Prime
HISIA ZANGU: Mambo saba, jicho la haraka haraka Simba vs Constantine

Muktasari:
- Jambo la kwanza. Siku chache baada ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho, Aishi Manula alikuwa mtazamaji wa mechi akiwa nje ya uwanja kwa mara nyingine tena. Mechi kama hizi walau wale wachezaji wazuri ambao hawachezi mara kwa mara huwa wanapangwa.
KULIKUWA na mambo machache ya kuyatazama haraka haraka katika jioni nyingine ya mechi ya CAF pale Uwanja wa Mkapa. Simba walikuwa nyumbani wakicheza na Constantine ya Algeria.
Jambo la kwanza. Siku chache baada ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho, Aishi Manula alikuwa mtazamaji wa mechi akiwa nje ya uwanja kwa mara nyingine tena. Mechi kama hizi walau wale wachezaji wazuri ambao hawachezi mara kwa mara huwa wanapangwa.
Aishi alikuwa mtazamaji kama sisi tu. Tofauti ni kwamba yeye alikuwa karibu na nyasi za uwanjani. Nadhani huu ni mwisho wake Simba. Sawa wanaweza kuwa walihitaji pointi tatu muhimu. Kuna uwezekano pia tunadai kwamba nafasi ya kipa huwa haibadilishwi mara kwa mara. Hata hivyo nilidhani kwamba Aishi alikuwa ana nafasi ya kucheza pambano hilo.
Jambo la pili. Rafiki zetu Constantine walikuja kufanya kama kile majirani zao, MC Alger walikuja kufanya katika pambano dhidi ya Yanga. Na wao walitaka mechi iishe kama ilivyoanza kitu ambacho kiliondoa ladha ya mechi. Walijiangusha mara nyingi.

Achilia mbali kujiangusha lakini hawakutaka kwenda kule ambako Moussa Camara alikuwepo na badala yake wakatumia muda mwingi kuharibu mbinu za Simba kuliko wao wenyewe kufanya mipango yao. Badala ya kutafuta sare kwa njia ya kusaka bao moja wao waliamua mechi iishe kama ilivyo. Na bado walishindwa.
Mpaka walipofungwa bao ndipo akili zikawarudi kwamba walikuwa wanakwenda kushika nafasi ya pili katika msimamo. Kidogo walianza kulitafuta lango la Simba lilipo, lakini walikuwa wamechelewa. Sielewi sana kuhusu mpira wa Afrika, kwani lazima timu ipoteze muda kutafuta ushindi?
Kule kwa wenzetu timu ikicheza katika mazingira ya kusaka sare au kutofungwa, basi watacheza kwa kujihami kwa kiasi kikubwa, lakini hawafanyi kama hawa Waarabu wanavyofanya. Kujiangusha mara kwa mara bila ya sababu za msingi. Wanaudhi mno.

Jambo la tatu. Kibu Dennis ni mchezaji muhimu kwa Simba kwa sababu anafanya vitu muhimu katika wakati muhimu. Watu walilalamika kiasi cha pesa kilichotengwa na Simba kwa ajili ya kumpa mkataba mpya, lakini kuna wakati anathibitisha ubora wake.
Simba walinuna wakati alipotoroka kwenda Norway mwanzoni mwa msimu huu na akachelewa kambi ya timu, lakini ukweli katika nyakati kama jana alithibitisha umuhimu wake. Kibu hafungi mabao mengi lakini anafunga mabao muhimu. Hilo ndilo jambo la msingi kwake.
Ana tatizo la kukosa mabao, lakini papo hapo huwa anafunga mabao muhimu kama alilofunga jana. Haishangazi kuona umuhimu wake ndani ya timu unakuwa mkubwa huku akiwa anabebwa zaidi na tabia yake ya kuhaha uwanjani.

Kuna wakati ana matatizo yake, lakini kwa Simba ya leo anabakia kuwa mmoja kati ya wachezaji wachache sana ambao wana umuhimu mkubwa. Angeweza kuwa mchezaji wa kawaida katika Simba ile ya Jose Luis Miquissone na Clatous Chota Chama lakini kwa Simba hii Kibu ni muhimu.
Jambo la nne. Rafiki yetu Elie Mpanzu tunaendelea kumpa muda, lakini anapaswa kujitazama kwa kiasi kikubwa. Jana alifanya jambo moja muhimu la pasi ya kisigino kwa Kibu aliyefunga kwa shuti kali, lakini achilia mbali tukio hilo Mpanzu ambaye tulikuwa tunamsikia ni tofauti na ambaye tulikuwa tunamuona uwanjani jana.
Mpanzu alikosa mabao ya wazi na wala hakuwa na uamuzi mzuri kama ambavyo tulitegemea kutoka kwake wakati tukisubiri ajiunge na Simba katika dirisha dogo. Anashindwa kuleta tofauti ambayo tunaitegemea kutoka kwake.

Anahitaji kubadilika kwa sababu muda si mrefu mashabiki watamgeuka na kumpotezea uwezo wake wa kujiamini kabisa. Kuna dhana kwamba hakucheza mpira kwa muda mrefu, lakini unapowaza ndani ya kiwango hiki alienda kufanya majaribio na Genk basi ilikuwa wazi kwamba angefeli majaribio.
Jambo la tano. Nadhani Simba wamewafundisha watani zao kitu cha kufanya katika mechi hizi. Wamewafundisha kuchukua pointi zote tatu muhimu katika mechi za nyumbani. Iwe jua iwe mvua Simba huwa wanakosea mara chache pale wanapohitajika kufanya jambo la maana katika Uwanja wa Mkapa.
Tazama mashambulizi yao namna yalivyokuwa hatari kulinganisha na mashambulizi ya Yanga siku moja kabla ya hapo. Simba walikuwa ni watu wa kwenda moja kwa moja katika boksi la adui kwa njia zote. Pembeni na katikati.
Jambo la sita. Wale mashabiki waliofanya ujinga wa kung’oa viti katika pambano kati ya Simba na Sfaxien nadhani jana walishuhudia matokeo ya ujinga wao. Kucheza bila ya mashabiki sio utamaduni wetu. Sio maisha yetu. Ni utamaduni wa Waarabu kutokana na kufungiwa mara kwa mara.

Pambano la jana limetutia dosari ya kijinga. Uwanja mtupu. Nadhani tukio lile halipaswi kujirudia tena. Linawaacha wachezaji wakiwa. Lakini kama ingekuwa mechi muhimu zaidi kuliko ilivyokuwa, basi Constantine wangekaza zaidi na wangepata faida ya kucheza katika uwanja mtupu ugenini.
Kitu cha saba. Simba imebadilika zaidi. Wanaweza kwenda hata fainali kama wakitaka. Wanacheza kwa kasi kubwa tofauti na msimu mmoja uliopita. Wachezaji wengi wapya wamekuwa muhimu katika kikosi cha Simba. Usajili wa safari hii haukukosewa sana na wachezaji wapya wamekuwa na mchango mkubwa.
Kocha Fadlu Davis naye amekuwa na mchango mkubwa ukiangalia namna timu inavyocheza unaona kabisa kuna kitu wanatafuta na kweli wanakipata. Mpira ni mchezo wa hadharani na sasa ni wakati wa kuwapongeza Simba kwa kurudisha makali yao.