JICHO LA MWEWE: Sarakasi za maisha ya Akpan leo yupo Ihefu

VICTOR Akpan ametolewa kwa mkopo kwenda Ihefu ya Mbarali kule Mbeya. Maisha yake ya soka ndani ya miezi sita iliyopita yamekwenda kama filamu. Utaamua mwenyewe kucheka au kununa.

Akpan alifika katika viwanja vya mazoezi vya Azam pale Chamazi mwishoni mwa msimu uliopita. Alikuwa na jopo la watu wa Coastal Union ambao walikuwa wanataka kumuuza kwenda Azam. Kwa utaratibu wa Azam shughuli zao za mambo ya soka huwa zinafanywa katika ofisi zao pale Mzizima na sio Chamazi.

Ikapigwa simu moja kwamba msafara wa Akpan unapaswa kwenda Mzizima na sio Chamazi. Mabosi wa Azam walikuwa ofisini Mzizima kumsubiri Akpan ili wamalizane naye. Wangeweza kuendelea kusubiri hadi leo. Unajua kitu gani kilitokea?

Wakati msafara wa Akpan ukitoka Chamazi kuelekea Mzizima, Simba walitonywa kwamba Akpan anakaribia kusaini Azam.

Ikapigwa simu ya haraka kwenda kwa Akpan na watu wake. Akpan akabadili mawazo. Alisikika akiwaambia watu ndani ya gari kwamba Simba ilikuwa timu bora kwake kuchezea kwa sababu wanacheza mechi nyingi za kimataifa na itakuwa rahisi kwao kumtangaza kuliko Azam.

Hii ni akili ya Wanigeria na wachezaji wengi wenye mtazamo wa mafanikio.

Safari ya kwenda Mzizima ikafia njiani. Gari likakata kona kuelekea ofisi za watu wa Simba. Walichokuwa wanataka watu wa Coastal ni hela tu ya mauzo ya mchezaji. Hawakujali sana anapokwenda. Dili la kwenda Azam likafa. Mchezaji akasaini Simba. Sijui kiasi alichopewa, lakini najua Coastal walipewa Shilingi 10 milioni. Mchezaji mwenyewe nasikia alipewa kiasi kama hicho cha pesa.

Sijui ni kitu gani ambacho Simba na Azam walikiona kwa Akpan, lakini tunavyozungumza ni ndani ya miezi sita tu anacheza kwa mkopo katika klabu ya Ihefu kule Mbeya.

Simba wamepigwa na hasara mbaya. Swali linarudi pale pale, Simba na Azam waliona kitu gani kwake? Inawezekana angekwenda Azam hadithi ingekuwa tofauti? Tatizo lake Simba lilikuwa timu yenyewe au mchezaji mwenyewe? Angekuwa mchezaji wa Kitanzania tungeweza kuhisi jambo lakini kwa mchezaji wa kigeni hii sio kawaida.

Mara zote tunaamini wachezaji wazawa wakisaini Simba na Yanga huwa wanaridhika. Wengine wanaanza kunenepa. Wengine wanaanza kutanua makwapa. Haiwezekani kama hii ilitokea kwa Akpan.

Wanaijeria ni wapambanaji hasa. Hawana masikhara na maisha. Ni wazi Akpan aliingia Simba akiwa amepania hasa.

Akaenda zake Misri katika kambi ya maandalizi ya msimu. Nuksi ilianzia kule. Kocha wake wa kwanza Simba, Zoran Maki akamkataa. Viongozi wa Simba wakapigwa na butwaa.

Mwanzoni walidhani masikhara. Hata hivyo msimamo wa kocha uliendelea kubakia kama ulivyo. Simba wakaanza kuhisi hasara mapema.

Kilichonishtua ni pale alipokuja Juma Mgunda. Huyu jamaa alikuwa amefanya kazi na Akpan pale Tanga. Kama kuna kitu Simba walikiona kwa Akpan basi ni kwa sababu ya Mgunda. Katika kikosi chake alikuwa panga pangua. Niliamini kuwasili kwa Mgunda ungekuwa mwanzo wa Akpan kutamba Msimbazi. Haikutokea.

Mgunda wake akaendelea kumpiga benchi. Labda Mgunda alihisi kwamba ingeonekana anampendelea mchezaji aliyetoka naye Tanga. Hata hivyo mbona Mgunda alishachukua maamuzi ya kuwaacha baadhi ya wachezaji nje? Mmojawapo alikuwa Pape Sakho.

Baada ya Mgunda akaja kocha wa sasa Mbrazil, Robertinho. Huyu naye amekaa mazoezini na Akpan kwa siku kadhaa. Amekwenda naye hadi Dubai. Na yeye akaungana na Zoran pamoja na Mgunda kutoona chochote kutoka katika miguu ya Akpan. Hatimaye ametolewa kwa mkopo kwenda Ihefu.

Sio yeye peke yake. Hata Nelson Okwa ametolewa kwa mkopo kwenda Ihefu. Sitaki kumzungumzia Okwa kwa sababu siifahamu vizuri dili yake. Najiuliza maswali kuhusu Akpan tu. Nani alikatisha safari yake kutoka Chamazi kuelekea Mzizima ambako ilikuwa asaini Azam? Aliona nini kutoka kwa Akpan? Chochote alichokiona basi kimeipa Simba hasara ya shilingi 200 milioni. Huu ndio ukweli unaouma. Si ajabu jumba bovu ilibidi liwaangukie Azam.

Ni kweli wakati mwingine wachezaji hufeli pindi wanapohama sehemu moja kwenda nyingine. Katika soka uhamisho ni bahati nasibu tu. Unaweza kufeli na unaweza kufanikiwa. Lakini kwa nini Akpan amefeli mazoezini? Alianza kufeli akiwa mazoezini kule Misri. Walau angeanza kufeli katika mechi.

Alianza kufeli katika macho ya makocha kabla mashabiki wa Simba hawajamuona akiwa amevaa jezi yao. Ni kitu cha kushangaza. Mara nyingi wachezaji ufeli wakiwa wamevaa jezi lakini kwa Akpan imekuwa tofauti.

Baadaye alikuwa akipewa dakika chache katika mechi lakini hakuweza kumshawishi yeyote ndani na nje ya Simba.

Nadhani ianze kuwa funzo kwa viongozi wetu wa mpira. Waache kukurupuka. Wachezaji wengi wamepata pesa nyingi za usajili kwa sababu tu imesikika wanatakiwa na wapinzani.

Tabia hii ya kukurupuka sidhani kama itaisha. Timu hazisajili kwa malengo na badala yake huwa wanachungulia mchezaji ambaye anatakiwa na wapinzani.

Nitakusimulia kichekesho kingine kuhusu uhamisho huu wa Akpan. Coastal Union waliishia kuwa washindi kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya filamu ambayo waliitengeneza kupitia kwa mchezaji anayeitwa Abdul Suleiman ‘Sopu’. Huyu alitumika kuhakikisha Simba inaweka haraka pesa za Akpan katika akaunti ya Coastal Union.

Ilikuwa hivi. Simba walimsaini Akpan bila ya kuweka shilingi 100 milioni katika akaunti ya Coastal Union. Lakini hapo hapo wakajikuta katika vita ya kumuwania Sopu na Azam baada ya staa huyo kufanya vyema katika pambano la fainali dhidi ya Yanga pale Arusha. Sopu alikuwa na mkataba na Coastal.

Hata hivyo, Azam walifanikiwa kumsainisha Sopu kabla ya Simba lakini watu wa Simba hawakujua. Coastal wakatumia mwanya huo kuwaambia Simba kwamba hawawezi kufanya nao kabla hawajamalizana katika dili la Akpan. Hapo ndipo Simba walipolazimika kuweka pesa ya usajili ya Akpan kwa haraka ili wampate Sopu.

Mara tu Simba walipoweka hela ya Akpan katika akaunti ya Coastal Union Wagosi hao wa Kaya wakairuhusu Azam kumtangaza Sopu. Kwa mara nyingine tena Coastal walikuwa wamepata msaada wa mbio za wakubwa kukimbizana katika harakati za usajili wa wachezaji. Leo mchezaji yupo Ihefu kwa mkopo.