HISIA ZANGU: Phiri alivyotuondolea kelele za malalamiko kwa Matola

JINSI maisha yanavyokwenda kasi. Ghafla jina la Suleiman Matola limeondoka katika midomo ya mashabiki wa Simba. Wiki chache zilizopita walikuwa wanaimba aondoke. Sasa hivi wamekaa kimya. Hii ndio tofauti ya Wazungu na sisi.

Wazungu hawana unafiki. Kwa mfano kuna kundi kubwa la mashabiki wa Manchester United hawamtaki mmiliki wao ambaye ni familia ya Glazier. Washinde, wafungwe, watoke sare msimamo wao ni ule ule. Hawana unafiki. Kila siku wanakwenda na mabango yao ‘Glazier out’ hata kama wiki iliyopita wametoka kushinda.

Mashabiki wetu wale wafuata mkumbo pale Msimbazi sasa hivi wapo kimya. Siku ile jioni walimzomea Matola baada ya pambano dhidi ya KMC kumalizika kwa sare. Asubuhi Matola alikuwa katika ndege akiwa na kikosi cha Simba akielekea Malawi kucheza na Bata Nyassa Bullets.

Mambo mawili makubwa yalifanyika. Kwanza kabisa viongozi wa Simba hawakusikiliza kelele za mashabiki. Ni dalili za uongozi imara. Hauwezi kupelekeshwa na kelele za mashabiki. Lakini pia Matola mwenyewe aliziba masikio.

Kama Simba wangemzuia Matola kwenda Malawi wangekuwa wamefanya jambo la ajabu na si ajabu wangeivuruga timu. Inawezekana kuna kundi kubwa la wachezaji ambao wana imani kubwa na Matola na ni mshkaji wao.

Nini kilitokea? Simba walicheza vizuri na kushinda mabao mawili ugenini dhidi ya Nyasa Big Bullets. Bao moja la Moses Phiri lilikuwa maridadi hasa. Mashabiki wakasahau kuongea kuhusu Matola wakatumia wiki nzima kulijadili bao la Phiri.

Mechi iliyofuata Simba ikashinda tena. Phiri akafunga tena bao maridadi. Wakaenda zao Zanzibar kucheza mechi za kirafiki wakashinda. Habari ikawa ni Mzungu Dejan Georgijevic aliyetangaza kuondoka klabuni na sio Matola tena.

Juzi katika Uwanja wa Mkapa Mnyama ameunguruma tena. Kawachapa Dodoma Jiji mabao 3-0 shukrani kwa bao jingine la Phiri ambaye anaonekana kuwa katika fomu. Mashabiki waliondoka na furaha na wote wakamsahau Matola.

Na mpaka ninapoandika makala haya mashabiki wapo kimya juu ya Matola. Nadhani ni mashabiki wasiojielewa. Mashabiki wote ambao wanajielewa huwa hawayumbishwi na matokeo. Wanasimama katika ukweli wa kile wanachokiamini.

Niliwahi kuandika hapa kwamba mashabiki wetu huwa hawajui kwanini wapo katika msimamo fulani. Mfano suala hilihili la Matola muulize shabiki aliyekuwa amekaza mishipa ya shingo akidai hamtaki Matola ukimuuliza ni kwanini msimamo wake ni huo atakwambia ‘Aondoke tu mbona makocha wanafukuzwa yeye anabakia kila mara’

Hii ni hoja kuu ya mashabiki lakini hawana hoja yoyote nyingine ambayo ina ushahidi kama vile anahujumu timu au vinginevyo. Binafsi namuonea huruma Matola kwa sababu naamini bado anatembelea katika uzi mwembamba. Wanadamu wanaoishi Tanzania wengi wao ni wanafiki.

Tazama namna gani wamemsahau sasa hivi ambapo kila kitu kinaonekana kuanza kwenda sawa. Lakini kama Simba ikitokea ikapoteza mechi au kucheza vibaya siku chache zijazo basi bado kuna asilimia kubwa gunia la misumari likamuangukia yeye.

Ukibisha jaribu kujikumbusha Matola alikuwepo katika vikosi vya Simba ambavyo viling’ara katika miaka ya karibuni chini ya makocha mbalimbali lakini hatukuwahi kusikia mashabiki wakilalamika uwepo wake katika benchi la ufundi.

Kuna mambo mawili yanaweza kutokea mbele ya safari endapo Simba itacheza mechi fulani kwa kiwango kibovu. Utaratibu wetu ni kutafuta mchawi. Kuna asilimia kubwa mashabiki wakarudi tena kwa Matola au wakaamua kumsaka mchawi mwingine. Ili mradi mchawi asakwe.

Tanzania mpira wa miguu tumeuondolea ubinadamu. Hakuna kitu kingine ambacho tunaweza kukielewa zaidi ya ushindi. Haishangazi kuona hatujawahi kuacha kusaka mchawi.

Tukiachana na suala hilo la Matola, ndani ya uwanja Simba wanaonekana kuanza kuimarika taratibu. Wachezaji wengi wameanza kucheza vizuri. Bado naona nina matatizo na Nelson Okwa ambaye hajaonyesha tofauti yake na baadhi ya wachezaji ambao tunao nchini.

Lakini Augustine Okrah ameendelea kuwa bora. Ana kasi, mbio, chenga lakini zaidi ni kwamba ana maamuzi mazuri. Sijaelewa ni kitu gani kilichosababisha agombane na Dejan ambaye anaamini Okrah alikuwa anamnyima pasi. Na hasa pale ninapozingatia Okrah sio mchezaji mchoyo wa pasi.

Kitu kingine ambacho Okrah anawapa Simba ni uwezo wake wa kupiga mipira iliyokufa. Wakati mwingine unaweza kuishinda mechi ya soka kwa kutumia vema mipira iliyokufa kama unaona wachezaji wako wanashindwa kuwafungua wapinzani kwa urahisi. Okrah anaweza kuja kuibeba Simba katika mechi muhimu zaidi kwa kutumia tu mipira iliyokufa hata kama timu haikucheza vema.

Zaidi ya yote kwa sasa habari ya mjini ni Phiri. Simba ilihitaji mshambuliaji wa aina yake baada ya msimu uliopita kuwa na washambuliaji watatu ambao walipungukiwa makali, Meddie Kegere, Chris Mugalu na John Bocco.

Baada ya Simba kumkosa Cesor Manzoki kulikuwa na kelele nyingi kwamba timu hiyo imefanya kosa kubwa kuanza msimu bila ya kuwa na mshambuliaji mwingine lakini ni wazi Phiri ameanza kuwanyamazisha watu. Kelele za umuhimu mkubwa wa Simba kuwa na mshambuliaji mwingine zimeanza kupungua.

Kitu cha muhimu ni kwa mzawa, Habib Kyombo kuvaa vyema viatu vya John Bocco. Juzi alifunga bao maridadi lakini mwenendo wake kwa ujumla sio mzuri. Labda bao la juzi litamrudishia nguvu ya kujiamini.

Lakini mwingine ambaye inabidi arudi katika ubora wake kwa haraka zaidi ni Clatous Chotta Chama. Asipojiangalia umuhimu wake ndani ya kikosi cha kwanza unaweza kwenda kwa Okrah. Chama bado hajarudi kuwa Chama yule ambaye tunamfahamu.