KWAKO MWALIMU KASHASHA: Fainali Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa kiboko

JUZI Jumatano, kulifanyika mchezo wa fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambao ulizikutanisha timu za Yanga na Simba.

Katika mchezo huo wa fainali, Yanga iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 4-3 dhidi ya Simba baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wanaokadiriwa kufikia 12,000 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Ni fainali za 15 za mashindano hayo tangu mwaka 2007 ambapo Azam wanaongoza kutwaa taji hilo wakiwa wamelichukua mara tano wakifuatiwa na Simba iliyotwaa mara tatu wakati Yanga na Mtibwa Sugar kila moja imechukua ubingwa mara mbili.

Jumla ya timu tisa zilishiriki katika mashindano haya ya mwaka huu ambazo ni Yanga, Simba, Azam, Mtibwa, Namungo kutoka Tanzania bara na kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na timu nne ambazo ni Chipukizi, Malindi, Jamhuri na Mlandege.

Fainali hizi za 15 zilikuwa nzuri sana kwani tangu awali timu zilionekana kudhamiria kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ama kumaliza zikiwa katika nafasi za juu na sio kuondolewa katika hatua za mwanzoni.

Timu zilipeleka vikosi vyao kamili na hakukuwa na idadi kubwa ya wachezaji kutoka katika junior team kama ambavyo zilikuwa zikifanya katika mashindano hayo miaka ya nyuma. Ingawa baadhi ya timu zilikosa wachezaji ambao wako katika timu ya taifa itakayoshiriki katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan), wale waliokuwepo Zanzibar walipambana vilivyo kuhakikisha wanazipa heshima timu zao.

bahati mbaya kwa timu kutoka Zanzibar, hatua ya nusu fainali ilishirikisha timu nne za kutoka Tanzania Bara tu ambazo ni Namungo, Yanga, Azam na Simba baada ya zile za Zanzibar kushindwa kumaliza katika nafasi za juu katika makundi matatu ya mashindano hayo ama kupata nafasi moja ya best loser.

Na Baada ya hatua ya nusu fainali, Watani wa jadi, Simba na Yanga walifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya Yanga kuifunga Azam kwa mikwaju ya penati huku Simba ikiifunga Namungo kwa mabao 2-1.

Kwa ujumla ilikuwa ni derby ambayo ilionyesha maana hali ya derby na ushindani wa hali ya juu. Kulikuwa na mbinu zilizotofautiana kwa timu zote mbili ambapo Simba kocha wao alitumia mfumo wa 4-4-2 flat na baadaye akabadilisha na kuanza kutumia 4-4-2 diamond wakati Yanga wenyewe walitumia mfumo wa 3-5-2, Yanga wakijaribu kushambulia zaidi kupitia pembeni wakiwatumia zaidi Tuisila Kisinda na Saido Ntibazonkiza huku Simba wakijaribu kupenya kupitia katikati.

Makipa wa pande zote mbili walikuwa bora kuanzia katika dakika 90 za mchezo na hata katika hatua ya mikwaju ya penati na ndio maana haikushangaza kuona kila kipa akiokoa penalti moja.

Walinzi walikuwa wanapata mashambulizi ya mara kwa mara lakini walikuwa wanajitahidi kufukia mashimo na uzuri ilichagizwa na wachezaji kama asilimia 60 wa vikosi kamili vya timu hizo. Nilichokiona ni kwamba presha ya mechi kutoka nje ya uwanja iliwaingia wachezaji na kupelekea kukamiana jambo ambalo lilisababisha wafanyiane madhambi ya mara kwa mara.

Hata hivyo mwamuzi alijitahidi kwa kiasi kikubwa kumanage mechi kwani vinginevyo angeweza kutoa kadi nyingi na kupelekea kuuvuruga mchezo na kupoteza ile ladha ya fainali na hatimaye baadaye wachezaji wakaonyesha utulivu.

Siwezi kuamini wanaosema kuwa Matola hakuiandaa timu katika upigaji wa penati kwani suala la kukosa penalti ni la kawaida ambalo limewahi kuwatokea wachezaji wengi.

Tofauti kubwa niliyoiona katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ni kwamba waandaaji na wasimamizi wanazingatai sana utaratibu uliowekwa. Watu wanaingia uwanjani kiustaarabu tofauti na huku bara ambako utaratibu wa uingiaji umekuwa ni changamoto. Viongozi wako imara katika kusimamia yale ambayo yamepangwa kwa mujibu wa utaratibu wa mashindano na mashabiki wamekuwa wanatekeleza kile wanachoelekezwa.

Tumeona mashabiki wamekaa majukwaani kistaarabu wakiwa wamechanganyika wa timu tofauti na hatujaona kukitokea vurugu japo mashabiki wengi waliokuwepo ni walewale ambao wakiwa huku bara huwa ni vinara wa kuanzisha vurugu.

Kwa hiyo kimsingi mashindano haya yameacha fundisho kubwa kuanzia katika timu kiufundi na hadi kwa mashabiki ambalo tunaweza kulitumia katika kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini. Mwisho wa siku niwapongeze Yanga kwa kutwaa ubingwa ambao wamestahili kulingana na maandalizi na kiwango walichoonyesha lakini pia nizipongeze timu nyingine kwa kuonyesha ushindani wa hali ya juu.


Imeandikwa na Alex Kashasha