Kangwa beki anayetoa funzo Ligi Kuu Bara

Muktasari:

MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2016/17, Azam FC iliingia sokoni kutafuta beki wa kushoto wa kusaidiana na Gadiel Michael ambaye kwa sasa anakipiga Simba.

MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2016/17, Azam FC iliingia sokoni kutafuta beki wa kushoto wa kusaidiana na Gadiel Michael ambaye kwa sasa anakipiga Simba.

Jicho la mabosi wa Azam lilitua nchini Zimbabwe kwenye timu ya Highlanders FC na kumuona Bruce Kangwa na kumsajili.

Ujio wa Kangwa ulikuwa wa kimya kimya lakini baada ya kuanza kucheza, watu majukwaani walimuimba kutokana na kiwango bora alichokionyesha jambo lililomfanya Gadiel akae benchi kabla ya kutimkia Yanga msimu uliofuata.

Kangwa anasimulia maisha yake ya soka alipofanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

Anasema alianza kucheza soka mtaani kama ilivyo kwa wachezaji wengine na baadaye alijiunga na Highlanders

“Hata mimi nilianzia mtaani kwetu ambapo nilizichezea timu nyingi na baadaye kusajiliwa Highlanders mwaka 2009 nilipodumu kwa miaka sita kabla ya kuja Azam,” anasema Kangwa.


AMTAJA PETER NDLOVU

Moja ya majina ambayo si rahisi kusahaulika nchini kwao kwenye soka ni Peter Ndlovu, mshambuliaji wa zamani wa Highlanders, Coventry City, Birmingham City, Huddersfield Town, Sheffield United, Mamelodi Sundowns, Thanda Royal Zulu, Highfield United na Black Mambas kuwa ndiye alimfanya Kangwa kupenda soka kulingana na ubora na mafanikio aliyoyapata wakati akicheza.

“Nilishawishika kucheza soka nilivyomuona Ndlovu, alikuwa bora zaidi pia alipata mafanikio na kuufanya mpira usionekane mchezo wa kihuni.”


MAISHA AZAM

Amedumu Azam zaidi ya miaka minne sasa na anasimulia namna maisha yalivyo huku akielezea machungu yake ya kushindwa kutwaa taji la ligi tangu ajiunge.

“Maisha ya Azam yako poa, nimejifunza mengi kupitia timu hii. Nimejifunza utamaduni wa Tanzania na soka lake pia nimeongeza marafiki wengi chanya, nafurahi kuwa hapa na sina kinachoniuma zaidi ya kukosa ubingwa Ligi Kuu, inauma sana lakini bado hatujapoteza matumaini tunaendelea kupambana.

“Sio kwamba sipati ofa nyingine, hapana! naangalia maslahi yangu kwanza na hadi sasa Azam bado ni timu bora zaidi kwangu na nitaendelea kuitumikia kwa moyo wangu wote,” anasema.


SIMBA, YANGA USIPIME

Kuhusu wachezaji wanaompa shida timu yake inapokutana nao kwenye michuano mbalimbali.

“Kila tukikutana na Simba au Yanga lazima mechi iwe ngumu, hizi ndio mechi ambazo siwezi kuzisahau, kingine nipo tayari wakati wote hivyo hakuna mchezaji ninayemhofia lakini baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga wapo vizuri na wanatoa changamoto kidogo.

“Hauwezi kuwa mkubwa bila changamoto, achana na kupata majeruhi, hadi kufika hapa nimepitia changamoto nyingi na nyingine ni ngumu sana ambazo siwezi kuzitaja hapa, haikuwa rahisi kufika hapa bali tumekwepa mishale mingi,” anaeleza


DUBE KAMA MESSI

Kuhusu mchezaji wake bora kwa sasa, beki huyo hakusita kuweka wazi kwamba ni Mzimbabwe mwenzake Prince Dube ambaye ni kinara wa kufumania nyavu akiwa na mabao 14 na kwa nje alimtaja Lionel Messi.

Pia aliwataja Yakub Mohammed raia wa Ivory Coast na Mzimbabwe Never Tigere wote wa Azam kuwa wachezaji wengine anaokubali ubora wao.


FAMILIA IPO CANADA

Pamoja na kuwa yeye ni raia wa Zimbabwe na sasa anacheza soka nchini, lakini familia yake ipo nchini Canada na anaeleza kuwa ana mke na mtoto mmoja.

“Mke wangu ni raia wa Canada hadi sasa tumebahatika kupata mtoto mmoja wa kiume kama Mungu akijaalia ipo siku watakuja Tanzania,” anasema.


MSOSI NI WALI KUKU

Nyota huyo aliyekuwa na kikosi cha Zimbabwe kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 nchini Gabon anaweka wazi kuwa msosi wake mkuu ni wali na kuku ingawa chakula kingine pia anakula.

“Tanzania kuna misosi mingi mitamu ambayo napenda kula lakini hadi sasa nimevutiwa sana na wali-kuku, napenda sana kula aina hiyo ya chakula kuliko kingine chochote,”


NDOTO ZA

KIBINGWA

Kati ya vitu ambavyo wachezaji wengi wanaota ni kucheza ligi nje ya Afrika lakini Kangwa anatamani anatamani kubeba makombe ya mashindano mengi kabla hajastaafu.

“Makombe yana thamani sana, natamani kushinda makombe mengi makubwa kuliko kuhamahama timu, malengo yangu ni hayo pamoja na kuwa msaada kwenye timu ya Azam na Zimbabwe,” anasema.