HISIA ZANGU: Yanga wana mlima, Simba inahitaji kusafisha haswa

GHAFLA tu Yanga imejipeleka katika maji marefu. Yanga wamefika katika fainali ya kombe la Shirikisho na hii ina maana kwamba msimu ujao lengo lao kubwa linakuwa kutwaa ubingwa. Ubingwa upi? Ndio swali la kwanza la msimu. Msimu ujao watakuwa katika michuano ya Ligi ya mabingwa.

Kwa namna ambavyo wanajisikia kwa sasa siamini kwamba mabosi wa Yanga watawaambia mashabiki wao kuwa  lengo kubwa ni kufika robo fainali au nusu fainali. Nasubiri kwa hamu kusikia lengo lao la msimu ujao. Nasubiri kwa hamu kusikia mashabiki wao watapokeaje lengo lao.

Halafu kuna watani wao sasa. Simba. Simba wameumizwa kukaa katika makochi na kuishuhudia Yanga ikicheza fainali za Shirikisho. Wao walikuwepo misimu michache iliyopita lakini hawakufikia hatua hii. Kuwatazama Yanga wakishinda ugenini mbele ya CAF, Patrice Motsepe haikuleta picha inayopendeza kwao.

Kuwatazama wachezaji wa Yanga wakivalishwa medali na  Patrice Motsepe huku Afrika na dunia ikishuhudia sio jambo la kupendeza katika mboni za macho yao. Sawa Yanga haikuchukua ubingwa lakini jukwaa walilosimama kushindana lilikuwa kubwa. Ilikuwa ni heshima kubwa kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa Simba kuna watu wanafahamu kuwa hauwezi kujifariji kwa kushangilia Yanga kukosa kombe huku wewe mwenyewe ukiwa haufanyi jambo lolote. Miaka michache iliyopita Simba walikuwa imara zaidi kimataifa na Yanga kazi yao ilikuwa kupokea wageni wa Simba au kushangilia Simba anapopoteza mechi za kimataifa.

Walipoingia GSM hawakutaka maisha yao yaendelee kuwa hivyo. Wamepambana vya kutosha mpaka kufikia hatua ya kujiheshimisha kucheza hatua ya fainali kombe la Shirikisho. Mashabiki wa Simba hawatataka kusikia lugha yoyote zaidi ya kufika fainali katika michuano watakayoshiriki msimu ujao.

Hatua yoyote watakayofikia isiwe fainali itaonekana hawakuwa na msimu mzuri katika michuano ya kimataifa. Ya ga ameshaweka kipimo kwao. Lakini hata Yanga wenyewe wanalazimika kutumia kipimo hiki hiki msimu ujao katika michuano ya kimataifa.

Kesi yangu ya msingi hapa ni kwamba wote wanaweza kujikuta kule kwa akina Wydad Casablanca, Al Ahly, Mamelodi, Raja na wakubwa wengine wa Afrika. Wapo tayari kwa vita? Wapo tayari kujiwekea lengo la fainali hata kama njia yenyewe itakuwa ya wakubwa kule katika Ligi ya mabingwa? Kuna kazi kubwa ya kufanya.

Yanga wana kazi mbili au tatu kubwa. Kwanza ni kumbakisha kocha wao, Nasireddine Nabi. Wasifu aliojitengenezea katika michuano hii unamuweka Nabi sokoni. Moja kwa moja anakuwa miongoni mwa makocha bora wa ndani katika soka la Afrika hata kama hafikii hadhi za akina Pitso Mosimane. Huu ndio ukweli.

Zaidi ni kwamba Nabi amepata uzoefu mkubwa katika michuano hii lakini amekijua vema kikosi chake. Ukimpoteza Nabi msimu ujao utakuwa unajirudisha hatua kadhaa nyuma. Ghafla unaweza kujikuta unapata kocha ambaye atahitaji muda kukijua kikosi chake.

Baada ya hapo Yanga wanahitaji kumbakisha Fiston Mayele. Hii itakuwa kazi ngumu. Afrika haina washambuliaji wengi wa aina yake kwa sasa. Mshambuliaji ambaye amekuhakikishia mabao saba katika michuano ya Shirikisho lazima atajikuta yupo sokoni akiwindwa. Kama wanataka kujiwekea lengo la kufika fainali yoyote msimu ujao lazima uwe na Mayele.

Baada ya kufanikisha haya mawili ndio unaweza kuanza kazi ya kusajili wachezaji wengine wapya ambao watakuja kukiimarisha kikosi na sio kuongeza idadi. Kama unampata winga aliye hatari zaidi ya Tuisila Kisinda na Bernard Morrison linakuwa jambo bora zaidi. Kuna mapungufu katika maeneo hayo.

Kwa Simba ndio kuna kazi zaidi. Wamefika hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa, wamefika nusu fainali michuano ya FA, wameshika nafasi ya pili katika msimu. Haukuwa msimu mbaya sana lakini wametumia idadi ndogo ya wachezaji kutimiza haya. Narudia, kuna pengo kubwa kati ya wachezaji wanaoanza na wasioanza pale Msimbazi. Pengo ni kubwa.

Wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza Simba wana uhakika wa kuanza mechi ijayo. Ni tofauti na Yanga ambao wanapishana mara kwa mara kwa sababu wengi bora. Haishangazi kuona wamefika hadi mwisho salama katika michuano mbalimbali ambayo wameshiriki msimu huu. Wamefika fainali mbili na wametwaa ubingwa wa Ligi.

Na sasa Simba wana nafasi ya kurekebisha makosa ambayo waliyafanya katika madirisha matatu yaliyopita ya uhamisho wa wachezaji. Wameanza kwa kumsafisha Augustine Okrah. Aliingia katika timu kwa mikwara kama vile alikuwa anaenda kuwa mrithi wa Louis Miquissone lakini mwishowe hakuwa na mchango wowote mkubwa klabuni zaidi ya kuwa mtovu wa nidhamu.

Kuna wachezaji wengi wa kusafisha pale Msimbazi lakini kitu cha msingi ni kuwaleta wachezaji wengine wenye ubora zaidi ya wale wanaoondoka. Inabidi waletwe wachezaji wenye ubora mkubwa ambao watapunguza umuhimu wa akina Clatous Chama katika kikosi.

Nimetazama mechi mbili za Simba na Wydad Casablanca nimejiridhisha kwamba Simba wangeweza kuwatoa Wydad kirahisi tu kama wangekuwa na ile timu ya Miquissone. Tatizo wameshuka chini kuanzia pale. Walipoteza nafasi nyingi Uwanja wa Mkapa halafu wakafungwa bao rahisi walipokwenda Casablanca.

Wanahitaji kuleta watu wa maana. Hawahitaji kubahatisha. Vinginevyo lengo lolote la kufika fainali litakuwa uongo kwa mashabiki. Kuna wachezaji ambao umri umesogea na wanaishi klabuni kwa ajili ya majina ambayo walitengeneza siku za awali. Hawa nao inabidi waondoke.

Kuna wachezaji ambao ni vijana lakini hawaisadii Simba kama ilivyokuwa inafikiriwa. Hawa ndio rafiki zangu akina Peter Banda. Hawajawahi kuziba pengo lililoachwa na akina Miquissone mpaka kufikia hatua ya Kibu Dennis kuwa mchezaji muhimu kikosini kuliko wao.

Vyovyote ilivyo Yanga imejivuta katika maji marefu kwa kujipeleka fainali, lakini na watani wao pia wamejikuta katika maji marefu kwa sababu lazima kwanza wafikie hatua ya fainali ndipo ambapo wataweza kueleweka. Huu ni uzuri wa utani wa jadi wa Simba na Yanga. Wanasukumana katika mafanikio.

Bahati nzuri zaidi ni kwamba sasa hivi upinzani wao umehamishiwa zaidi katika mechi za kimataifa. Ni jambo zuri. Tusubiri msimu ujao lakini hakuna ambacho tutawasikiliza zaidi ya kufika fainali.