JICHO LA MWEWE: Mkude angeteta na Chuji kwa dakika kumi tu

Muktasari:

MARA ya mwisho kumsikia rafiki yangu Athuman Idd ‘Chuji’, nadhani ilikuwa msimu uliopita. Alikuwa anaichezea timu iliyotawaliwa na njaa Singida United. Wakacheza na Coastal Union pale Singida. Mpira ulipoisha akaondoka na basi la wapinzani wao yaani Wagosi wa Kaya kurudi Tanga!

MARA ya mwisho kumsikia rafiki yangu Athuman Idd ‘Chuji’, nadhani ilikuwa msimu uliopita. Alikuwa anaichezea timu iliyotawaliwa na njaa Singida United. Wakacheza na Coastal Union pale Singida. Mpira ulipoisha akaondoka na basi la wapinzani wao yaani Wagosi wa Kaya kurudi Tanga!

Rafiki yangu mwingine, Jonas Mkude amuulize Chuji kuhusu maisha haya. Maisha ya kukaa bila ya timu. Au wakati mwingine maisha ya kuchezea timu ndogo. Yanakuwa maisha ya kijinga kweli kweli.

Majuzi nasikia Mkude amewasumbua tena Simba. Makosa ni yale yale tu. Ndani ya miezi sita mara mbili amepelekwa katika Kamati ya Maadili. Ukiulizia kuhusu makosa unaambiwa yale yale tu ya kuchelewa kambini, kuzima simu na mengineyo.

Kama Mkude akiweza kuteta mambo mawili matatu na Chuji ambaye naamini ni rafiki yake, atamshauri vitu vingi. Ukiwa staa mkubwa wa Simba au Yanga ni rahisi kuona maisha haya ya raha ni ya kudumu. Maisha ya kupendwa, maisha ya kupata pesa kwa urahisi, maisha ya kuhudumiwa vema kama mrembo mzuri katika kundi la wanaume wenye pesa.

Kinachomsumbua Jonas kwa sasa ni muda. Anapata shida kupanga muda wake binafsi na muda wa timu. Anataka mambo yote mawili yaende kwa wakati mmoja. Wachezaji wengi wa kulipwa (Professional) duniani huwa wanaishi maisha ya mateso.

Wachezaji wanatamani sana pombe na pia wanawake. Wanatamani starehe. Zaidi ya hivyo wana pesa mifukoni. Kinachokosekana huwa ni muda. Na hapa ndipo inapohitajika kafara kubwa ya kuwa mchezaji wa kulipwa. Hauwezi kuishi maisha ya Mwanasheria au Mwalimu. Kazi yako ni ya matumizi ya nguvu zaidi.

Wachezaji wengi wanajikuta wakitumia muda mwingi zaidi katika kulimbikiza pesa zao na kufanya matanuzi kwa wiki mbili au tatu wakati msimu unapofika tamati. Baada ya hapo wanarudi kazini. Vinginevyo maisha ya wikiendi yanakuwa magumu kwa sababu wanahitajika zaidi kazini.

Kina Cristiano Ronaldo wana pesa nyingi, lakini wanaishi maisha haya ya mateso. Unaamka, unaenda mazoezini, Jumamosi unacheza mechi, Jumapili kocha anawaita kwa ajili ya kufanya kitu kinachoitwa ‘recovery’, yaani kuurudisha mwili katika hali nzuri.

Jumatatu unarudi tena katika mazoezi na maisha yanaendelea. Haya yanatokea wakati wenzetu hawakai hata kambini, lakini wanaheshimu ratiba. Haya yanatokea wakati kina Ronaldo wanamiliki ndege binafsi, magari ya kifahari, boti za kifahari lakini hakuna wanachoweza kufanya zaidi ya kuheshimu ratiba ya kazini.

Hili jambo linaonekana kumshinda Mkude. Hata hivyo kama akiteta na rafiki yake Chuji atamwambia tu, kwamba kumbe mpira ukiisha mguuni yanajitokeza mambo mengi. Kwanza kabisa muda unakuwepo mwingi tu. Tatizo pesa inakosekana kwa sababu mbalimbali.

Kwanza wachezaji wetu wanashindwa kuwekeza vema, lakini pia wengi hawana shule kwa sababu muda ambao walipaswa kusoma ndio huo huo walikuwa wanautumia kwa kucheza soka. Halikuwa kosa. Kosa ni kutotumia akili katika maisha ya soka.

Mastaa wengi wa zamani walikuwa wasumbufu kama hivi, lakini baadaye wamekuja kugundua kwamba ni bora wangekuwa na nidhamu na juhudi wakati wanacheza soka ili wafike mbali kisoka, wapate pesa nyingi na mwishowe wafanye uwekezaji mkubwa kwani mwisho wa soka, muda wa kupumzika na kulewa unapatikana sana, lakini tatizo linakuwa pesa.

Mkude anaweza kuteta na Chuji amwambie tu, jinsi ambavyo hawa mashabiki wengi wanao ambao wanamhusu kwa sasa watamkimbia. Mashabiki ni wanafiki. Wanakupenda pale ambapo unakuwa hodari uwanjani. Unaweza kudhani utaishi maisha hayohayo pindi ukistaafu lakini wapi.

Ukiachwa tu na hizi timu wale mashabiki wenye uwezo wa kipesa ambao ni wafanyabiashara na wafanyakazi wenye vipato hawapokei simu zako. Hili Chuji hawezi kumficha Mkude kwa sababu nina uhakika wa asilimia 100 kwamba linamtokea na amewahi kuniambia.

Kama ambavyo mashabiki sasa hivi wanavyotamani kupiga picha na Mkude basi ndivyo hivyo hivyo ambavyo mashabiki walikuwa wanatamani kupiga picha na Chuji. Na kabla ya Chuji walikuwa wanatamani kupiga picha na kina Hamis Gaga na Said Mwamba.

Ni suala la ratiba ya ustaa tu. Hizi timu wamepita mastaa wengi na hawataacha kupita. Kinachotokea ni zamu tu na ndio maana sasa hivi ni zamu ya Mkude. Hata hivyo zamu yako inapofika inabidi uwe makini kweli kweli na ujifunze kupitia kwa wale ambao walikuwa mastaa.

Bahati nzuri Mkude asijifunze kupitia kwa mastaa wa zamani sana. Ajifunze kupitia mastaa wa karibuni tu kama kina Chuji. Asiende kwa kina Athuman China, atete kidogo tu na Chuji atamwambia jinsi ambavyo anahitaji kuwa na nidhamu kwa sasa.

Hili ni la kwake mwenye Mkude, lakini kuna jingine ambalo linatuhusu sisi wengine wenye uzalendo na taifa. Mkude ni mmoja kati ya wachezaji wachache wazawa wanaotuwakilisha vema katika timu kubwa inayofanya vizuri nchini Simba.

Hii Simba imetawaliwa na mastaa wengi wa kigeni ambao wamekuwa roho ya timu. Wawakilishi wetu ambao wanaingia katika kikosi cha timu ya taifa ni Mkude mwenyewe, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein, John Bocco na Shomari Kapombe.

Mkude akiondoka Simba ataiidhoofisha Stars, kwani ataondoka katika mechi nyingi za kimataifa ambazo anapata sasa hivi. Hii ni hasara kwa taifa. Bahati mbaya ni kwamba Mkude akiondolewa Simba ni wazi kwamba timu hii yenye noti kwa sasa itasaka mchezaji wa kigeni wa kucheza nafasi yake.

Tungependa wachezaji wazawa wanaotamba katika timu hizi wasifanye makosa ya kuachia nafasi kwa sababu timu yetu ya taifa bado imeendelea kutegemea zaidi wachezaji wa ndani. Nje tuna idadi chache ya kina Mbwana Samatta.