Mafaza wanaokiwasha Championship

Muktasari:

WAKATI Championship ikizidi kurindima kwa timu kusaka nafasi ya kuungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, zipo sura kongwe ‘mafaza’ ambazo zinakiwasha balaa kwenye ligi hiyo.

WAKATI Championship ikizidi kurindima kwa timu kusaka nafasi ya kuungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, zipo sura kongwe ‘mafaza’ ambazo zinakiwasha balaa kwenye ligi hiyo.

Michuano hiyo ambayo awali ilifahamika kama Ligi Daraja la Kwanza, msimu huu inashirikisha timu 16 ambazo zinacheza kwa mfumo wa ligi tofauti na msimu uliopita ilipochezwa kwa makundi.

Hadi sasa vita imekuwa kali kwa timu shiriki kutokana na ushindani ulivyo kwenye mbio za kupanda Ligi Kuu msimu ujao, huku wakongwe wakionyesha mchango ndani ya uwanja.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya baadhi ya nyota wakongwe wanaokiwasha kwenye michuano hiyo pamoja na michango katika timu zao.


Dany Mrwanda - Ken Gold

Pamoja na ukongwe wake kwenye soka, lakini Mrwanda ndiye injini ya Ken Gold na hili halina ubishi kwa sababu kuwepo kwake kikosini kumeisaidia kupata matokeo mazuri kwa sasa.

Mrwanda ambaye alianza soka la ushindani miaka ya 2002 hadi kuzitumikia timu kadhaa ikiwamo Simba, Yanga na Taifa Stars, tayari ameifungia mabao mawili timu hiyo na kuipa alama nne muhimu.

Pamoja na kucheza soka lakini unaambiwa awapo uwanjani haishii kukimbia, bali hutoa maelekezo kwa wachezaji alionao ndani ili kutimiza vyema majukumu yao kuisaidia timu kupata matokeo.

Kutokana na umuhimu na mchango wa supastaa huyo ameaminiwa na benchi la ufundi kupewa kitambaa cha unahodha kuhakikisha hakiharibiki kitu.


Samwel Kamuntu -Transit CaMP

Pamoja na kushindwa kuipandisha kwa misimu miwili mfululizo aliyocheza klabuni hapo, lakini Kamuntu amekuwa moja ya wachezaji wenye mchango mkubwa katika kikosi cha Transit Camp.

Hadi sasa wakati ligi hiyo ikimalizika raundi ya tatu tayari ameifungia bao moja wakati wakiisurubu African Lyon kwa mabao 2-1 wakiwa ugenini.

Kama haitoshi nyota huyo aliyewahi kutesa na JKT Tanzania, Stand United na Ruvu Shooting msimu uliopita aliisaidia timu hiyo kufika mechi za mchujo ilipomaliza nafasi ya tatu. Kutokana na mchango wake kikosini amekuwa na uhakika wa namba licha ya vita kubwa kwani amekuwa na mwendelezo mzuri kwa maafande hao.


Ally Shiboli - African Sports

Hakuna shaka kwamba staa huyu umri wake umekwenda, lakini unaambiwa shughuli yake uwanjani sio ya kitoto na kwa sasa anaitumikia African Sports akichuana kuipandisha tena Ligi Kuu.

Shiboli ambaye aliwahi kutamba na timu nyingi ikiwa Simba, Coastal Union, JKT na Dodoma Jiji kwa sasa ndiye mkongwe zaidi kikosini humo lakini anaaminiwa na kocha wake, Kessy Abdallah.

Pamoja na kwamba hajafunga bao lolote - kukumbwa na majeraha kumempa wakati mgumu na kuzikosa mechi mbili za mwisho baada ya kuumia wakati walipocheza na Fountain Gate na kutoka suluhu.

African Sports pia inao nyota wa zamani waliowahi kuzichezea timu mbalimbali akiwemo Omega Seme na Jamal Mwambeleko wakishirikiana kuipa matunda timu hiyo ya jijini Tanga.


Salum Telela - Ndanda FC

Kiungo huyu ndiye nahodha wa Ndanda FC ambayo kwa sasa inashiriki Championship na matumaini ya wadau na mashabiki wa timu hiyo mkoani Mtwara yapo kwa nyota huyo kuwavusha.

Telela ambaye alizitumikia timu kubwa ikiwamo Yanga iliyomsajili kutoka Moro United, licha ya kwamba timu yake haijapata matokeo mazuri, lakini mchango wake unaonekana uwanjani.

Nyota huyo uwepo wake kwenye timu hiyo kunaamsha ari na morari kwa wachezaji chipukizi na kuongeza hali ya ushindani kutokana na historia yake kwenye medani za soka nchini.


Hamad Kibopile - Green Warriors

Kibopile sio jina geni kwa wadau na mashabiki wa soka nchini kutokana na kazi aliyoifanya kabla ya kutua kwa wajeda hao.

Jamaa amezichezea timu nyingi nchini kwa mafanikio akianza kuitumikia Mbeya City, Majimaji, Stand United, Arusha FC na Dodoma Jiji.

Kwa sasa mkali huyo anaichezea Green Warriors inayosaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu na nyota huyo amekuwa chaguo la benchi la ufundi chini ya kocha Azishi Kondo.


Yusuph Mgeta - Pamba

Beki huyu mwenye mwili wa ulioshiba ndiye mkongwe katika kikosi cha TP Lindanda inayoshiriki Championship kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Alizitumikia timu nyingi kama Toto Africans, Stand United, Tanzania Prisons, African Lyon na Ruvu Shooting lakini bado anaendelea kukiwasha jijini Mwanza.

Pamoja na ukongwe wake, lakini kwa muda alioitumikia timu hiyo kwa takribani msimu wa tatu sasa, lakini timu imekuwa na matokeo mazuri ikiwamo kunusa kupanda Ligi Kuu na kuishia mchujo.

Kwa sasa tayari timu hiyo imeendelea kuwa vizuri kutokana na kucheza mechi tatu ikiwa haijapoteza hata moja, ikishinda mbili na sare moja ikiruhusu mabao mawili.


Amis Tambwe - DTB

Achana na mambo ya umri, Tambwe bado ni moto wa kuotea mbali kwenye soka la ushindani na sasa anakinukisha DTB inayoongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Katika kudhihirisha uwezo wake, anacheza na kitambaa cha unahodha na amekitendea haki kwa kuipa usukani timu yake na kuongoza kwenye orodha ya wafungaji bora.

Tambwe, raia wa Burundi, hakuna asiyejua kazi yake kwani hata Simba na Yanga alifanya maajabu akiibuka mfungaji bora kwa nyakati tofauti.

Nyota huyo ambaye alicheza timu kubwa za ndani na nje mbali na Simba na Yanga pia amekipiga Vital’O ya Burundi na Fanja FC ya nchini Oman.


Wasikie Makocha

Kocha Mkuu wa African Sports, Kessy Abdalah anasema uwepo wa nyota watatu wenye uzoefu kikosini kwake inawaongezea kujiamini hata vijana wengine.

Anasema wana matumaini makubwa kwa wachezaji hao na wengine kwa kushirikiana wanaweza kufikia malengo na kuongeza ushindani na mvuto kwenye ligi.

“Tunawatambua kwa uwezo wao, kwa sababu hata huko nyuma walifanya vizuri, hivyo kuwepo kwao ndani ya timu wanafanya ichangamke na kuleta mvuto,” anasema Abdalah.

Naye Muhibu Kanu ambaye ni mtendaji mkuu wa DTB kwa sasa, anasema usajili wao unalenga kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu, ndio maana wameleta majembe kama hayo.

“Usajili wetu unaendana na malengo ya klabu, tumeamua kuwaleta mastaa kama hao ili kumaliza kazi mapema na uzuri matokeo siyo mabaya na kila mmoja anaonesha mchango wake,” anasema Kanu aliyewahi kuwa kocha.