HIZI LEVO MAJI YA SHINGO

Muktasari:

LIGI Kuu Bara inaelekea ukingoni huku timu nyingi zikiwa zimebakiza mechi nne tu kabla ya kumaliza msimu isipokuwa Simba iliyobakisha mechi saba.

LIGI Kuu Bara inaelekea ukingoni huku timu nyingi zikiwa zimebakiza mechi nne tu kabla ya kumaliza msimu isipokuwa Simba iliyobakisha mechi saba.

Yanga, Coastal na KMC zimebakiza michezo mitano kila mmoja huku vita kubwa katika ligi hiyo kwa sasa ikiwa ni kwa timu zilizo mkiani ambazo zinapambana kujinasua na janga la kushuka daraja.

Wakati Ligi ikielekea ukingoni kuna jambo la kushangaza baada ya wachezaji wengi waliokuwa katika nafasi 10 za juu za ufungaji bora msimu uliopita mpaka sasa kuonekana kupata wakati mgumu wa kufikia rekodi zao msimu huu.

Hadi sasa Prince Dube wa Azam ndio anaongoza chati ya ufungaji bora akiwa amefunga mabao 14 akifuatiwa na John Bocco wa Simba aliyefunga 13 wakati Meddie Kagere ana mabao 11, Chris Mugalu akifunga mabao 10 wote hao kutoka Simba.

Hizi ni levo ambazo hawa jamaa waliziweka wenyewe msimu uliopita lakini msimu huu zinaonekana ni maji ya shingo kwao wenyewe kuzifikia.


Kagere -

Simba

Meddie Kagere msimu uliopita ndiye aliibuka kinara wa ufungaji baada ya kutupia mabao 22 tuzo aliyochukua mara mbili mfululizo baada ya msimu wa 2018/19 kufunga mabao 23.

Msimu huu mambo yameonekana kwenda kombo kwake kwani hadi sasa amefunga mabao 11 na amekuwa hapati nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza jambo ambalo linamuathiri katika kutimiza ndoto yake ya kutwaa tena kiatu cha dhahabu kwa mara ya tatu.

Kocha wa Simba, Didier Gomes amekuwa akimtumia zaidi Mugalu na Bocco.

Kama atapata nafasi ya kucheza mechi zilizobaki labda anaweza kufanya maajabu ingawa ni ngumu kwake kufikia mabao ya msimu uliopita.

Mhilu - Kagera Sugar

Mpaka sasa Yusuf Mhilu amefunga mabao tisa akibakisha mabao manne ili kuifikia rekodi yake ya msimu uliopita alipomaliza ligi akiwa amefunga mabao 13.

Hata hivyo, inabidi afanye kazi kwani timu yake imebakiwa na mechi tatu tena dhidi ya Ihefu, Polisi Tanzania na Coastal Union huku wakiwa katika presha kubwa ya kujinasua na janga la kushuka daraja.

Kama Mhilu akikomaa mechi hizo anaweza akafikisha mabao ya msimu uliopita ingawa si kazi rahisi.


Reliants Lusajo - Namungo

Alimaliza na mabao 12 msimu uliopita lakini mpaka sasa msimu huu hata nusu yake hajafika akiwa tayari amepachika wavuni mabao matano.

Alianza msimu akiwa na timu ya KMC kabla ya kuona mambo magumu kwake ndani ya timu hiyo na kurejea timu yake ya zamani ya Namungo anayoichezea hadi sasa.

Namungo imebakiwa na michezo mitatu kabla ya msimu kumalizika dhidi ya Simba, Azam na Ruvu Shooting hivyo Lusajo anatakiwa kupambana ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita na kuivunja.


Obrey Chirwa - Azam

Hadi sasa Mzambia huyu ameifungia timu yake mabao matano tu na kudaiwa mabao saba ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita alipofunga mabao 12.

Alianza vizuri ligi akicheza sambamba na Dube lakini majeraha yakampunguza kasi na hata sasa licha ya kurejea uwanjani amekuwa hapati nafasi ya kuanza kutokana na kasi ya Dube, Iddi Nado na Ayoub Lyanga ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara.


Peter Mapunda - Dodoma Jiji

Anafahamika kama mtaalamu wa mpira ya friikiki lakini msimu huu unaweza kuwa msimu mbaya zaidi kwake kwani hadi sasa amepachika wavuni bao moja tu.

Msimu uliopita alimaliza na mabao 12 hivyo Dodoma Jiji ambayo ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kuamua kumsajili lakini amekuwa hapati nafasi ya kucheza mechi nyingi, ni kwamba hawezi kufikia hata nusu ya mabao aliyofunga msimu uliopita.


Wazir Junior - Yanga

Baada ya kumaliza ligi akiwa amefunga mabao 12 msimu uliopita, Yanga ilitupa ndoano na kumsajili ili kukio-ngezea nguvu kikosi hicho msimu huu.

Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti kwani hadi sasa ameifungia timu hiyo bao moja tu wakati huu ligi ikielekea ukingoni huku akiwa hana nafasi kabisa ya kuanza kikosi cha kwanza.

Hapana shaka mwisho wa msimu ataonyeshwa mlango wa kutokea na hana nafasi ya kufikisha hata theluthi ya mabao yake ya msimu uliopita hivyo watoto wa mjini wanasema imeisha hiyoo.


Paul Nonga - Gwambina

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Yanga na Lipuli hadi sasa ameifungia Gwambina mabao matano, mabao sita pungufu ya msimu uliopita alipomaliza ligi na mabao 11.

Anaweza kuafanya maajabu katika mechi nne zilizobaki ili kufikia rekodi yake ingawa si kazi ndogo hivyo anatakiwa kupambana.


Daruwesh Saliboko -Polisi TZ

Amefunga mabao manne katika timu yake mpya iliyomsajili baada ya kufanya vizuri msimu uliopita akiwa na Lipuli ya Iringa iliyoshuka daraja.

Mshambuliaji huyu alimaliza ligi msimu uliopita akiwa amefunga mabao 11 wakati huo akiwa Lipuli lakini msimu huu mambo yamekuwa magumu kwake kwani hata nusu ya mabao hayo hajafikisha.


Bigirimana Blaise -Namungo

Straika huyu raia wa Burundi hadi sasa amefunga mabao manne tu na hataweza tena kurejea uwanjani kwa sasa hadi msimu ujao kutokana na majeraha ya goti yanayomsumbua.

Bigirimana alimaliza msimu uliopita akiwa amefunga mabao tisa na kama si majeraha basi msimu huu huenda angefikia rekodi hiyo.

Mchezaji huyo yuko nje ya uwanja tangu Januari mwaka huu alipoumia mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba uliofanyika Januari 11, Zanzibar.

Bigirimana anasema “Sitoweza kucheza tena labda mpaka Julai, inaumiza kukosa ligi kwa muda mrefu lakini wakati mwingine niseme ni bahati mbaya hivyo namshukuru Mungu kwa yote na naamini atanisaidia msimu ujao nitarejea nikiwa vizuri.”


Ayoub Lyanga -Azam

Msimu uliopita aliichezea Coastal Union na kumaliza ligi akiwa amefunga mabao tisa hivyo Azam kuvutiwa naye na kuamua kumsajili msimu huu. Hadi sasa ana mabao sita. Mechi nne zimebaki akikomaa atafikia.