KIZUNGUMKUTI ANGUKO LA MAZEMBE NA UKUBWA WA NDOTO ZA DAJIDALI

Tuesday April 06 2021
mazeme pic
By Eliya Solomon

UNAWEZA usiamini kilichotokea lakini ndio ukweli huo kwamba mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe kutoka DR Congo, Ijumaa ya wiki iliyopita wametupwa nje ya mashindano hayo baada ya kupoteza mechi yao iliyopita ya Kundi B dhidi ya Chabab Belouizdad ya Algeria.

Mabao ya Amir Sayoud na Youcef Bechou ndio yaliyowafungashia virago Mazembe ambao walikubali kipigo cha mabao 2-0 na kilichobaki kwao ni kukamilisha ratiba tu ya kushiriki mashindano hayo ambapo watacheza mchezo wao wa mwisho wakiwa nyumbani dhidi ya Al Hilal.

Maelfu ya mashabiki wa TP Mazembe huko DR Congo, yamesikitishwa na kuvurunda kwa timu hiyo ambayo anaichezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu kwa awamu ya pili, ya kwanza aliichezea akiwa na Mbwana Samatta.

Akiwa Lubumbashi yalipo maskani ya TP Mazembe, Mtanzania, Dajidali Alli ambaye anaichezea Corbeaux FC, anaeleza vile mashabiki wa timu hiyo walivyochukizwa kutokana na kufanya vibaya kwa timu hiyo na kipi kimeiangusha.

“Mashabiki wengi wamechukia maana walitegemea kuona timu ikifanya vizuri, mambo yameenda tofauti na matarajio yao, kila mtu anaongea lake mtaani, wapo ambao wanaamini kocha aliishiwa mbinu, wengine wanasema wachezaji ndio ambao wamezingua kwenye mashindano,”

“Huu ni mwaka wa sita wamekuwa wakisikia ubingwa kwenye bomba, sio maisha ambayo wameyazoea maana miaka fulani walikuwa wakitesa, hasa wakati ambao Samatta alikuwa kikosini, lakini nadhani hiki ni kipindi cha mpito tu,” alisema.

Advertisement

Mara ya mwisho kwa TP Mazembe kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa 2015, waliifunga USM Alger ya Algeria kwenye michezo yote miwili ya fainali, wa kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 wakiwa ugenini halafu wakiwa nyumbani walitoa dozi ya mabao 2-0.

Samatta ambaye alikuwa mfungaji bora wa michuiano msimu huo akiwa na mabao saba, alitupia kwenye fainali zote mbili na kuondoka DR Congo huku akiwa amewaachia taji hilo kubwa Afrika na kwenda zake Ulaya ambako alitua KRC Genk.

Dajidali anasema wapo ambao wanamkumbuka Samatta kutokana na makubwa ambayo alifanya; “Wanashindwa kuelewa kuwa kuna vipindi lazima vitokee kwenye mpira, binafsi naona kama ubora wa Ligi yetu ya ndani unashuka ndio maana timu zetu zimeanza kuchemka.

“Ni kweli kuwa Ligi ya DR Congo ni bora ila sio kwa kiwango kama cha miaka kadhaa nyuma, wachezaji wengi wamekuwa wakikimbilia Ulaya, wale ambao wanaonekana kuwa bora, wanaenda Mazembe ndio maana karibu kila msimu wao ndio wanatwaa ubingwa wa Ligi ya ndani,” anasema.

Mtanzania huyo ambaye anacheza Ligi Daraja la Kwanza, anasema hali ya hewa ndani ya TP Mazembe imechafuka ndio maana alikuwa akikumbana na vizuizi vingi kila ambapo alikuwa akijaribu kutafuta nafasi ya kuonana na Ulimwengu.

Licha ya kuichezea Corbeaux FC ambayo inatajwa kuwa na mahusiano ya karibu na Mazembe, bado aliwekewa ngumu kutokana na presha kubwa ya kusuasua kwa klabu hiyo ambayo ilianza kwa kutoa sare mbili mfululizo.

“Tajiri Moise Katumbi atakuwa ameumizwa sana na kutolewa kwenye mashindano kwa Mazembe lakini ndio mpira, nadhani wanatakiwa kuangalia mbele na kuona namna gani wanaweza kusawazisha makosa yao,” anasema na kuongeza.

“Nasubiri hali ikitulia nitamfauta Ulimwengu na kuongea naye kama mdogo wake kwa sababu sote ni Watanzania, binafsi huwa namkubali sana maana huwa najifunza mambo mengi kutoka kwake, kuhusu kutetea ubingwa wa Ligi ya ndani sioni kama hilo ni suala la kuliongelea, hakuna wa kuwazuia.”

Pamoja na hayo ambayo yametokea, Dajidali anaamini kuwa ipo siku milango ya kheri itafunguka upande wake na kupata nafasi ya kuichezea TP Mazembe kama ambavyo amekuwa akimshuhudia Mtanzania mwenzake, Ulimwengu akikiwasha huko Lubumbashi.

Advertisement