JICHO LA MWEWE: Bernard Morrison kituo kinachofuata?

RAFIKI yangu mmoja kiongozi Simba wakati ule sakata la Morrison kusaini Simba likiwa limeanza kuchanganya alinipigia simu na kukoroma kweli kweli. “wanamuonea tu. wanamsingizia mambo mengi eti kwamba hana nidhamu. Kwanza hajasaini kule. Wanamuonea tu. wamemzushia mambo mengi tu. kijana ana nidhamu na ana akili sana.”

Nilimkumbuka rafiki yangu Ijumaa mchana baada ya kuitazama barua ya Simba. iliandikwa kifundi kweli kweli. Amepewa ruhusa ya kupumzika mpaka mwishoni mwa msimu, halafu hapo hapo wakamtakia maisha mema katika maisha yake ya soka kwingineko.

Kwamba bungo lililomshinda nyani yule na nyani huyu pia limemshinda. Nilimkumbuka sana rafiki yangu. Hapo mitaa ya kati ya waliwahi kumsimamisha sikusema kitu. lakini sasa kifupi wameamua kuchana naye kabisa.

Nazijua klabu zetu. Mchezaji kama yeye, mwenye kipaji kama yeye, alikuwa anahitajika sana katika mbio za kuwafukuza Yanga mpaka mwishoni mwa msimu. Mchezaji kama yeye apewe ruhusa sasa hivi wakati ilikuwa wazi kwamba Simba ingeifunga Pamba na kucheza na Yanga siku chache zijazo. Anapewaje ruhusa?

Nadhani lugha iliyotumika ilikuwa ni ya kuficha aibu zaidi. wamejaribu kumfichia aibu zake nyingi kwa ajili ya kuendelea kuwasimanga watani zao kwamba wamepoteza mchezaji mzuri. Hata hivyo ukweli wa mambo Ben aliendelea kuwa yule yule tu.

Na sasa wamechoka. Wameagana naye huku Simba wakiwa wamebakiza mechi saba za Ligi. Kuna hisia zinaendelea ndani ya Simba. kwamba Morrison amerudisha mahusiano mazuri na waajiri wake wa zamani. Kwamba pia haitumikii timu kwa moyo wote. Kwamba hata pambano la watani lililopita alikuwa anaisaka kadi nyekundu.

Lakini zaidi ni kwamba kuna hisia Morrison amerudi kwa waajiri wake wa zamani au yupo njiani kurudi kwa waajiri wake wa zamani. Matokeo yake amekuwa mchezaji asiyeaminika zaidi pale Msimbazi. Walikuwa wanaishi naye kwa mashaka kwa muda mrefu.

Kutokana na kuishi huku kwa mashaka kulikuwa na makundi mawili. Kundi la kwanza lilikuwa halitaki Morrison apewe mkataba mpya. kundi la pili lilitaka apewe mkataba mpya. Hii ndio habari ya mwisho niliyokuwa nayo achilia mbali zile za uvumi kwamba amerudi kwa waliomleta. Hatimaye inaonekana kundi la kwanza limeshinda. Wameachana na kipaji maridadi ambacho kimekuwa na makandokando mengi. Kwanza nje ya uwanja kulikuwa na tatizo hili la nidhamu ambalo lilionekana kushamiri kila siku.

Majuzi tu alikuwa katika kituo cha polisi cha Chang’ombe akishutumiwa kumchoma shabiki mmoja wa soka na kitu chenye ncha kali. Sijui kesi yenyewe imeisha vipi. Sijui pia hata kwanini aliondoka uwanjani peke yake baada ya mechi.

Lakini ndani ya uwanja Simba nadhani wamefikia maamuzi haya kutokana na kutopata walichokitarajia kutokwa kwake. Katika siku yake hakuna mchezaji kama Morrison nchini. Uwezo wake wa kukokota mpira, kulisaka lango hauna mpinzani.

Hata hivyo kwa miezi 24 iliyopita Morrison amekuwa na siku chache kama hizi. Hesabu kwa vidole ni mechi ngapi ambazo Morrison amefanya mambo makubwa sana uwanjani akiwa na jezi nyekundu ya Simba. Sio mechi nyingi.

Uzuri wake ni kwamba katika ubora wake lazima Morrison atakuchanganya akili. Na ndio maana alilazimisha yawepo makundi mawili yaliyogawanyika kuhusu mustakabali wake Simba. utamkumbuka Morrison kwa jinsi ambavyo utajisikia lakini mwisho wa siku lazima ukumbuke kwake ana kipaji kikubwa.

Kituo kinachofuata? Sijui wapi. Hata hivyo anaonekana kufurahia maisha ya Tanzania. Yeye na Tanzania wamefunga ndoa. Kwa sasa anaongea vema lugha ya Kiswahili kuonyesha kwamba anaipenda Tanzania.

Hata hivyo kwa tabia zake nadhani sio bahati mbaya kwa yeye kuwa hapa hata kama ana kipaji kikubwa. Ni Tanzania tu ndipo mastaa wanapoishi bila ya nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja lakini tunawashangilia.

Niliwahi kusema mahala. Kuna sababu lukuki za mastaa wenye vipaji vikubwa wa nje kuja hapa. Wengi wao wana tatizo la umri, wengine wana tatizo la nidhamu kubwa ya nje ya uwanja. Tanzania ni mahali salama. Fikiria, kuna mchezaji staa wa timu kubwa majuzi aliingia katika matatizo ya nidhamu na kocha wake lakini tukaambiwa kuwa ni majeruhi. Nani hapendi kuishi katika maisha haya.

Nadhani Morrison atabakia nchini. Wapi? sijui. Lakini kuna mambo mawili hapa. Kama kweli ameshasaini mahala basi ni habari njema kwake. Kama bado hajasaini basi atapata wakati mgumu kupata dau kubwa kwa sababu hayupo katika nafasi nzuri ya kudai dau kubwa. Ili mchezaji apate dau kubwa inabidi agombaniwe na hawa wakubwa. Ni kama ilivyotokea wakati akitoka zake Yanga kwenda Simba. Lakini kwa sasa Simba wamefanya kazi nzuri ya kuharibu dau la anakokwenda. Ni akili nzuri ambayo Simba wameitumia.

Katika yote haya pia nimemkumbuka marehemu Zacharia Hans Poppe. Nimemkumbuka sana. Suala la Morrison kwenda Simba alijimilikisha yeye mwenyewe. Akalibeba. Akamuhamisha hata katika nyumba aliyokuwa anakaa na kumpeleka sehemu nyingine.

Wazungu wangeweza kutupa usemi wao kwamba kwa sasa marehemu Hans Poppe anatikisika kwa hasira klabuni. Kama Mungu angempa pumzi mpaka nyakati hizi naamini angekuwa mmoja kati ya watu ambao wangeamuru Morrison aache. Hans Poppe alikuwa hapendi ujinga.

Tusubiri na kuona ambako Morrison atakwenda. Hata hivyo nabashiri tu kwamba kokote ambako atakwenda huu utakuwa uhamisho wake wa mwisho nchini. Nadhani anaweza kutulia kidogo kwa sasa akacheza soka. Anajua kwamba hawezi kurudi Simba.

Wakati akiwa Simba nadhani alikuwa ameweka akiba ya kipande cha moyo kwamba anaweza kurudi Yanga. Anajua kwamba watu wa Yanga walikuwa wanamtamani. Walikuwa wanamtamani kutokana na kipaji chake lakini pia walikuwa wanamtamani pia kwa ajili ya kuwakomoa watani. Ndio maisha yetu.

Hata hivyo Simba hawawezi kumtamani tena Morrison. Naomba kukumbushwa mchezaji ambaye aliichezea Simba mara mbili na Yanga mara mbili. Sina kumbukumbu sahihi. Morrison itabidi atulize kichwa huku akijua kwamba huenda huu ukawa uhamisho wake wa mwisho.