Inawezekana Simba na Yanga kutamba pamoja barani Afrika

Wednesday April 07 2021
simba, yanga pc
By Edo Kumwembe

WAKATI mwingine maisha yanashangaza sana. Jinsi soka la Afrika ambavyo limeanza kubadilika kwa kasi. Unajiuliza swali moja. Simba wanakwenda juu au wakubwa wengine wanakwenda chini? Nadhani majibu yote ni sahihi.

Simba wamewekeza katika kikosi chao. Wanafanya vema kwa sasa. Wakubwa wengine akina TP Mazembe na Vita na wengineo wanakwenda chini kwa kasi. Hauwezi kulinganisha makali yao na kikosi kama cha Simba kwa sasa.

Kuna watu hapa nchini hawataki kukubaliana na ukweli huu. Watani wa Simba Yanga itawachukua muda mrefu kukubaliana na ukweli huu kwamba Simba ipo juu kwa sasa. Kuna ambao wanasubiri Simba ipate matokeo mabovu.

Kuna mashabiki walingoja Simba itolewe katika hatua za mwanzo walipocheza na Platinum kisha Plateau United. Simba wakapita. Kuna watu wakasubiri Simba itolewe katika hatua ya makundi, bado wakatoboa. Wameongoza kundi.

Na sasa kuna mashabiki wa watani zao wanasubiri Simba ichapwe katika mechi zake mbili za robo fainali dhidi ya mpinzani yoyote mkali ambaye atakumbana naye. Hatuwezi kujua atapangwa na nani na hatuwezi kujua kama adui ajaye anaweza kufanikiwa kumuuza mnyama.

Kuna uwezekano mkubwa wakaenda mbali zaidi mpaka hatua ambazo watakutana na Mamelodi Sundowns au Waydad Casablanca. Hatujui lini. Lolote linaweza kutokea. Kuna wengine wameanza kuota ndoto za Simba kuwa bingwa wa Afrika.

Advertisement

Vyovyote ilivyo nadhani watani zao Yanga wasisubiri Simba ishuke chini. Kinachopaswa kwa sasa ni Yanga kushika hatamu na kusuka kikosi kikali ambacho kitaifuata Simba ilipo. Imeanza kuonekana kama dhana kwamba Simba na Yanga haziwezi kutamba pamoja. Sio kweli.

Kwa wakati mmoja, Yanga na Simba kwa pamoja zina uwezo mkubwa wa kipesa. Kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kile ambacho huwa kinatokea Misri, Congo, Morocco na kwingineko. Wababe wawili utawala soka la Afrika kwa wakati mmoja.

Pale Misri kuna wakati Zamalek na Al Ahly walikuwa wanatawala soka la Afrika kwa pamoja. Wote wawili wanaweza kutesa katika michuano ya Klabu bingwa ya Afrika au mmoja akatesa katika kombe la Shirikisho. Mara nyingi walikuwa wanacheza wote katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa sababu Misri wanaingiza timu nyingi zaidi.

Watazame Wamorocco. Ni mara ngapi Waydad Casablanca na Raja Casablanca walitesa kwa pamoja katika michuano ya Afrika? kama wote hawatesi katika michuano ya aina moja basi mwingine anatesa katika michuano mingine.

Pale Congo kuna wakati TP Mazembe walikuwa wanatesa upande mmoja na Vita walikuwa wanatesa upande mwingine. Wote walikuwa na vikosi vikali. Usingetamani kukutana na yoyote kati yao. Usingependa kwenda Lubumbashi wala Kinshasa.

Kuna dhana ya kijinga hapa nchini. Kwamba kama Yanga akiwa juu basi haiwezekani Simba apande juu mpaka Yanga ashuke chini. Hivyo hivyo kama ilivyo sasa. Inaonekana kama vile kama Yanga haitafanikiwa kwenda juu mpaka Simba ishuke chini.

Sioni ulazima huu. Kama Simba wakifanikiwa kuipatia Yanga nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika basi ni suala la Yanga kutengeneza timu kali na kuhakikisha inashindana vema katika michuano hii kama Simba inapofanya kwa sasa.

Walichoonyesha Simba ni mfano mzuri katika uwezekaji wa kikosi uwanjani. Na hili ni jambo linalowezekana kama GSM wataamua kujikita ipasavyo katika kuhudumia timu ya uwanjani na kupata sapoti kwa mashabiki.

Tatizo kubwa la mashabiki wa Yanga ni kudhani kwamba timu yao haipigi hatua kwa sababu muda mwingi wanautumia kujilinganisha na Simba. ukweli ni kwamba Simba wamepitia mchakato mrefu wa ndani na nje ya uwanja kufika walipofika.

Simba imepitia kwa akina Shizza Kichuya na mpaka leo imeangukia kwa akina Clatious Chotta Chama kuweza kufika ilipofika. Yanga wanatamani timu yao iwe bora ndani ya usiku mmoja tu.

Kitu kingine kinachoweza kuwapa nguvu watu wa Yanga ni ukweli kwamba huu ndio muda mwafaka wa kupanda juu wakati baadhi ya timu za Afrika zikiwa zinaanguka. Kumbe inawezekana tu kama kuna uwezekaji wa maana katika timu.

Simba ametumia faida hizi mbili kwa wakati mmoja. Amewekeza kwa wachezaji wazuri lakini hapo hapo akapata faida ya timu kama TP Mazembe kuzeeka na kushindwa kurudia katika makali yao. Hata hawa Vita wa juzi sio wale ambao alicheza nao miaka miwili nyuma. Wameshuka.

Moja kati ya ndoto zangu ni kuona Simba na Yanga zikicheza pambano kali la michuano ya Afrika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. ishawahi kutokea hivyo kwa Zamalek dhidi ya Al Ahly, imewahi kutokea hivyo kwa Raja dhidi ya Waydad na imewahi kutokea hivyo kwa TP Mazembe dhidi ya Vita.

Tatizo letu kubwa Watanzania ni akili za maskini. Wakati mwingine tunaamini watu matajiri wamekuwa hivyo kwa sababu yetu. Tunaamini katika kushuka kwao kuliko kuwafikia walipofika. Kufanikiwa kwa Yanga sio kushuka kwa Simba. kufanikiwa kwa Simba sio kushuka kwa Yanga.

Naamini mafanikio makubwa ya Simba yatakuwa yamejenga wivu wa Yanga kuifikia Simba ilipo pengine kuliko kutumia nguvu nyingi kuizomea isifike mbali. Ni utani wa kawaida kwa Simba na Yanga kutoombeana mema lakini isifike mahali furaha ya kufungwa kwa mtani ikawa kubwa kuliko mafanikio yako mwenyewe.

Kila la kheri kwa Yanga katika mapambano yao ya kuijenga timu yao. Mwaka 1993 Yanga walichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na kati pale Uganda na Simba walikuwa wakifika fainali za kombe la CAF dhidi ya Stella. Ni kitu kinachowezekana.

Advertisement