MAONI: Wajumbe TFF, wasifanye makosa uchaguzi

Friday June 11 2021
mkwabi pic

PAZIA la Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 7, mwaka huu limefunguliwa rasmi mapema wiki hii.

Wadau mbalimbali wameanza kuchangamkia fomu za kuwania nafasi kwenye uchaguzi huo utakaofanyikia jijini Tanga, akiwamo mtetezi wa kiti cha Urais wa shirikisho hilo, Wallace Karia.

Huu ni uchaguzi utakaowaweka viongozi wa TFF kwa miaka mingine minne ijayo, kuongoza soka la Tanzania.

Uongozi ambao utaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na uongozi wa sasa wa shirikisho hilo ili kusukuma mbele zaidi gurudumu la mchezo wa soka nchini.

Kutokana na kiu kubwa ya Watanzania katika kuona soka letu linasonga mbele kutoka lilipo kwenda kwenye mafanikio makubwa zaidi ni fursa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi huo wa TFF, kuhakikisha wanafanya uamuzi sahihi.

Uamuzi wa kuchagua viongozi bora ili kulisongesha mbele soka la Tanzania ni wajibu wao hivyo wanapaswa kuwa makini katika kuwasikiliza na kuwapima wagombea watakaojitokeza na kupitishwa kwenye kinyang’anyiro hicho, ili kuhakikisha wanapatikana viongozi bora na sahihi wanaohitajika kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Advertisement

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TFF ndio wanaoweza kuihakikishia Tanzania nafasi ya inasonga mbele au kurudi nyuma kutoka mahali ilipo kisoka kwa sasa.

Wao ndio wanaoweza kuiamulia Tanzania na TFF kwa ujumla iongozwe na viongozi wa aina gani kwa miaka minne ijayo.

Hivyo ni lazima wajumbe watakaoenda Tanga miezi miwili ijayo kuchagua viongozi wa TFF wajue mapema kwamba, Watanzania wanataka kuona soka lao linasonga mbele. Soka litakaondokana na makando kando yaliyochangia kukwamisha kupiga hatua ndani ya miaka minne iliyopita.

Viongozi ambao wataendeleza mazuri na makubwa yaliyojitokeza ndani ya miaka minne iliyopita ili kuzidi kupiga hatua na sio kuirudisha nyuma Tanzania.

Wajumbe hao ndio wanashikilia hatma ya soka la Tanzania kwani, kama wataamua kutanguliza masilahi yao mbele badala ya masilahi ya soka la Tanzania, basi watatuchagulia viongozi bomu watakaoturudisha nyuma miaka minne ijayo.

Lakini kama watakuwa wazalendo na kutanguliza masilahi ya soka la Tanzania, basi ni wazi uchaguzi wa jijini Tanga utakuwa wa neema kwa wanafamilia ya soka kwa kuchaguliwa viongozi waaminifu, waadilifu na wenye njaa ya maendeleo ya kweli.

Kama wadau wakubwa wa michezo hususani wa soka nchini, tunaamini wajumbe wenye kukidhi matakwa na watakaokuwa na uhalali wa kushiriki uchaguzi huo, wataenda Tanga wakiwa na dhamira moja ya kuiletea Tanzania uongozi makini.

Uongozi makini ambao utaendesha soka la Tanzania kwa uadilifu, uaminifu na weledi wa hali ya juu, ili kuipeleka mbele zaidi kutoka hapa tulipo sasa.

Kosa lolote ambalo wajumbe hao watalifanya kwa kuchagua viongozi wasiofaa kwa kuendeshwa kwa mihemko au shinikizo la watu wachache, ni wazi Tanzania itaendelea kubaki ilipo na wajumbe hao ndio watakaobeba mzigo wa lawama hapo mbele.

Wadau wa soka ambao wameanza kuufuatilia uchaguzi huo tangu ulipotangazwa mapema, ili kuona wajumbe wa mkutano huo watasuka ama kunyoa katika kuhakikisha soka la Tanzania linasonga mbele mahali lilipo ama watalirudisha nyuma.

Advertisement