HISIA ZANGU: Namna Haji Manara alivyowafunika Aziz Ki na Manzoki

NCHI hii bwana. Siku nyingine usiniulize kwanini tupo hapa tulipo. Siasa zipo kila nyanja. Kwa mfano, huku kwetu katika michezo, hasa soka, jioni ya Jumamosi ilipaswa kuwa ya mastaa wawili maarufu wa soka waliotingisha katika dirisha la uhamisho la wachezaji Tanzania kwa sasa.

Azizi Ki na Cesar Manzoki. Walikuwepo wengi lakini huyu Aziz Ki anabakia kuwa mchezaji aliyetingisha zaidi katika dirisha la uhamisho la wachezaji msimu huu. Simba na Yanga wote walimpigania baada ya kuona kiwango chake katika mechi mbili ambazo klabu yake ya zamani ASEC Mimosas ilicheza na Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba wanaweza kuficha ukweli kwamba walimtaka sana lakini bahati mbaya walizidiwa akili na Yanga. Simba wataficha na wataendelea kuficha kwamba hawakumtaka Aziz Ki. Ndivyo siasa za mpira wetu zilivyo. Wote huwa zinatufundisha ile hadithi ya utotoni ya ‘Sizitaki mbichi hizi’.

Lakini jioni hii hii ya Jumamosi Yanga walicheza pambano kubwa zaidi la kujiandaa na msimu wao, Wiki ya Mwananchi, walicheza dhidi ya Vipers ya Uganda ambayo ina mshambuliaji anayeitwa Manzoki. Huyu anakaribia kuwa mchezaji wa Simba. Zimebaki asilimia chache avae jezi nyekundu na nyeupe za Msimbazi.

Wakati huu Manzoki akikaribia Msimbazi, watu wa Simba na Yanga wote walikuwa na shauku ya kumuona Manzoki. Watu wa Simba wanaamini kwamba kando ya Moses Phiri, huyu Manzoki ndiye mshambuliaji ambaye amesababisha washambuliaji wao, Meddie Kagere na Chris Mugalu waondolewe klabuni.

Simba wanataka kujua ni kitu gani hasa ambacho Manzoki anacho miguuni. Walikuwa wanatamani wamuone katika pambano hili dhidi ya Yanga. Hapo hapo Yanga walikuwa wanatamani kujua Manzoki ni mchezaji wa namna gani. Kwao walikuwa wanasubiri kumzomea zaidi.

Kabla ya mechi picha ambazo zilikuwa zimesambaa zaidi ni zile za Manzoki kutua Dar es salaam pengine kuliko ujio wa timu yake Vipers. Alionekana akiwa sambamba na Crescentius Magori mmoja kati ya vigogo wa Simba ambao wanasifika kuwa mafia katika nyakati za uhamisho wa mastaa kama hizi.

Wote tunasubiri kuwaona Aziz Ki na Manzoki. Kilichotokea ni kwamba wote walikaa katika mabenchi ya timu zao. Ni Aziz Ki ndiye ambaye aliingia uwanjani katika kipindi cha pili. Manzoki hakucheza. Hatujui kwanini hakucheza. Labda Yanga walipanga kuihujumu kwa kuwatuma wachezaji wao wakamvunje staa huyu mtarajiwa wa Simba.

Lakini kabla hatujajua kwanini makocha wao hawakupanga, ghafla likatokea tukio ambalo lilitufanya tusijishughulishe tena na mastaa hao. Akatokea Haji Manara, ofisa Habari wa Yanga aliyefungiwa miaka miwili kwa kile kinachoitwa kumdharau hadharani Rais wa TFF, Wallace Karia. Akaingia uwanjani na kutambulisha wachezaji wa timu ya Yanga.

Mpaka sasa sielewi kama Haji alikuwa sahihi au hapana. Ninachoelewa ni kwamba tukio lake lilikuwa maarufu kuliko mechi yenyewe. Tukio lake lilikuwa maarufu kuliko uwepo wa mastaa wapya katika kikosi cha Yanga. Tukio lake lilikuwa maarufu kuliko uwepo wa Manzoki uwanjani.

M-wisho wa mechi Yanga ilifungwa mabao 2-0 lakini watu wakaishia kumuimba Haji. Yanga walishangilia, Simba wakahoji kulikoni. Asubuhi tukaamka na Haji katika vyombo vya habari. Zaidi ni kwamba TFF ikamfungulia shtaka jingine yeye pamoja na Rais mpya wa Yanga, Hersi Saidi.

Binafsi nilikuwa Misri katika kambi ya Azam. Sikutazama soka. Hii inakuwa bahati mbaya kwangu na kwa watu wote ambao hawakutazama mechi. Hauwezi ukapita katika vyombo vya habari na kujua kwanini Manzoki hakucheza. Hakukuwa na maoni ya kocha wa Vipers kuhusu suala hilo.

Hata kama sio maoni lakini kungeweza kuwa na habari za uchunguzi kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu Manzoki kujua kwanini hakucheza katika pambano hilo. Hatukuweza kujua. Katika dunia ya kisasa ya soka pamoja na ile ya uandishi wa habari hii ingeweza kuwa habari nzuri. Wote wakazama kwa Haji.

Kwa upande wa Aziz Ki hakukuwa na maoni ya kichambuzi kuhusu kiwango chake kwa dakika alizocheza. Huyu ni mchezaji ambaye alisubiriwa kwa hamu nchini. Tulipaswa kujua walau mawili matatu kuhusu dakika alizocheza. Bahati mbaya kama ulitaka kufuatilia kuhusu habari zake basi ungejikuta ukikumbana na habari za Haji.

Achana na hao, hili linakwenda kwa wachezaji wapya na wa zamani katika upande wa Yanga. Upande ambao watu wengi walikuwa na maslahi nao zaidi kwa sababu Yanga ni timu ya nyumbani. Kipi kiliwawasibu mpaka wakapoteza pambano hata kama lilikuwa la kirafiki.

Hauwezi kusoma popote zaidi ya kukumbana na habari za Haji kutambulisha wachezaji. Haya ndio matokeo ya siasa katika mpira wa Tanzania. Popote alipo Haji anaweza kujisifu namna gani ameweza kuwa mkubwa kuliko mpira wetu. Anazungumziwa kila kona.

Kazi yake zamani ilikuwa inaitwa ‘katibu mwenezi’ na haikuwa na umaarufu huu. Ni kazi ambayo isingeweza kuharibu pambano moja zuri la soka. Sijui namna gani dunia imekwenda kasi na leo tunaweza kukaa chini kumjadili mtu mwenye cheo cha kawaida katika klabu kuliko pambano lilivyokwenda pamoja na mambo mengine.

Huu ndio uharibifu uliotokea katika soka letu. Hata hapa kuna wasomaji wengi ambao wangependa nielezee maoni yangu kuhusu kama Haji alikuwa sahihi au hapana. Watu hawataki kujadili kiini cha tatizo. Ukweli ni kwamba kiini cha tatizo ni Watanzania kuendekeza siasa katika michezo.

Sijui kama wenzetu wana nafasi hizi katika soka la Ulaya, Amerika Kusini, Asia na maeneo mengine ya Afrika. Ninachojua ni kwamba sisi tumetengeneza utaratibu wetu wa ajabu ambao sasa tunavuna matunda yake. Tunazidi kutoka katika kujadili mpira na tunajadili zaidi mambo ya nje ya uwanja.

Wale ambao tulikuwa tunawashutumu kwa kutokuwa wazalendo kwa kupenda zaidi mpira wa Ulaya kuliko wa kwetu hatuna cha kuwaambia. Tunaficha sura zetu. Wenzetu wanafaidi mpira tu. Hawana mambo mengi nje ya uwanja. Hawamjui ofisa habari wa Manchester United wala Barcelona. Huu ndio ukweli mchungu. Tazama tu jinsi ambavyo Haji amefanikiwa kuifunika mechi ya thamani kati ya Yanga na Vipers. Mechi nzuri ya Wiki ya Mwananchi. Miaka kadhaa ijayo anaweza kutazama nyuma na kututambia kwa wajukuu zake jinsi alivyokuwa gumzo katika pambano hilo ingawa hakuwa mchezaji wala kocha.

Ni tofauti na namna ambavyo baba yake, Sunday Manara anatazama nyuma takribani miaka 48 iliyopita na kujisifu namna alivyolifunika pambano la Yanga na Simba pale Nyamagana akiwa kama kiungo mahiri mshambuliaji wa Yanga. Tuachane na siasa katika soka.