JICHO LA MWEWE: Edward Manyama wa juzi, jana na keshokutwa

NIWAKUMBUSHE tu kwamba Charles Edward Manyama alicheza Yanga miaka ya karibuni. Sio zamani sana. Kuna watu wasio na kumbukumbu ambao wanajisahaulisha kwamba huyu sio mchezaji mgeni katika soka letu. Ndani ya miaka kumi hii alikuwa mchezaji wa Yanga.

Walimchukua kutoka JKT Ruvu akacheza mechi mbili tatu kabla ya kuonekana kuwa Yanga walifanya makosa kumchukua kutoka alikokuwa na kuvaa jezi ya timu yao. Baadaye wakaachana naye akaendelea na maisha yake.

Baadaye aliibukia Namungo na kuwa mmoja kati ya mabeki wazuri wa pembeni. Napenda staili yake ya kujua kuruka na kufunga mabao ya vichwa. Anajua kuutumia urefu wake vema. Baada ya kuonyesha hili wakubwa wakaanza kutiana vikumbo.

Azam wameinasa saini yake akitokea Ruvu Shooting ambayo alijiunga nayo katikati ya msimu uliopita. Naambiwa kwamba Azam ndio ambao walifanya fitina akaenda zake Ruvu kabla ya kumchukua rasmi hivi majuzi.

Simba walikuwa katika mbio za kumnasa Manyama na tayari walikuwa wamejipanga kutibua dili la Manyama kwenda Azam, lakini naambiwa kwamba Manyama mwenyewe alishaamua asiende katika timu zenye presha akaamua kwenda Azam.

Kwanini Manyama huyu huyu ambaye alikuwa anaonekana hafai leo ni lulu na watu wamemgombea? Kuna mtu au watu wajanja pale Yanga walikiona kitu katika miguu yake. Wakapambana akasaini katika timu yao. Hata hivyo mara nyingi huwa inaishia hapo.

Mara nyingi huwa hatuwalindi wachezaji chipukizi wenye vipaji. Huwa hatusimami upande wao. Kwa hizi timu wanaoapaswa kuwajibika ni mashabiki, viongozi na benchi la ufundi. Inabidi tuwaondolee presha na kuwatia moyo hili wakae vizuri kisaikolojia.

Kipindi ambacho Manyama alikuwa anacheza Yanga hata Simon Msuva alikuwa anacheza Yanga. Mwanzo wa maisha ya Msuva pale Yanga ilikuwa shida tupu. Alikuwa anazomewa na mashabiki na kutukanwa sana pindi alipokuwa anakosea.

Sio wachezaji wote wanaweza kuhimili hili, lakini Msuva aliweka pamba katika masikio yake na baadaye akaibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi kikosini. Baadaye akauzwa kwenda Morocco na leo yupo katika moja kati ya klabu kubwa barani Afrika, Wydad Casablanca.

Hata hivyo sio kila mmoja anaweza kuwa kama Msuva. Wengine wana mioyo laini. Ndio hawa kina Manyama. Anaweza kuzomewa mechi mbili tatu moyo wake ukafa. Akajiona hafai. Kabla ya Yanga alikuwa amejiamini kucheza bila ya presha katika timu yake.

Na unaweza kuona baada ya Yanga pia akarudisha uwezo wake wa kujiamini kwa kucheza kama alivyokuwa anacheza katika timu yake ya awali. Huu ndio ukweli ambao wanakumbana nao vijana wengi wanaoingia kucheza Simba na Yanga bila ya kulindwa.

Mwingine aliyewahi kukumbana na ukweli huu ni Hassan Dilunga. Katika kipindi kile kile cha Manyama, Dilunga alihamia Yanga akaenda kukutana na kina Thabani Kamusoko. Yalikuwa maji mazito kwake. Baadaye akaonekana hafai akaenda zake Mtibwa Sugar akajiamini na kurudi kiwango chake. Leo amerudi tena katika timu kubwa.

Achilia mbali kutowalinda katika kiasi hiki lakini wakati mwingi hatuwaandai kuja kuwa wachezaji wakubwa baada ya wakubwa waliopo kuondoka. Waingereza huwa wanaita natural successor. Unasubiri fulani aishe hili huyu achukue nafasi yake taratibu.

Sisi kila wakati tunataka wachezaji wapya bila ya kuwakomaza vijana taratibu kuja kuchukua nafasi za wakubwa. Mfano ni namna ambavyo Pep Guardiola alimlinda Phil Foden kuja kuwa staa mkubwa siku za usoni.

Foden alijikuta katika rundo la mastaa wakubwa pale Manchester City kina David Silva, Raheem Sterling, Kelvin De Bruyne na wengineo. Lakini Guardiola alikuwa anampa nafasi taratibu Foden aje kuchukua nafasi zao siku za usoni. Leo ni tegemeo. Tanzania anaweza kusajiliwa mchezaji kinda na watu wakataka matokeo hapo hapo. kwa mfano, Yanga waliwahi kumsajili kinda aliyewika na kikosi cha timu y taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Yohana Mkomola na wakataka hapo hapo awafungie mabao. Angewezaje?

Tutofautishe kati ya mchezaji aliyekamilika na mchezaji aliye katika mchakato. Kwa mfano, binafsi naamini kwamba mchezaji kama Charles Ilanfya atakuja kuibuka kuwa tishio na atarudi katika timu kubwa kati ya Azam au Yanga kama Simba wakiamua kuachana naye mwishoni mwa msimu huu. Ni mchezaji aliye katika mchakato wa kuwa mchezaji mkubwa. Lakini pia kwa upande wa wachezaji wenyewe nadhani inabidi wawe na washauri wa kuwaongoza pindi wanaposaini katika klabu hizi. Nadhani wanakosa washauri wazuri katika kuwafanya waone tofauti ya kucheza timu ndogo na timu kubwa.

Kuna wachezaji wengi makinda wakiingia katika timu hizi wanajiona wamemaliza. Hawajui wapo katika mchakato wa kwenda mbele zaidi. wengi wanajiona wamefika na wanabadilisha tabia zao.

Hili la Manyama ni fundisho jingine kwa klabu zetu. Yanga walipoteza mchezaji mahiri kutokana na ukosefu wa umakini wa namna ya kumtunza mchezaji. Huyu sio wa kwanza na hawezi kuwa wa mwisho kama hatutakuwa na maamuzi ya kisoka.

Mchezaji mwingine mzuri ambaye Yanga walimpoteza ni David Luhende wa Kagera Sugar. Ukiangalia mpira ambao Luhende anacheza pale Kagera Sugar huku akiwa mmoja kati ya walinzi wenye pasi nyingi za mabao katika Ligi unajiuliza kwanini Yanga waliachana naye na kwenda kuteseka kwa walinzi wengine wa pembeni ambao hawafikii hata nusu ya uwezo wa Luhende.

Yanga hawa hawa waliwahi kuachana na Amri Kiemba katika njia za ajabu lakini baadaye Kiemba akaibukia kwingine na kucheza soka safi. Hatimaye baadaye alirudi katika timu kubwa wakati alipochukuliwa na Simba. Akiwa na Simba alionyesha kiwango cha juu kiasi cha kutakiwa na klabu moja kubwa ya Morocco.