za kwanza ilipocheza mechi zake 11 za kwanza na hivyo kuifanya timu hiyo kuweka rekodi tamu ya kuvuna pointi za kutosha kwenye mechi hiyo, kama ilivyokuwa imefanya kwenye msimu iliyonasa ubingwa 2019/20.
Katika kipindi kama hicho, Liverpool ilikuwa imevuna pointi 31 na kuweka pengo la pointi sita baada ya mechi 11 kabla ya kwenda kubeba ubingwa huo kwa tofauti ya pointi 18.
Historia inawabeba Liverpool. Kikosi hicho cha Slot kinakuwa timu ya sita kwenye historia ya Ligi Kuu England kuongoza ligi walau kwa pointi tano baada ya mechi 11. Mara zote tano nyingine timu zilipofanya hivyo, zilinyakua ubingwa – ambapo ni Manchester United msimu wa 1993/94, Chelsea 2005/06, Man City 2011/12, Man City 2017/18 na Liverpool wenyewe 2019/20.
Katika timu 11 ambazo zilizidi pointi za Liverpool 28 baada ya mechi 11, ni tatu tu ndizo zilishindwa kubeba ubingwa. Kwa sasa, Liverpool imecheza mechi 14 na imekusanya pointi 35 kwenye 42 ilizopaswa. Kuahirishwa kwa mechi yao ya Everton kumetibua hesabu zao, ambapo ushindi ungewafanya kufikisha pointi 38 katika mechi 15.
Kwenye mechi 11 za kwanza Liverpool ilipoteza pointi tano, lakini kwenye mechi tatu ilizocheza mbele kufikisha 14, Liverpool imepoteza pointi mbili. Si mbaya.
Nani atabeba ubingwa 2024/25?
Ingali mapema. Lakini, kwa uzito wa historia mambo yanaikataa Arsenal na Chelsea kutokana na idadi ya pointi walizopoteza kwenye zile walizostahili kuzivuna. Arsenal na Chelsea zenyewe zilipaswa kuwa na pointi 45 kwa sasa kwa mechi ilizocheza, lakini sasa, zimekusanya pointi 29 na 31 mtawalia.
Kwenye mechi 11 za kwanza timu hizo zilikuwa nyuma kwa pointi tisa. Hakuna, timu yoyote huko nyuma iliyowahi kuzidiwa zaidi ya pointi nane baada ya mechi 11 za kwanza na kisha ikabeba ubingwa.
Lakini, kwenye soka mambo ambayo hayawezekani yamekuwa yakiwezekana wakati mwingine. Kwa kifupi tu, kwenye Ligi Kuu England kuna mabingwa wanane waliwahi kutoka nyuma kwa tofauti ya pointi tisa au zaidi kwenye mechi 11 za kwanza na kisha ikachukua ubingwa. Pengine linaweza kujirudia kwenye msimu huu.
Mfano mzuri kwenye hilo ni Arsenal ya kocha Arsene Wenger, ambapo ilifuta pengo la pointi 13 dhidi ya Man United baada ya mechi 19 katika msimu wa 1997/98 na kunyakua ubingwa huo.
Man City ilipambana kutokea nyuma kwa tofauti ya point nane baada ya mechi 28 katika msimu wa 2022/23 na baada ya mechi 17 katika msimu wa 2023/24 na kwenda kushinda ubingwa.
Msimu huu, Man City imekuwa na kiwango duni, lakini hilo linaweza lisiwe tatizo kwao kwenye msako wa ubingwa, wakati wakipambana kunyakua taji lao la tano mfululuzo.
Liverpool wanapaswa kukumbuka kitu kilichofanywa na Arsenal msimu uliopita, ambapo iliketi kileleni kwenye msimu wa ligi kwa zaidi ya siku 248, lakini baadaye ilishindwa kunyakua ubingwa huo, ukanaswa na chama la Pep Guardiola.
Kuna mpinzani mwenye mechi ngumu?
Baada ya Arsenal kukutana na ugumu kwa wiki za hivi karibuni, kocha Mikel Arteta alidai kwamba hakuna timu kwenye Ligi Kuu England inayokabiliwa na changamoto kubwa kwenye mbio za ubingwa kuwazidi wao.
Arsenal inafahamu mtihani uliopo mbele yao katika kufukuzia mafanikio yao ya misimu miwili iliyopita huku ikiwa na kazi ya kuvuka zaidi. Kitu pekee ambacho Arsenal inapaswa kufanya msimu huu na kueleweka kwa mashabiki wake ni kupiga hatua moja juu zaidi baada ya kuishia kwenye namba mbili katika misimu miwili mfululizo.
Kwa sasa, Arsenal imebakiza mechi nne kabla ya kufika nusu ya msimu kwenye Ligi Kuu England, wakati vinara wa ligi hiyo wao wamebakiza mechi tano.
Ugumu wa mechi kwa kila timu kwenye mbio hizo ndicho kitu kitakachoamua kwenye hatima ya mchakamchaka huo.
Kwenye karatasi, Chelsea na Arsenal zinaonekana kuwa na ratiba nyepesi kidogo katika kuifikia nusu ya msimu, lakini mambo si magumu pia kwa Liverpool huku Man City bado wakionekana kwenye wakati mgumu wa kutambua hatima ya kiwango chao kwa sasa.
Liverpool inakabiliwa na mechi dhidi ya Fulham, Tottenham, Leicester City na West Ham United, wakati Man City ina shughuli mbele ya Manchester United, Aston Villa, Everton na Leicester City. Chelsea yenyewe itakabiliwa na kipute cha Brentford, Everton, Fulham na Ipswich Town huku Arsenal ikiwa na kazi mbele ya Everton, Crystal Palace, Ipswich Town na Brentford.
Makocha wanasemaje?
Arne Slot wa Liverpool anasema: “Tunafahamu msimu ni mrefu, hivyo tunapaswa kuendelea kufanya tunachofanya kwa sasa kwasababu timu kama Arsenal, City na Chelsea zote ni timu zinazotaka kushinda ubingwa na bado kuna mechi nyingi mbele. Hivyo, yatupasa kubaki kwenye ubora wetu hadi mwisho.”
Pep Guardiola wa Man City anasema: “Pengine baada ya miaka saba ya kushinda mataji sita ya Ligi Kuu England, pengine huu mwaka kuna mtu mwingine anastahili.”
Enzo Maresca wa Chelsea anasema: “Kwa upande wangu, tupo nyuma kwa timu hizi kama Man City na Arsenal na tunapambana kwa sababu hao wamekuwa na makocha wao kwa muda mrefu. Tupo nyuma yao, lakini Chelsea ni klabu kubwa duniani, tunahitaji kushindana na kushinda mechi zetu.”
Mikel Arteta wa Arsenal anasema: “Kushinda, kushinda na kushinda tena hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa. Mambo yanapochanganya na kuwa magumu, unapaswa kuonyesha ukali wako. Akili ya kila kitu kinapaswa kuelekezwa uwanjani.”
Mambo yatakuwaje? Je, Arsenal huu ni mwaka wa Arsenal? Man City itapindua meza baada ya mambo kuwa magumu au Chelsea itaduwaza watu?