HUKO CHAMPIONSHIP: Mastaa hawa watanogesha kinoma

UNAAMBIWA hakuna kijiji bila wazee, lakini ukija kwenye soka wajuzi wanakuambia hakuna ligi inayonoga bila kuwa na mastaa.

Huo ndio ukweli katika dunia ya sasa ya soka ndio maana nchi kama China na mataifa mengine ya Uarabuni miaka ya karibuni wamevunja benki ili kusaini mastaa wakubwa duniani kuzifanya ligi zao kufuatiliwa na wengi, kukua na kuwa bora.

Achana na hilo, Jumamosi Septemba 17, 2022 Ligi ya Championship (zamani Daraja la Kwanza) ilianza katika viwanja tofauti na ndani yake kuna mastaa kibao waliowahi kutisha kwenye ramani ya soka la Bongo wamesajiliwa na timu hizo na watakiwasha msimu huu.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mastaa wa Championship ambao wameanza kukiwasha mapema tu.


EDWARD SONGO (JKT TANZANIA)

Nyota huyo aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia JKT Tanzania hivi karibuni ataendelea kutegemewa tena kutokana na uhodari wa kuzifumania nyavu kwani msimu uliopita aliibuka kinara wa kufunga mabao 16 na kuchaguliwa mchezaji bora wa Championship.


DANNY MRWANDA (FOUNTAIN GATE)

Mrwanda amejiunga na timu hiyo akitokea KenGold ambapo msimu uliopita alihusika kwenye mabao 20 akifunga 13 na kuchangia saba (Assisti) katika mechi 24 alizocheza kati ya 30.

Nyota huyo amewika na timu mbalimbali za Simba, Yanga, Al- Tadhamon (Kuwait), Da Nang (Vietnam) na Mbeya Kwanza huku pia akihudumu timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa miaka tisa huku akibeba matumaini ya klabu hiyo inayopambana kupanda Ligi Kuu Bara.


JAMAL MWAMBELEKO (PAMBA)

Beki huyo wa kushoto naye ni miongoni mwa mastaa wanaotarajiwa kuibeba timu yake ili kuhakikisha inapanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao kutokana na uzoefu alionao kwani amewahi kucheza timu mbalimbali za Simba, Mbao, KCB ya Kenya na African Sports ya Tanga.


ABDULHALIM HUMOUD (FOUNTAN GATE)

Unapotaja miongoni mwa mastaa waliozunguka timu nyingi ndani na nje ya nchi hutaacha kulitaja jina la Humoud aliyejiunga na Fountain Gate msimu huu akitokea Mbeya Kwanza ambayo nayo inashiriki ligi hiyo baada ya kushuka kwa msimu uliopita. Miongoni mwa timu alizochezea ni, Simba, Azam FC, Coastal Union, Mtibwa Sugar, Sofapaka (Kenya), Namungo FC, Majimaji na Tshakhuma Tsha Madzivhandila ya (Afrika Kusini).


PETER MAPUNDA (PAMBA)

Mapunda amejiunga na timu hiyo akitokea Mbeya City baada ya mkataba wake kuisha huku akiwahi kuzichezea klabu mbalimbali za Majimaji na Dodoma Jiji huku uongozi wa Klabu hiyo ukiamini uzoefu alionao utakuwa ni chachu ya kutimiza malengo yao.


MAKA EDWARD (JKT TANZANIA)

Nyota huyo uzoefu wake unaweza kutimiza malengo ya kuirejesha timu hiyo ligi kuu kwani amewahi kuzichezea Geita Gold na Moghreb Tetouan ya Morocco.


KIGI MAKASI (KEN GOLD)

Makasi aliyewika na Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Ndanda anaendelea kusalia tena na kikosi hicho kwa msimu wake wa pili mfululizo kutokana na uzoefu wake.

HASSAN KAPALATA (JKT TANZANIA)

Baada ya mkataba wake kuisha na KMC alijiunga na JKT Tanzania ikiwa ni pendekezo la Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Malale Hamsini kwa lengo la kutengeneza timu imara itakayopambana ili kurejea ligi kuu kufuatia msimu uliopita kufeli hatua ya mchujo.


MOHAMMED RASHID (PAMBA)

Mshambuliaji huyo aliyewahi kutamba na Simba, Tanzania Prisons na JKT Tanzania anatazamiwa kuibeba timu yake kutokana na uzoefu wake.


OWEN CHAIMA (FOUNTAIN GATE)

Raia huyu wa Malawi amejiunga na timu hii baada ya kuiwezesha DTB sasa (Singida Big Stars) kupanda Ligi Kuu Bara msimu huu.

Chaima aliyewahi kutamba na Big Bullets ya kwao ni mchezaji wa kwanza wa Malawi kuichezea Fountain Gate huku uzoefu wake ukitajwa ndio sababu ya kusajiliwa.



MARCEL KAHEZA (PAMBA)

Huyu ni nyota mwingine ambaye anatazamwa kuibeba Pamba katika harakati za kuirejesha Ligi Kuu Bara kwa sababu ya uzoefu wake kwani amewahi kutamba na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi zikiwemo Simba, Polisi Tanzania, AFC Leopards (Kenya) na Majimaji.


PASTORY ATHANAS (FOUNTAIN GATE)

Msimu huu amejiunga na kikosi hicho akitokea Mbeya City huku uzoefu wake kwenye eneo la ushambuliaji ukitegemewa kuleta chachu na ushindani mkali kutokana na kupita timu mbalimbali kama Simba, Mbao, Singida United, Gwambina na Toto African.


ANDREW CHAMUNGU (MBUNI)

Nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichoipandisha Polisi Tanzania Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 ingawa ushindani wa nafasi ulimfanya kushindwa kuwika na kujikuta akitolewa kwa mkopo timu mbalimbali ikiwemo Kitayosce aliyokuwa msimu uliopita.

Akiwa na Kitayosce alifunga mabao saba na baada ya msimu kuisha aliwekewa donge nono na kuamua kutimkia Mbuni ya jijini Arusha.


RIPHAT MSUYA (JKT TANZANIA)

Msuya amejiunga na Maafande hao msimu huu baada ya mkataba wake na ‘Wakata Miwa’ Mtibwa Sugar kuisha huku akiwahi pia kutamba na Ndanda.


MSIKIE BUDEBA

Kocha Mkuu wa Mbuni FC, Leonard Budeba anasema wingi wa wachezaji wakubwa na wazoefu kwenye ligi hiyo ndio ambao umeleta ushindani mkubwa katika mashindano.

“Kwa misimu ya hivi karibuni tumeona timu zote zilizopanda Ligi Kuu Bara zilisheheni wachezaji wazoefu hii ni ishara tosha ya kuona ni jinsi gani wameongeza ushindani kwa kila klabu kusajili kwa sababu zina uwezo wa kukidhi mahitaji yao muhimu,” alisema Budeba.