Kwa Simba hii Watalia sana

SIMBA imeanza vizuri hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda mechi mbili mfululizo dhidi ya AS Vita na Al Ahly kwa bao 1-0 kila mmoja.

Timu hiyo inaongoza kundi A ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na AS Vita yenye pointi tatu sawa na Al Ahly iliyo nafasi ya tatu huku El Merreikh ya Sudan ikishika mkia ikia haina pointi.

Simba Imepania kufanya makubwa na kutinga robo fainali ya mashindano hayo kama ilivyowahi kufanya hivyo mwaka 2019 huku ikijivunia kikosi bora ilichonacho msimu huu.

2018/ 2019

Ndani ya miaka mitatu ,Simba ilianza safari yake ya mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 kwa kuanzia hatua ya awali kwa kuifunga Mbabane Swallos ya Swaziland mabao 4-1 nyumbani katika mchezo uliofanyika Novemba 28, 2018 kabla ya kuifunga tena ugenini mabao 4-0.

Mechi iliyofuata Simba ikachapwa ugenini mabao 2-1 na Nkana Red Devil ya Zambia lakini ikashinda nyumbani kwenye uwanja wa Mkapa mabao 3-1 na kutinga hatua ya Makundi ya mashindano hayo.

Simba ilipangwa kundi moja na Al Ahly , AS Vita na Saoura ya Algeria kwenye hatua hiyo lakini ilipambana na kutinga robo fainali kibabe na kuwaacha watu wakishindwa kuamini macho yao.

Timu hiyo ilianza mchezo wa kwanza kwa hatua ya makundi kwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Saoura katika mchezo uliofanyika Januari 12 ,2019 lakini ikapokea vipigo vikubwa mfululizo katika michezo iliyofuata ugenini dhidi ya AS Vita nchini Congo kwa mabao 5-0 na dhidi ya Al Ahly kwa mabao 5-0.

Iliporejea nyumbani Simba ilichapa Al Ahly bao 1-0 na kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali , kisha ikachapwa mabao 2-0 ugenini na Saoura lakini iliwaduwaza watu baada ya kushinda mchezo wa mwisho kwa Mkapa kwa kuichapa AS Vita mabao 2-1 na kutinga kibabe robo fainali.

Hata hivyo Simba haikufurukuta kwenye hatua hiyo ra robo fainali kwani ilijikuta ikitoka suluhu na TP Mazembe katika mchezo uliofanyika April 6, 2019 na kisha kukubali kipigo cha mabao 4-1 ugenini.

KWA MKAPA HUCHOMOKI

Jambo ambalo Simba wamelionyesha katika mashindano hayo ni jinsi wanavyotumia vizuri uwanja wao wa nyumbani wa Benjamini Mkapa jambo ambalo limekuwa likiwaogopesha hata wapinzani wao.

Tangu Simba ilipokubali kipigo cha bao 1 -0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola kwenye uwanja huo Februari 13, 2013, haijawahi kufungwa tena na timu yoyote kwenye mashindano hayo makubwa.

Desemba 15,2018 Simba ilichapwa mabao 2-1 na Nkana Red Devil nchini Zambia na lakini ikaja kushinda mabao 3-1 kwenye uwanja wa Mkapa Desemba 23 na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika .

Pia licha ya kuchapwa mabao 5-0 Al Ahly nchini Misri ilikuja kulipa kiasi kwa kuitandika timu hiyo bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Februari 12, 2019 lakini pia ilifungwa bao 5-0 na AS Vita nchini Congo lakini ikashinda kibabe kwenye uwanja wa Mkapa Machi 16, 2019 na kufanikiwa kufuzu robo fainali ya mashindano hayo.

Pia Desemba 23 mwaka jana , Simba ililala kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Platinum ya Zimbabwe lakini ikashinda nyumbani kwa mabao 4-0 na kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huu.


UGENINI MMH!

Licha ya kwamba msimu huu wameanza vizuri katika mechi za ugenini lakini Simba wanatakiwa kujitathimini na kuahakikisha wanashinda hata mechi nyingi za ugenini ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufika mbali katika mashindano hayo.

Tangu 2005 Simba ilikuwa ikipata wakati mgumu katika mechi za ugenini kabla ya kuzinduka Desemba 4, 2018 baada ya kuifunga Mbababane Swallos ya Swaziland mabao 4-0.

Baada ya mechi hiyo Simba ikapoteza mechi nyingine tatu za ugenini kabla ya kuzinduka tena mwaka jana kwa kuifunga Plateau United ya Nigeria bao 1-0 ugenini katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na Februari 12 mwaka huu kuichapa AS Vita bao 1-0 katika mechi ya hatua ya makundi.

Beki wa zamani a Simba Lubigisa Madata Lubigisa anasema kushinda nyumbani ni sawa lakini timu hiyo inatakia kubadilika na kupambana zzaidi kushinda mechi nyingi pia ugenini.

“Najua ugenini sio kazi rahisi kushinda lakini wanatakiwa kupambana kuhakikisha wanacheza kwa morali hiyo hiyo waliyonayo hata ugenini ili kupata ushindi au hata sare katika baadhi ya mechi kwani ukiwa nategemea tu kuwa nitashinda nyumbani inaweza kukugharimu kwani mpira wakati mwingine unadunda ,”anasema Lubigisa.


CHAMA SHUJAA

Simba ina kiosi bora msimu huu ambacho kinawabeba hata katika mashindano ya kimataifa lakini nyuma ya mafanikio yote hayo ya Simba ndani ya miaka mitatu huwezi kuacha kumpa sifa kubwa kiungo mzambia Clatous Chama’Mwamba wa Lusaka’.

Chama amekuwa akiibeba sana Simba katika mashindano hayo huku akiivusha hatua muhimu ambazo zimezidi kuifanya kuwa timu ya kuogopwa Afrika kwa sasa.

Kiungo huyu aliiwezesha Simba kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo Desemba 23 mwaka 2018 baada ya kufunga bao la kisigino na kuiongoza timu yake kuichapa Nkana Red Devil ya Zambia mabao 3-1.

Pia Chama hakuishia hapo kwani alisaidia timu yake kufuzu robo fainali baada ya kufunga bao la pili katika ushindi wa mabao 2-1 ambao Simba ilipta dhidi ya AS Vita ya Congo katka mchezo uliofanyika Machi 16,2019 kwenye uwanja wa Mkapa.

Ubora wa kiungo huyu mahiri uwanjani uliendelea kuibeba Simba kuisaidia kutinga tena hatua ya makundi msimu huu baada ya kuiongoza timu yake kuibamiza Platnum ya Zimbambe mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika Januari 6 mwaka huu.

Katika mchezo huo Chama licha ya kufunga bao la nne kwa penalti lakini alihusika katika mabao mengine mawili yaliyofuangwa na Erasto Nyoni na John Bocco.


ONYANGO, LWANGA BALAA

Kwa muda mrefu Simba ilikuwa ikihaha na safu yake ya ulinzi hivyo kujiweka katika wakati mgumu katika mashindano hayo makubwa.

Tangu enzi za kocha Mbelgiji Patrick Aussem timu hiyo ilikua haina mchezaji maalumu wa kucheza na muivory coast Pascal Wawa katika beki ya kati na mara nyingi kocha huyo alikuwa akibadilisha badilisha wachezaji wakati mwingine akimchezesha Erasto Nyoni, Kennedy Juma au Yusuph Mlipili.

Simba walipobaini hilo wakamsajili mkenya Joash Onyango msimu huu ambaye alileta gumzo kwa mashabiki wa soka ambao baadhi walikuwa wakimkejeli kwa kumuita mzee na mwenyewe akawajibu kuwa wala hashtuki na ipo siku atawanyamazisha.

Sasa muda ule aliosema Onyango umefika na sasa wote waliouwa wakimbeza wamenyamaza kimya kwa jinsi beki huyo alivyo katika kiwango bora huku akiwa msaada mkubwa kwa timu yake kwenye mashindano hayo ya kimataifa akishirikiana na Wawa, Mohammed Hussein’ Tshabalala’, Shomari Kapombe na kipa Aishi Manula.

Onyango ameonekana kucheza kwa jihadi kubwa akiwa mzuri ka mipira ya juu na chini lakini pia kushambulia pale inapobidi na ndio maana huwei kushangaa kuona kuwa tangu Simba ianze kushiriki mashindano hayo msimu huu imeruhu bao moja tu katika mechi sita ilizocheza mpaka sasa.

Pia usajili wa kiungo mganda Thadeo Lwanga umeonekana kuiimarisha safu ya ulinzi ya Simba kwan mchezaji huyo ameonekana kucheza ka kiwango kikubwa akivuruga mipango yote ya wapinzani kabla ya kufika eneo lao la hatari.

WASIKIE WADAU

Mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez anasema bado wana kazi kubwa mbele yao ili kuhakikisha kila mechi wanaipa uzito huku akiwaomba mashabiki kuendelea kuiapa sapoti timu hiyo kila inapocheza .

“Nawapongeza wachezaji wamekua wakipambana kila mechi.Bado tuna kazi kubwa mbele yetu na tunaichukulia kila mechi kwa uzito mkubwa.

“Tutaendelea kuwapa motisha wachezaji itakayowafanya wajisikie vizuri na kuzidi kujituma uwanjani naamini tuna timu bora itakayoshangaza kwenye mashindano hayo msimu huu ,” anasema Barbara.

Kocha mzoefu, Kennedy Mwaisabula’ Mzazi’ ameitabiria Simba kufika mbali kwenye mashindano hayo msimu huu kwa jinsi kila mchezo anavyojituma huku akimpa tano kocha wao kuwa yuko vizuri katika kuusoma mchezo na kundaa mbinu zake.

“Simba wanacheza kipambanaji sana na kama wakiendelea hivyo watafika mbali.Pia kocha wao yule anaonekana yuko vizuri katika mbinu zake.Angalia jinsi Simba walivyocheza ugenini na AS Vita na nyumbani na Al Ahly unaona kabisa ni tofauti na wenzake waliopita ambao walikuwa wakitumia mfumo ule ule iwe wanacheza kwa Mkapa au ugenini ,”anasema Mwaisabula.

Mchambuzi, Ally Mayay amekiri kua safu ya ulinzi ya Simba kwa sasa iko vizuri na kusema kuwa Lwanga ameongeza ugumu wa safu hiyo kupitika kirahisi.

“Ujio wa Lwanga umeiimarisha sana safu ya ulinzi ya Simba kwani ni kiungo mzuri ambaye amekuwa akiwalinda mabeki wake vema na hivyo kuwapunguzia kazi kubwa mabeki hao” anasema Mayay.