JICHO LA MWEWE: Filamu ya Manara, Barbara inavyovutia watazamaji

SAHAU kuhusu kilichotokea jana pale mwisho wa Reli Kigoma. Kulikuwa kuna mechi ya ‘pili’ baina ya Simba na Yanga, lakini siku chache kabla ya hapo kulikuwa na mechi ya kusisimua kati ya Msemaji wa Simba na Bosi wake.

Sijui kama tumuite Msemaji au tuseme aliyekuwa msemaji kwa sababu suala la yeye kuachia ngazi bado linatuchanganya. Hatujui kama ameondoka rasmi au bado yupo. Hakuna kitu rasmi. Tunachojua ni kwamba kila kitu kilikuwa kimefukiwa kwa muda kuelekea pambano la jana Kigoma.

Siku chache kuelekea pambano hili, Haji Manara akiwa kama Msemaji wa Simba alisikika katika ‘clip’ iliyoenea katika mitandao ya jamii akimbwatukia vikali Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo aliye pia bosi wake, Barbara Gonzalez kwa kile alichoeleza kwamba mtendaji huo au tumuite CEO, alikuwa amemzushia mambo mengi mazito kuhusu kuhujumu klabu hiyo.

Hujuma zilionekana kuwa nzito. Kwamba Manara alikuwa yuko karibu na watu wa Yanga kuelekea katika pambano la jana pale Kigoma. Ndio, Manara ana urafiki wa karibu na tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohammed anayemiliki wa kampuni ya GSM inayoisimamia Yanga kwa karibu kwa sasa.

Kwamba Manara alikuwa ameonekana Posta katika Ofisi za GSM na kisha Kigamboni ambako Yanga inaweka makazi yake siku zote. Unaweza kuguna, manara huyu huyu ambaye kila siku anainanga Yanga mitandaoni na kwingineko kumbe anaweza kuiuza Simba kwa Yanga?

Naweza kuwa mtu wa mwisho kuamini kwamba Manara anaweza kuihujumu Simba. Nimemjua Manara siku nyingi kiasi cha kuweza kuamini kwamba anaweza kujipatia pesa kwa matajiri wa wapinzani bila ya kuihujumu Simba. Mdomo huo anao.

Tutarudi huko baadaye. Kuna maswali mengi ya msingi yanajitokeza katika filamu hii. Simba ni timu ya kwanza kujinasibu kwamba inakwenda katika mabadiliko makubwa ya kiutawala na utendaji lakini bado wana safari ndefu ya kufika katika nchi ya ahadi.

CEO ni mtu mzito katika klabu. Manara anawezaje kumbwatukia CEO wake kiasi kile? Hata kama hakutaka sauti yake ifike katika masikio ya wengine, lakini hata kwa maongezi binafsi tu kulipaswa kuwa na chembe chembe za heshima baina yao hata kama mmoja wao alikuwa amekosea. Sauti ilikuwa kali na kulikuwa na vitisho vikubwa baina yao. Usingedhani kwamba mfanyakazi wa kawaida alikuwa anaongea na CEO wake.

Lakini hata kwa upande wa CEO mwenyewe, licha ya kubeba shutuma nzito dhidi ya Manara lakini tunaambiwa kwamba alikuwa amemfikishia Manara ujumbe kwa kupitia meseji ya mkononi tu. Uimara wa taasisi uko wapi hapa? Hakukuwa na umuhimu wa kikao baina yao au mawasiliano ya barua pepe? Inashangaza kidogo.

Tunarudi katika tatizo fulani la msingi ambalo wengine hawawezi kuliona. Sauti ya Manara inadai kwamba CEO amekuwa akimfuatafuata kwa muda mrefu tu. Hapa kulikuwa na kutazamana kwa jicho la pembeni. Kuna sababu ipo nyuma ya pazia.

CEO ni msaidizi wa karibu wa tajiri wa timu. Inadaiwa kwamba wote kwa pamoja hawaridhishwi na kitendo cha Manara kuwa karibu na kufanya biashara na mahasimu wa kibiashara wa tajiri huyo wa Simba. Manara kwa kutumia akaunti yake ya mtandao wa kijamii Instagram amekuwa na mikataba ya kutangaza biashara za mahasimu wa kibiashara wa tajiri wa Simba.

Ukweli ni kwamba Manara ana haki zote za kufanya hivyo, kwa sababu ile ni akaunti yake binafsi na sio ya Simba. Lakini ikumbukwe kwamba Manara ana mkataba na Simba na hana mkataba binafsi na tajiri wa Simba au kampuni zake. Kwanini tajiri ambane?

Mpaka hapo hakuna muingiliano wa kimaslahi (conflicts of interest) mpaka pale ambapo tajiri angeingia mkataba binafsi na Manara. Kilichopaswa ni tajiri kumpa mkataba binafsi Manara nje ya mkataba ule wa Simba. Nadhani hata watu wa juu wa Simba wanatambua hilo na ndio maana Manara ameendelea kushika nafasi hiyo licha ya kuendelea kutangaza bidhaa za kampuni hasimu kwa tajiri.

Kinachochekesha katika sakata hili la utangazaji wa bidhaa ni kitu hiki hapa. Msemaji wa klabu amekuwa maarufu sana kuliko wachezaji wake. Msemaji wa klabu ana wafuasi zaidi ya milioni tatu katika akaunti yake ya Instagram huku katika kundi la wachezaji mchezaji mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram akiwa na wafuasi laki nane tu. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Hii topiki nyingine na ya siku nyingine. Kwanini wachezaji wetu hawawi mastaa?

Baada ya kila kilichotokea kati ya Manara na CEO wake nadhani mabosi wengi wa Simba pamoja na mashabiki walisimama nyuma ya CEO na kumtupa Manara. Wengi walikasirishwa kwa uamuzi wa Manara kujibu mapigo siku chache kabla hawajacheza na mtani.

Alijitokeza kigogo anayeitwa Zacharia Hans Pope kumjibu Haji kwa niaba ya Simba. Alitoa hisia nyingi za moyoni akiwawakilisha watu wa Simba kimya kimya. Ambacho Zacharia alisahau ni kwamba Manara wamemtengeneza wenyewe kuwa kama alivyo.

Mara nyingi Manara alikuwa akiwabwatukia waandishi wa habari, wachambuzi, wachezaji wa watani au wa timu pinzani bila ya staha. Awe ana haki au hapana lakini, lugha yake inakuwa ile ile kama aliyoitumia kwa CEO. Kwanini hawakumdhibiti wakati huo na badala yake wanaamini ameongea maneno makali wakati huu?

Kama alivyowaita wachambuzi ‘takataka’ ndivyo alivyomwambia CEO ‘koma!’. Muosha huoshwa. Simba wangeweza kuja hadharani zaidi ya mara mbili kuomba radhi kwa kitu fulani ambacho Manara ameongea katika mitandaoni au katika mikutano na waandishi wa habari lakini walikuwa hawajitokezi.

Nini kitafuata? Sioni Manara akiwa na maisha tena kama kiongozi wa Simba kwa sasa. Ataondolewa rasmi katika nafasi yake muda wowote kuanzia sasa.

Tatizo ni kwamba Manara anataka kutapika nyongo kuhusu maisha yake Simba na kile anachoamini kuna ujanjaujanja unaendelea katika uwekezaji wa tajiri ndani ya Simba.

Hili jambo linamtesa tajiri. Manara anaweza kuvuruga mambo kwa sababu anajua mambo mengi yanayohusu mchakato na mengine ambayo hayapo sawa.

Ni ukweli unaotesa hasa kwa tajiri na wengineo hasa tukizingatia kwamba wote tunaujua mdomo wa Manara.

Hatua itakayochukuliwa na Simba dhidi Manara na kisha hotuba ya Manara dhidi ya waandishi wa habari itaendeleza ‘Part two’ ya filamu hii nzuri na ya kusisimua. Puto likipulizwa sana huwa linakaribia kupasuka. Sisi ni watazamaji tu.