KIBWANA: Kinda aliyehimili mziki wa Simba

Thursday July 15 2021
KIBWANA PIC
By Charity James

MASHABIKI wa Simba walitoka vichwa chini pale kwa Mkapa baada ya kuchapwa bao 1-0 na watani zao Yanga, ikiwa ni mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu.

Hakuna aliyeamini kilichotokea. Upande wa kulia wa Yanga ulikuwa salama chini ya miguu ya mchezaji aliyeonekana kuwa na umbile dogo zaidi kwenye mchezo huo mbali ya mshambuliaji Luis Miquissone. Huyu ni Kibwana Shomari.

Mbele ya Kibwana, nyota wa Simba Bernard Morrison na Clatous Chama aliweza kwenda nao sawa ingawa wanaonekana wasumbufu mbele ya wapinzani wao.

Kibwana alikuwa ukuta uliozuia dakika zote mashambulizi ya Simba yaliyofanywa ndani ya dakika 90, hali iliyosababisha hadi mwamuzi anapuliza kipyenga cha mwisho rangi ya nyekundu Simba wakiwa hawaamini.

Kibwana ni dabi yake ya kwanza kucheza akiwa na yanga, lakini kwa kile alichoonyesha ni kama mchezaji mzoefu ndani ya klabu hiyo ambayo msimu huu imejinyakulia pointi nne baada ya mzunguko wa kwanza kutoka sare ya bao 1-1 na mzunguko wa pili kuibuka na ushindi.

Tangu aanze soka la ushindani hakuwahi kupata kadi nyekundu na ni tangu aanze kucheza soka akisema siri kubwa ni nidhamu. Jamaa amekutana na matukio mengi, ila lile la Serengeti Boys na Wakongo hawezi kulisahau.

Advertisement

Katika mahojiano na Mwanaspoti amefunguka mengi kuhusiana safari yake ya kisoka hadi kufika Yanga.


DABI NI AKILI TU

Umri wake na kukosa uzoefu hakuna aliyeamini kama ataweza kufanya vizuri na kuisaidia timu yake kupata matokeo chini ya watani zao. Mwenyewe anasema haikuwa kazi rahisi kupambana dakika 90.

“Mpira ni akili na sio nguvu, nadhani kilichotokea upande wangu mpira ulikuwa rahisi kwa sababu nilitumia akili zaidi na sio nguvu, ukifuatilia utanielewa,” anasema beki huyo aliyemweka nje Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye pia jina lake lilikua kutokana na mchezo wa dabi.


NIDHAMU, KUJITUMA YANGA

Kibwana anasema ndoto za wachezaji wengi ni kucheza timu hizo kongwe kwenye soka na ili ufikie malengo ya mashabiki wa timu hizo ni kutwaa mataji mara kwa mara tofauti na timu nyingine zinazoshiriki ligi. Amefunguka kuwa kucheza timu hizo ni rahisi.

“Kila mchezaji ndoto ni kunyanyua kwapa, kwa Simba na Yanga ni rahisi sana kutokana na usajili wanaoufanya, malipo kwa wachezaji na huwezi kucheza timu hizi kama nidhamu yako mbovu na sio mtu wa kujituma mazoezini na hata pale unapopewa nafasi ya kucheza.”

NJIA YA KIMATAIFA

Kuhusu timu yake msimu huu, Kibwana anasema yapo matumaini makubwa kimataifa watatesa, lakini binafsi anajiandaa pia kuuwasha mwingi.

“Achana na ubingwa ambao haupo mikononi mwetu, bado tuna nafasi ya kushiriki kimataifa, nadhani pamoja na kutoka sana na timu za vijana bado naamini nina nafasi ya kutoka nikiwa Yanga kwa sababu akili sasa imekomaa, nacheza mechi nyingi za ushindani.

“Sijajua ni nchi gani nitaenda ila mipango yangu ni kutoka Tanzania na kwenda kujaribu soka la kulipwa nje natamani kuyaishi maisha ya Kelvin John, ni kijana ambaye amepata mafanikio makubwa akiwa na umri mdogo baada ya hivi karibuni kujiunga na KRC Genk ya Ubeligiji,” anasema


MECHI BORA

Anasema mechi dhidi Congo Brazzaville iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 18, 2016 ndiyo ilikuwa bora kwake iliyoisha kwa ushindi wa mabao 3-2.

“Ilikuwa mechi ya kufuzu Afcon ya under- 17, ilikuwa mechi yangu bora kwani ilikuwa na ushindani mkubwa sana,” anasema Kibwana.


UNDER 17 GABON NOMA

Hii ni mechi ambayo Kibwana hataisau. Ilikuwa mechi na Niger, ambapo Serengeti Boys ilitakiwa kushinda ili kufuzu Kombe la Dunia, lakini kilichotokea kwao ni majonzi kwake.

“Mechi ya mashindano ya Under- 17 Gabon ilikuwa mechi na Niger ya mwisho, tukitoka sare tunafuzu Kombe la Dunia lakini tulifungwa bao moja sitakuja kusahau hicho kitu.”


KIPAGWILE MTIHANI KWAKE

Kibwana anamtaja Iddi Kipagwile kama mchezaji ambaye anamsumbua sana uwanjani kwani akikutana naye nyasi huwa hazina amani, unaweza kuhisi kuna vita vya tatu ya dunia.

“Ni mchezaji mzuri, ana nguvu anacheza kwa akili kumkaba unatakiwa ujipange sana,” anasema


SH15,000 YAMUINGIZA UWANJANI

Wakati anaanza maisha ya soka, Kibwana amewahi kucheza ndondo na posho yake ya mechi hiyo ilikuwa ni Sh15,000 anayosema ilimsaidia kununua baadhi ya vifaa vya mazoezi.

“Nilicheza ndondo, ilikuwa ligi ya jezi nilipata 15,000 ambayo ndio niliitumia kununua vifaa vya mazoezi timu ya Black Vibe nilipopata pesa nikaenda kununua vifaa vya mazoezi.”


KAPOMBE, ABDUL FRESH

Kibwana anasema wachezaji Juma Abdul aliyekuwa anaichezea Yanga na Shomary Kapombe wa Simba ndio anaowakubali zaidi hapa nchini.

“Kwa ndani namkubali na navutiwa na Kapombe, Abdul na Salum Kanon kwa nje Dani Alves na Alexandra Anord,” anasema.

Kibwana ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi, yeye anafafanua zaidi: “Naweza kucheza kiungo wa pembeni, pia namba 2,3 hata hizo namba za pembeni nacheza zote 7, 11.”


KADI NYEKUNDU MOJA

Kibwana anaonekana kuwa mchezaji mwenye nidhamu na anayejitambua pia. Katika maisha yake ya soka amepata kadi nyekundu moja tu tena akiwa na timu ya watoto.

“Ni muda mrefu sana kwenye academy ‘Morogoro Youth’ ilikuwa mechi ya ligi ya jezi mechi ilikuwa na timu inaitwa Sida,” anaeleza na kwamba hakumbuki alifanya kosa gani.


FAMILIA YATOA BARAKA

Mchezaji huyo anasema wazazi wake wamempa bakara kutumia kipaji chake kuendesha maisha yake.

“Baba yangu tangu zamani alikuwa anapenda sana mpira haikuwa changamoto kumwambia nataka kucheza mpira, yeye ndio alikua kipaumbele,” anasema.

Anasema baba alimkazania kutimiza ndoto zake za kuwa mchezaji na wakati mwingine alihusika kumnunulia baadhi ya vifaa vya mazoezi.

Baba yake alisoma Shule ya Kibasila na alicheza Yanga B miaka ya nyuma hapo alipochaguliwa kupandishwa babake akapata matatizo ambayo hakutaka kuyaweka wazi huku akimwambia ndio chanzo cha yeye kuacha soka.

“Hajawahi kuniambia, nimefuata nyayo zake zaidi anasema vijana wengi wa sasa hatujui mpira kama miaka yao ya zamani huku akisisitiza kuwa wangekuwa wanalipwa vizuri zamani kama sasa angekuwa mbali kimaisha,” anasema Kibwana.

“Baba yangu alikuwa anacheza namba 10, hata watu wangu wa karibu walisema baba yangu alikuwa anajua sana mpira.”


ALIKOTOKA

Baada ya kucheza Academy ya Moro Youth alichaguliwa timu ya Mkoa wa Morogoro mashindano ya Copa Coca Cola yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

“Nilichaguliwa timu ya Taifa chini ya miaka 15, pia nikapelekwa Under- 17 timu ya taifa na nikajiunga Mtibwa Sugar U-20 na baadaye nilipandishwa timu ya wakubwa ndipo Yanga waliniona huko,” anasema na kuongeza kuwa sasa anakipiga Yanga na kujituma akitambua kuna maisha baada ya soka.

Advertisement