KONATE Mkimbizi kutoka Mali anayeitesa Liverpool

Muktasari:

KIMBEMBE kitakuwa katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi kwa sababu timu nyingi kubwa zitakuwa sokoni kufanya usajili wa kujenga vikosi vyao baada ya msimu huu zilizo nyingi kuonyesha viwango vibovu.

PARIS, UFARANSA

KIMBEMBE kitakuwa katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi kwa sababu timu nyingi kubwa zitakuwa sokoni kufanya usajili wa kujenga vikosi vyao baada ya msimu huu zilizo nyingi kuonyesha viwango vibovu.

Miongoni mwa timu zinazotarajiwa kufanya usajili ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool, ambayo msimu huu inasumbuliwa na upungufu mkubwa kwenye safu yake ya ulinzi baada ya Virgil van Dijk kuwa nje kwa zaidi ya miezi minne.

Mmoja kati ya mabeki wa kati iliowaweka kwenye rada zake ni pamoja na Ibrahima Konate wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Ufaransa, ambaye alitengeneza pacha nzuri na Dayot Upamecano, anayetarajiwa kuondoka na kujiunga na Bayern Munich. Lakini unamfahamu Konate ni nani?


Konate ni nani?

Konate alizaliwa Mei, 25, 1999 jijini Paris, Ufaransa. Jina lake kamili ni Ibrahima Konate.

Taarifa zinasema alizaliwa kwenye familia yenye watoto wengi, hivyo yeye ni miongoni mwa viziwanda. Familia yake ina asili ya Mali kama zilivyo za kina Ousmane Dembele na N’golo Kante ambazo pia zimetokea nchini humo.

Kwenye maisha yake ya utotoni inasemekana jamaa alikuwa mpole sana ukilinganisha na ndugu zake.

Konate alikuwa akikubali kufanya kile kazi aliyoamrishwa kufanya na watu ambao walikuwa juu kiumri kwa upande wake.

Vilevile muda mwingi alikuwa yupo bize na mazoezi kwa kuwa alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasoka mkubwa tangu utotoni.


Safari katika soka

Ni miongoni mwa wachezaji walioanza kucheza soka wakiwa na umri mdogo. Hii ilitokana na ruhusa aliyopewa kutoka kwa wazazi wake ambao waliona kucheza soka kutasababisha mwanao asijiingize kwenye vitendo vichafu ikiwa ni pamoja na kutumia dawa za kulevya.

Hii iliwafanya wawe bega kwa bega naye, na alipofikisha umri wa miaka 10 walimsaidia kumuombea nafasi ya kwenda kufanya majaribio kwenye akademi ya PSG ambapo alifanikiwa kupita na kuanza kucheza kwenye timu za vijana.

Inaelezwa kwamba maisha ya utoto kwenye viunga vya Paris yalikuwa mazuri ikizingatiwa kilipokuwa kiwanja cha mazoezi na nyumbani kwao hakukuwa na umbali mkubwa.

Mchezaji huyo alionyesha kiwango bora akiwa kwenye akademi hiyo hadi alipofikisha umri wa miaka 14, ambapo ndipo ubora wake ulizidi kuonekana. Hatimaye timu mbalimbali ziliwasilisha ofa kwa ajili ya kuinasa saini yake ili ziende kumkuza kwenye akademi zao.

Kulikuwa na misururu ya timu kama Rennai na Caen, lakini mwisho aliamua kusaini Sochaux kwa sababu ndiyo ilikuwa ya kwanza kuwasilisha ofa na ilikuwa nono kuliko zote.

Hata hivyo, licha ya dili kuwa lilishakamilika, kabla hajasaini mama yake aliwaambia lazima atembelee miundombinu ya klabu kabla hajamruhusu mwanawe kujiunga nao.

Akisimulia Konate mwenyewe anasema: “Nilienda na mama kutembelea akademi yao ili kukagua miundombinu, mama alikuwa na wasiwasi kwa sababu hata shule sikuwa nimemaliza.”

Baada ya kukagua na kujiridhisha hatimaye mama huyo alimruhusu Konate kuanza kuitumikia timu hiyo ambapo muda huo alikuwa akiishi kwenye hosteli za timu, na akaondoka nyumbani kwao jambo ambalo lilikuwa gumu kwake, lakini ilibidi ajitahidi na kuzoea.

Nyota huyo alicheza hapo hadi ulipofikia muda wa kufuzu na kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza, lakini ghafla mambo yalibadilika kwa sababu alipata matatizo ya kiafya yaliyosababisha afanyiwe upasuaji na kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Baadaye alirudi na kupandishwa timu ya wakubwa, lakini ilibidi aanzie kwenye timu B.

Hapo pia kulikuwa na stori ya kuhuzunisha kwani hakupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, jambo lililomkasirisha na kuamua kuondoka.

“Niliamua kuondoka kwa sababu hata mmliki wa timu naye ilionekana kumshinda, mbaya zaidi hata kocha wa kikosi cha akiba, Albert Cartier ambaye ndiye alikuwa akitufundisha naye aliondoka. Mara hii nilipata ofa nyingi za timu barani Ulaya ikiwa ni pamoja na RB Leipzig,” anasema Konate.

Hatimaye baada ya kuondoka Sochaux mwaka huo huo 2017,

alijiunga na RB Leipzig kwa usajili huru na baada ya kutua hapo alipata shida katika msimu wake wa kwanza tu, lakini taratibu akaanza kuzoea na baada ya hapo amekuwa stori nyingine huku timu kibao zikihitaji saini yake kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Maisha na bata

Haijajulikana ikiwa Konate ana mchumba kwa sababu hajawahi kumuweka hadharani. Mara nyingi ambazo amekuwa akionekana huwa na panya wake ambaye amemfuga muda mrefu.