JICHO LA MWEWE: Simba ya 2003 vs Simba ya leo

ZAMANI huwa inachekesha sana. Kitu chochote cha zamani huwa kina thamani. Umewahi kujiuliza, ni wachezaji wangapi wa kikosi cha Simba cha sasa ambao wangeingia katika ‘first eleven’ ya kikosi cha Simba kilichoitoa Zamalek michuano ya Afrika mwaka 2003?

Utafumba macho na kuwafikiria mastaa kibao wa wakati ule. Vipi kuhusu Ulimboka Mwakingwe? Vipi kuhusu Marehemu Christopher Alex? Kina Victor Costa, Boniface Pawassa, Suleman Matola ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi, Ramadhan Wasso, Said Swedi na wengineo wengi.

Unapata wakati mgumu kufikiria ni mastaa gani wa sasa wa Simba wangecheza kikosi kile. Lakini fumba macho pia waza mastaa wa sasa wa Simba. Ni mastaa wangapi wa wakati ule wangepata nafasi katika kikosi cha sasa. Hiki kikosi cha kina Luis Miquissone, Clatous Chama, Bernard Morrison, Pascal Wawa na wengineo wengi.

Baadhi ya watu wa zamani wangedai kwamba kikosi kile kilikuwa bora zaidi. Huu ni uzamani. Uzamani unapendwa. Ukweli ni kwamba hauwezi kurudisha nyuma nyakati lakini naamini kikosi hiki cha Simba ni bora kuliko kikosi kile cha Simba. Nitazua mjadala na wale waliokipenda kikosi cha zamani watakuwa na hoja zao.

Kwanza kabisa kikosi kinatandaza zaidi soka. Wanamiliki mpira. Ukitazama jinsi ambavyo Simba waliwafunga Al Ahly majuzi ni kwamba kuna nyakati nyingi za mechi walikuwa wakikaa na mpira zaidi na kutengeneza nafasi. Hawakubahatisha kuwafunga Al Ahly. Walitawala takwimu nyingi za mechi.

Simba ile ya mwaka 2003 ilicheza kwa kusaka matokeo zaidi. Haikuwa ikitawala mechi. Pambano lao dhidi ya Zamalek pale Cairo walishindwa walau kupiga pasi sita mfululizo. Sioni hili likitokea kwa Simba hii. Wanaweza kushinda, kufungwa au kutoka sare lakini sioni kama wanaweza kutawaliwa kulikopitiliza kama usiku ule wa mwaka 2003.

Hoja kubwa ambayo haina jibu kamili hapa ni kama Waarabu hawa wa leo ni bora kule wale wa wakati ule. Hatujui vema lakini kwa sasa Al Ahly ndio timu bora Afrika. Swali ni je, kiwango cha soka Afrika kimepungua au kipo vile vile? Hili ni swali gumu. Simba hii ingecheza na Zamalek ile maisha yangekuwa tofauti? Sina jibu la moja kwa moja.

Lakini tuangalie wachezaji mmoja mmoja. Shomari Kapombe anaweza kuwa zaidi ya Said Swedi. Sina shaka. Mohammed Hussein Tshabalala anaweza kuwa zaidi ya Ramadhan Wasso. Sina shaka. Pale katikati naamini mpaka leo Victor Costa angecheza.

Kuna watu wawili ambao naamini wangecheza katika safu ya ulinzi mpaka sasa. Kipa Juma Kaseja na mlinzi wa kati, Victor Costa. Tatizo kuanzia eneo la kiungo kwenda mbele maisha yangekuwa magumu kwa wengineo. Sawa Ulimboka Mwakingwe alikuwa bora lakini sidhani kama ana uwezo wa Luis Miquissone.

Lakini pia katika kikosi kile sijaona mchezaji ambaye ana ubora wa Clatous Chama. Huu ndio ukweli ambao wengi hawatakubali kuumeza kwa sababu wanadamu tumezaliwa tukiupenda zaidi uzamani kuliko usasa. Ipo katika fani zote katika maisha yetu.

Kikosi cha sasa cha Simba kitakubalika zaidi miaka 20 ijayo. Wakati huo watu watakuwa wakiwazungumzia akina Chama katika ulimi tofauti zaidi na sasa. Mechi hizi dhidi ya akina Al Ahly zitakumbukwa zaidi kama ambavyo kila siku tunalikumbuka vema pambano la Simba na Zamalek la mwaka 2003.

Zamani niliwahi kujadili hili jambo na Mwanamuziki maarufu wa zamani wa Twanga Pepeta, Ally Choki. Wakati huo Twanga walikuwa wanatamba na nyimbo nzuri kama ‘Jirani’, ‘Chuki binafsi’, ‘Aminata’ na nyinginezo. Hata hivyo watu wengi walikuwa wanawaponda Twanga Pepeta pindi walipokuwa wanawalinganisha na bendi mbili kongwe, Sikinde na Msondo. Nakumbuka Choki aliniahidi kwamba nyimbo zao Twanga Pepeta zitaheshimika zaidi baada ya miaka mingi ijayo. Ni kweli nyimbo zile ukizisikia leo unapata hisia za ajabu. Labda kwa sababu nyakati zimepita na tayari nyimbo hizo zimeingia katika kundi la nyimbo za zamani.

Tabia hii ya kuupenda uzamani katika soka huwa inanishangaza wakati mwingine. Nawafahamu washambuliaji wengi wa zamani ambao walikuwa hawafiki hata nusu ya ubora wa Mbwana Samatta lakini wanavyozungumzwa ni kama vile walikuwa bora kuliko Samatta kitu ambacho sio cha kweli.

Kuna mawinga wengi wa zamani hawakuwa na akili ya Simon Msuva lakini kila winga wa zamani inaonekana kama vile alikuwa hatari zaidi ya Msuva. Unachoka zaidi pale unapojikumbusha kwamba Samatta na Msuva wamefanya mambo makubwa zaidi ughaibuni lakini bado tuna mastaa wengi wa kawaida wa zamani utajwa kuwa bora kuliko wao.

Nadhani ni hulka ya wanadamu kuvipenda zaidi vizazi vyao. Naamini hata sasa hivi kuna wachezaji wengi wa kawaida ambao tutakuwa tukiwamwagia sana sifa siku za mbele lakini kwa sasa ni wachezaji wa kawaida tu. Tabia hii inaanzia kwa mchezaji mmoja mmoja na kisha inaamini katika kundi la wachezaji.

Nafungua mjadala nikiamini kikosi hiki cha Simba ni bora kuliko kile cha mwaka 2003. Eneo pekee ambalo linanipa tabu ni lile la kulinganisha kikosi hiki na kile cha mwaka 1993 ambacho kilifika fainali za CAF. Kundi la kina Edward Chumilla na wenzake linahitaji kujadiliwa kwa heshima zake. Lilibeba nyota wengi wakali.