Kwa silaha hizi... Simba mbona freshi Afrika

Sunday October 10 2021
silaaha pic
By Thobias Sebastian

SIMBA juzi asubuhi ilikuwa uwanjani kutesti mitambo yao kirafiki kwa kuvaana na Cambiaso inayonolewa na kocha Mecky Maxime na kuwafumua mabao 4-1, huku leo ikitarajiwa kurudi tena uwanjani kunoa makali kabla ya kwenda kuvaana na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itaanzia ugenini dhidi ya wapinzani wao katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza itakayopigwa Oktoba 17 kabla ya kurudiana wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam ili kujua kama itavuka tena makundi kwa mara ya nne.

Simba ilishacheza hatua hiyo mwaka 2003, 2018-2019 na 2020-2021 na kati misimu miwili ya mwisho ilipenya robo fainali na kukwamishwa na TP Mazembe na Kaizer Chiefs.

Mshindi wa jumla wa mechi zote mbili baina yao ndiye atakayekata tiketi ya kwenda makundi, huku atakayekwama atatupwa Kombe la Shirikisho Afrika kucheza hatua ya mchujo na timu zitakazopenya raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi za klabu barani Afrika.

Simba ilipangwa na Caf kuanzia raundi ya kwanza kutokana na kufanya vyema msimu uliopita katika michuano hiyo ikitolewa robo fainali, huku wapinzani wao wakipenya mbele ya DFC Bome Arrondissement Club ya Afrika ya Kati wakiing’oa kwa jumla ya mabao 2-1.

Timu ya Galaxy iliyoanzishwa 2014, ina umri wa miaka saba na kwa jinsi ilivyocheza mechi za awali ni wazi Simba ikitumia vyema silaha zake vyema hususan uzoefu ilionao kwenye michuano hiyo itapenya kiulaini, hata kama siku zote soka ni dakika 90 za jasho na damu.

Advertisement

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya silaha ambazo kama Kocha Didier Gomes na jeshi lake kwa ujumla watazitumia zitawarahisishia kazi mbele ya wapinzani wao hao. Endelea nayo...!


KUANZIA UGENINI

Ingawa imekuwa ni utamaduni wa soka la Afrika kuamini kucheza ugenini ni changamoto kutokana na hila zinazofanywa na wenyeji kuhakikisha wanatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri, bado hiyo haiwezi kuwa kikwazo kwa Simba dhidi ya Galaxy.

Katika msimu uliopita ikiwa hatua ya makundi Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita ya DR Congo kisha kulazimisha suluhu na El Merrikh ya Sudan, kuonyesha kuwa Simba ikijipanga inatusua ugenini na pia itawapa picha ya kitu gani inachotakiwa kukifanya kwa mechi ya marudiano nyumbani.

Rekodi zinaonyesha Galaxy haina rekodi tamu ikicheza nyumbani kwani katika mechi tatu za kimataifa, imeshinda mara moja dhidi ya DFC Bome, huku nyingine mbili ikipasuka mbele ya Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns zote za Afrika Kusini. Hata katika mechi za Ligi Kuu iliyopita, imekuwa na matokeo mchanyato ikishinda na kupasuka kwenye dimba lao kuonyesha kuwa, kama Simba itafunga busta na kuwavaa kibabe Galaxy mjini Gaborone, inaweza kushinda.

Galaxy inasifika kwa kucheza soka la kushambulia ikiwa nyumbani, ila ni lazima iwe na tahadhari yasije yakawakuta kama yale ya Kaizer Chiefs waliowafumua mabao 4-0 na kushindwa kupindua meza nyumbani licha ya kushinda 3-0.


UWANJA WA NYUMBANI

Kati ya silaha kubwa inayowabeba kwa misimu yote ya kimataifa Simba ni uwanja wa nyumbani. Haijawahi kupoteza katika mechi za Caf tangu 2013 walipofumuliwa bao 1-0 na Recreativo do Libolo ya Angola walioenda kuwanyoosha tena 4-0 waliporudiana nao ugenini.

Simba imewahi kupata sare kama mbili tu nyumbani katika mechi za hivi karibuni tangu ilipolala kwa Waangola baada ya UD Songo ya Msumbiji na TP Mazembe ya DR Congo kukomaa nao, lakini mechi zao zote imekuwa ikishinda kuonyesha kama itaendelea na moto huo mambo yanaweza kuwa upande wao kutegemea na jinsi itakavyovuna katika mechi yao ya kwanza ya ugenini.

Kucheza nyumbani mbele ya mashabiki ni silaha inayoweza kuibeba Simba dhidi ya Galaxy hasa ikizingatiwa imesajili wachezaji wenye ubora na uzoefu wa mechi za kimataifa, sambamba na wale waliobakishwa kikosini kwa muda mrefu ambao baadhi walikuwa kwenye majukumu ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa.


UBORA NA UDHAIFU

Benchi la ufundi la Simba chini ya Gomes linatakiwa kutenga muda wa kutosha kuifuatilia Galaxy na kufahamu ubora na udhaifu ilionao katika kikosi chake.

Miongoni mwa ubora wanalionao Galaxy ni wazuri katika kukaba na hutumia nguvu zaidi kuutafuta mpira pindi wanapo ipoteza, wanashambulia zaidi kupitia pembeni na wanao wachezaji wenye uwezo wa kupiga mashuti. Kati ya mabao ambayo wamekuwa wakifungwa mara kwa mara ni yale yanayotokana na mashambulizi ya haraka na hilo linatokea kutokana na kupenda zaidi kushambulia. Benchi la ufundi na wachezaji wa Simba wanatakiwa kufahamu udhaifu na ubora na mengineyo ya kiufundi ili kwenda kuufanyia kazi na kuwa bora katika mechi zote mbili.


KUCHEZA KITIMU

Katika misimu miwili ambayo Simba imefanikiwa katika mashindano ya kimataifa kikosi chake kilikuwa kinacheza kitimu zaidi kuliko uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ambao hutumika baada ya mazingira kuwa magumu.

Ukiangalia mechi ambazo Simba walipata ushindi dhidi ya vigogo wa soka Afrika, Al Ahly na AS Vita - mechi tatu - mbili Benjamin Mkapa na moja Kinshasa walikuwa wakicheza kitimu kuliko uwezo binafsi.

Misimu hiyo ilikuwa rahisi kuona mpira unatoka kwa Pascal Wawa kwenda kwa Rally Bwalya ambaye aliupeleka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone anafunga bao au mazingira mengine ya aina hiyo. Tangu msimu huu umeanza wachezaji wapya na waliokuwepo msimu uliopita kikosi cha Simba kimeonekana hakijapata muunganiko zaidi.

Katika mechi za namna hii inahitajika timu ambayo inacheza kwa pamoja katika kushambulia na kuzuia mashambulizi ya wapinzani, lakini kama kuna wachezaji wake watacheza kibinafsi maana yake watakuwa na upungufu ambao utasababisha kufungwa.

Ingawa Simba ya sasa licha ya kutozoeana, bado inacheza kitimu zaidi na kama itatumia majembe yake kwa ufasaha itatoboa mbele ya Galaxy.


KUEPUKA MAKOSA

Miongoni mwa mambo mengine ambayo Simba wanapaswa kuyaangalia na kuongeza umakini katika kuyafanyia kazi ni kufanya makosa yanayojirudia mara kwa mara katika mechi za kimataifa hasa kufungwa mabao ya aina moja yanayotokana na mipira ya krosi ambayo mabeki na kipa hushindwa kuiokoa mapema.

Simba wamekuwa wakiruhusu mabao mengi ya mashuti ya mbali ambayo ni moja ya staili ya Galaxy inayotumia pale inapobaini inacheza na timu isiyowaruhusu kulifikia lango kirahisi.

Galaxy hupenda kushambulia kupitia pembeni kkwa upiga krosi nyingi kwa washambuliaji wao, ambapo kuna wachezaji wazuri wenye uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na hayo ndio upungufu wa Simba wanaotakiwa kuufanyia kazi kwa Kocha Gomes kuzungumza mapema na vijana wake hasa kipa Aishi Manula na mabeki.


REKODI YAO

Msimu 2018-2019, Simba iliweka rekodi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu ilipobadilishwa mfumo 1997 na kuondolewa na TP Mazembe kwa mabao 4-1.

Msimu uliofuata wa 2019, Simba waliondolewa katika hatua ya awali na UD Songo kwa bao la ugenini baada ya kutoka suluhu Msumbiji na kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam jambo ambalo halikutegemewa na wengi. Miongoni mwa sababu ambazo zilisababisha Simba kuondolewa mapema ni kutokana na aina ya wapinzani ambao walikuwa wanakwenda kukutana nao, lakini pia rekodi kubwa waliyokuwa nayo msimu uliopita.

Msimu huu Simba wanakwenda kukutana na hali kama hiyo kwani msimu uliopita waliishia robo fainali na waliondolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na aina ya wapinzani wanaokwenda kukutana nao hawana rekodi za kutisha.

Simba inatakiwa kuacha kuangalia rekodi walizokuwa nazo katika mashindano hayo hasa zile za msimu uliopita - aina ya timu ambayo wanakwenda kukutana nayo, bali wanatakiwa kukaza mwanzo mwisho na kuanza kupata matokeo mazuri ugenini.

Kama Simba itashindwa kulizingatia hili na wakaingia na rekodi zao za msimu uliopita yanaweza kutokea yale ya UD Songo, lakini wakiichukulia mechi hiyo kwa umuhimu mkubwa kama wanacheza na moja ya timu kubwa barani Afrika huenda wakamaliza kazi katika mchezo wa kwanza ugenini.


WASIKIE makocha

Kocha msaidizi wa Simba, Hitimana Thierry anasema katika kipindi hiki Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama licha ya baadhi ya wachezaji wao kwenda katika majukumu ya timu za taifa, waliopo wameanza maandalizi kwa ajili ya mchezo na Galaxy.

“Tumebakiwa na siku kumi za kufanya maandalizi ya kutosha ambayo naamini ndani yake tutafanya kila kilicho bora ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zote mbili,” anasema Hitimana.

Kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma anasema kikosi cha Simba msimu uliopita kilifanya vizuri katika mashindano hayo kutokana na wachezaji wake wengi kujitolea na sio uwezo wa mchezaji mmojammoja.

“Wachezaji wa Simba wakienda kucheza kitimu zaidi na kuangalia namna ya wapinzani wao walivyo (watafanikiwa).

“Naamini kuna wachezaji bora waliokuwepo msimu uliopita na wapya katika kikosi na wanaweza kufanya vizuri katika mechi zote mbili,” anasema Djuma na kuongeza kuwa sio rahisi pengo la Clatous Chama na Luis Miquissone kuzibwa kwa haraka kutokana na rekodi walizoziacha Msimbazi.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema mara zote katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika mechi za ugenini lazima zinakuwa ngumu kutokana wapinzani na kwa namna yoyote hutumia mbinu nyingi ili kupata ushindi mkubwa.

“Wachezaji na benchi la ufundi la Simba wanatakiwa kwenda na plani kubwa ya kucheza kwa kujilinda na kushambulia kwa umakini mkubwa ili kushindwa kuwapa mianya Galaxy ambayo wataitumia kufunga mabao,” anasema Ulimboka.

Advertisement