Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Martina mrembo aliyetingisha katika tenisi enzi hizo

Muktasari:

  • Katika masumbwi  haiwezekani kusimulia habari za mchezo huu bila ya kueleza mafanikio ya wana ndondi wa zamani kama Muhammad Ali, Joe Luis, Rocky Marciano, Joe Frazier, Floyd Patterson na Mike Tyson.

KWA kawaida unapozungumzia  mchezo wowote ule wapo watu huwezi kukwepa kutoa simulizi zao kutokana na ustadi na mafanikio yao yaliyoacha kumbukumbu isiyosahaulika.

Katika masumbwi  haiwezekani kusimulia habari za mchezo huu bila ya kueleza mafanikio ya wana ndondi wa zamani kama Muhammad Ali, Joe Luis, Rocky Marciano, Joe Frazier, Floyd Patterson na Mike Tyson.

Vivyo hivyo katika soka wachezaji nyota kama Pele, Diego Maradona, Garincha, Stanley Mathews, Michel Platini, Johan Cruyff na hivi karibuni Lionel Messi na Cristaiano Ronaldo haiwezekani kukosa kuwataja unapongumzia mchezo huu.

Katika tenisi huwezi kulikwepa jina la yule aliyejulikana kama Malkia wa Tenisi, Martina Navratilova, mzaliwa wa Czechoslovakia (sasa imegawika katika nchi mbili, Czech na Slovakia) na ambaye sasa ni raia wa Marekani.

Mwanamke huyu amekuwa mchezaji bora wa tennis duniani kwa miaka 10 kutoka 1978 hadi 1988 na siku hizi hutoa matamshi makali kukosoa uamuzi ya serikali ya Marekani na baadhi ya taasisi za kiraia za kimataifa.

Katika salamu zake za kuukaribisha mwaka 2025 aliwataka wasichana wacheze tenisi ili kujenga afya zao na kujitafutia ajira kupitia katika mchezo huu.

Tuzo alizopata ni nyingi ambazo hata mwenyewe nyingine hazikumbuki. Alishinda mashindano 168 ya mchezaji mmoja mmoja idadi kubwa kuwahi kukaribiwa na mchezaji yeyote  duniani, mwamume au mwanamke. Ameweka historia kwa kushinda michezo ya mashindano  1,440 na kupoteza 213 tu na kuweka rekodi ya kushinda mara tisa mashindano ya Wimbledon Open.

Katika mwaka 1984 aliweka rekodi ya  kuibuka kidedea katika michezo 86 mfululizo.

Alizaliwa Oktoba 18, 1956, katika hospitali ambayo pia ndiyo aliyozaliwa mama yake katika kijiji cha Oevnice, Czechoslovakia, akiwa na jina la Martina Subertova. Wazee wake waliachana  mwaka 1962 akiwa na miaka mitatu na  mama yake aliolewa na Miroslav Navratil aliyekuja kuwa mwalimu wake wa kwanza wa tenisi. Hapo ndipo alipochukua jina la baba wa kambo  na kujulikana kama  Martina Navratilova.  Aliongeza herufi tatu za ova  mwisho wa jina lake ambazo kwa lugha ya Kicheki ova ni kwa mtoto wa kiume na ova ni ya mtoto wa kike.

Katika mwaka  1972, akiwa na miaka 15, alichukua ubingwa wa taifa wa tenisi wa Czechoslovakia na mwaka uliofuata alikuwa mchezaji wa kulipwa na kushinda mashindano yake ya kwanza ya kimataifa katika mji wa Orlando, Marekani, 1974.

Mama huyu anayetumia zaidi mkono wa kushoto kupiga mpira, iwe wa kasi au wa kinyonga, alivutia mashabiki wa tenisi kila pembe ya dunia na wakati wote alipokuwa akicheza alionekana mtu aliyejituma kupita kiasi, hata pale lipokuwa na umri mkubwa.

Martina akiwa chipukizi, aliingia fainali za Grand Slam mara mbili na kushindwa  1975 katika fainali ya mashindano ya wazi ya Australia akiangushwa na Evonne Goolagong Cawley na ya Ufaransa alibwagwa na Chris Evert, wanawake waliotamba sana katika miaka ya 1970 na mwanzoni mwa 1980.

Baada ya kushindwa na Evert katika nusu fainali ya mashindano ya wazi ya Marekani akiwa na miaka 18 aliomba kuishi Marekani kama mkimbizi. Alisema  hakufurahia utawala wa kikomunisti wa nchi yake, Czechoslovakia na akapewa uraia.

Katika mwaka 1978 alishinda mashindano ya Wimbledon alipopambana na Evert katika fainali kwa seti 3-0 na kuwa mchezaji bora duniani.

Baada ya hapo alishinda mashindano 86 mfululizo mpaka alipoangushwa kutokana na kujiamini katika mashindano ya wazi ya Ufaransa 1986. Kati ya 1982 na 1984 alipoteza michezo sita tu, lakini wote waliomshinda aliwanyuka walipokutana kwa mara ya pili.

Alichaguliwa mchezaji bora wa mchezao wa wawili wawili kwa miaka mitatu kuanzia 1980 na baada ya wachezaji wengi kushindwa kumpindua alichomoza chipukizi Steffi Graf wa Ujerumani ambaye alimshinda 1987 walipopambana katika fainali ya mashindano ya wazi ya Ufaransa.

Hata hivyo, alilipiza kisasi kwa kumfunga Graf katika fainali za Wimbledon na mashindano ya wazi ya Marekani ya mwaka huo huo.

Lakini mwishoni mwa 1987 Graf alimpora Martina hadhi ya kuwa mchezaji namba moja duniani na kushinda mataji makubwa ya Grand Slam mara nne katika mwaka 1988, ikiwa pamoja na kumfunga Martina 5-7, 6-2, 6-1 katika fainali ya Wimbledon.

Katika mwaka 1989, Graf na Martina walikutana katika fainali za Wimbledon na mashindano ya wazi ya Marekani na Graf alishinda mara zote mbili.

Wakati marafiki zake walipomtaka astaafu ili asiadhirike, Martina alisema alitaka kuuonyesha ulimwengu kuwa umri si hoja na ujuzi hauzeeki.

Alijitokeza kucheza kwa nguvu kama alivyokuwa miaka 10 nyuma na kushinda Grand Slam 1990 na lengo lake kubwa lilikuwa kupambana tena na Graf ambaye alitolewa katika nusu fainali na Zina Garrison.

Katika fainali, akiwa na miaka 33, Martina alimshinda Garrison 6-4, 6-1 na kuweka rekodi ya kuwa bingwa wa Wimbledon mara tisa.

Mnamo 1991 alifungwa katika mashindano ya wazi ya Marekani na aliyekuwa mchezaji namba moja duniani wakati ule, Monica Seles. Katika nusu fainali Martina alimtupa nje Graf.

Katika mwaka 1994,  akiwa na miaka 37 na kuitwa bibi kizee wa tenisi, huyu mama alifika fainali ya Wimbledon, lakini alishindwa katika seti zote tatu na  Conchita Martinez.

Baada ya hapo alistaafu katika mashindano ya mchezaji mmoja mmoja, lakini katika mwaka 2000 alirudi kwa kishindo kucheza michezo ya wawili wawili. Kwa mshangao wa wengi, katika mwaka  2002 alijimwaga uwanjani kurudia mashindano ya mchezaji mmoja mmoja kwa kumwangusha mchezaji namba 22 duniani, Tatiana Panova.

Hata hivyo, alionekana kuishiwa nguvu katika mzunguko wa pili na kushindwa na Daniela Hantuchova katika seti tatu.

Katika mwaka  2003, alishinda michezo ya wachezaji wawili wawili wa jinsia za mchanganyiko katika mashindano ya wazi ya Australia na ya Wimbledon.  Ushindi huu ulimfanya kuwa mchezaji mkongwe kabisa, akiwa na miaka 46 na miezi minane kuwa bingwa wa Grand Slam. Hadi leo hajatokea mchezaji mwenye umri uliokaribia huo kuwa bingwa wa tenisi.

Ushindi  wa Wimbledon ulimuweka sawa na rekodi ya Wimbledon ya Jean King ya kushinda mara 20 mashindano ya wanawake na kuimarisha ushindi wake wa grand slam kufikia mara 58, mtu wa pili baada ya Margaret Court aliyeshinda mara 62.

Katika michezo yake ya mwisho , mwezi Aprili, mwaka 2006,  akiwa pamoja na Nadia Petrova alishinda mashindano ya Montreal, Canada. Mnamo tarehe 6 Julai, 2006 alicheza mchezo wake wa mwisho Wimbledon na kushindwa na Andy Ram wa Israel.

Mama huyu , ijapokuwa siku hizi hujitokeza sana katika mambo ya kisiasa na haki za raia, atakumbukwa zaidi katika medani ya tenisi.

Sio rahisi kutokea mwanamke wa miaka 46 au zaidi kutamba hivi.