HISIA ZANGU: Kapombe wa mechi 100 na Kelvin John wa juzi

NILIONA mahala kwamba Shomari Kapombe ametimiza mechi 100 tangu aanze kuichezea Simba. Nadhani ni katika ujio wake wa pili akitokea Azam. Kuna wakati alicheza Simba kisha akaenda zake Ulaya. Akarudi kuitumikia Azam na baadaye akatimkia Simba.

Shomari ni mwamba katika nafasi yake. Sijaona mpinzani wake katika nafasi yake. Amecheza mechi nyingi za Ligi Kuu Bara na za kimataifa hadi kufika alipofika. Amecheza mechi nyingi pia za timu ya taifa ‘Taifa Stars’. Kifupi Simba na Taifa Stars wamefanya uwekezaji mkubwa kwake.

Nilikuwa nawaza ambavyo Tanzania wachezaji wanapitia safari ndefu mpaka kufika wanapofika. Jaribu kumtazama Shomari amecheza mechi ngapi mpaka kukomaa katika kiasi ambacho amekomaa. Wachezaji wa Tanzania huwa wana safari ndefu mpaka kukomaa hasa katika miaka hii. Afadhali wachezaji wa zamani.

Natazama jinsi ambavyo Genk wanavyomuandaa Kelvin John katika safari yake ya kuwa staa mkubwa klabuni. Ni safari tofauti na ile ambayo Shomari ameandaliwa. Kelvin anacheza katika timu ya vijana ya Genk ambayo huwa ina michuano miwili.

Kelvin anacheza katika ligi ya vijana ya Ubelgiji ambayo tayari Genk wametwaa ubingwa. Yeye ni miongoni mwa wafungaji bora wa ligi hiyo. Lakini Kelvin pia anacheza katika michuano ya vijana ya Uefa. Michuano hii pia Kelvin amekuwa akifanya vizuri. Mechi hizi huwa zinamtia mchezaji uzoefu. Hakuna staa wa Ulaya ambaye hakupita katika michuano hii. Labda kwa wale ambao wamekwenda Ulaya wakiwa wakubwa na wachezaji kamili kama kina Mbwana Samatta.

Tofauti ya Kelvin na Shomari ni kwamba Shomari kapatia uzoefu humohumo katika mechi ambazo amecheza. Kelvin ameanza kupata uzoefu katika mechi nyingi za vijana. Na ndio tofauti ya Kelvin na vijana wa Simba na Yanga na timu nyingine za Tanzania. Wanacheza mechi ngapi kwa wiki? Kila siku wapo mazoezini.

Kwa sababu ya umaskini wetu wachezaji hawana ligi. Huwa kuna michuano kama ya Uhai Cup ambayo inakuja na kuondoka ndani ya wiki chache. Wenzetu wanacheza kila wikiendi na vijana wanakomaa wakiwa wadogo. Iko wapi ligi ya vijana ya Afrika Mashariki na Kati? Haipo. Wenzetu wanacheza kila wikiendi.

Matokeo yake yanasaidia pia kwa vijana kutodanganya umri. Mchezaji anakomaa katika wakati mwafaka. Katika umri mdogo unakuta mchezaji anafanya mambo makubwa. Sisi wachezaji wetu wanachelewa kupevuka na ndio maana wanalazimika kudanganya umri ili kwenda sambamba na wazungu.

Tatizo hili sio la Tanzania pekee. Hata nchi nyingi za Afrika wachezaji wanachelewa kupevuka na hivyo kujikuta wakidanganya miaka ili waende sambamba na wenzao wa Ulaya. Wachezaji kama kina Kelvin wana bahati ya kuwahi kucheza Ulaya mapema na hapana shaka hata maisha yao ya soka yatakuwa marefu.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba zamani tulikuwa na wachezaji wanaopevuka mapema hapa nchini. Kwa mfano, Edibily Lunyamila aliichezea timu ya taifa wakati akiwa kidato cha nne. Leo sioni kama kuna mchezaji wa kidato cha nne anayeweza kucheza timu ya taifa ya wakubwa. Sidhani hata kama kuna mchezaji wa kidato cha nne anayecheza katika timu za vijana.

Nilisoma na Renatus Njohole na Ally Mayai katika Sekondari ya Jitegemee. Tulikuwa katika kidato cha tano. Njohole alikuwa anacheza Simba na alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya vijana. Mayai alikuwa anacheza Yanga. Pambano la Agosti 1998 kati ya Simba na Yanga ambalo Simba walifungwa mabao 3-1 liliwakutanisha wanafunzi wawili wa Jitegemee.

Leo sidhani kama kuna wanafunzi wawili wa shule ya sekondari wanaoweza kucheza pambano la Simba na Yanga. Lakini pia kulikuwa na wachezaji wanatoka chuo kucheza hizi timu. Mfano ni Leodeger Chilla Tenga. Leo hatupati wachezaji wa namna hiyo.

Nadhani wakati ule wachezaji walikuwa wanawahi kukomaa kwa sababu ya kucheza mechi nyingi za shule. Tulipoua michezo ya shule kila kitu kikaanza kwenda kombo. Lakini hata wakati huu tukiwa bize na kitu kinachoitwa academy bado wachezaji wetu wana mechi chache. Wanashinda zaidi mazoezini.

Katika umri wa miaka 22 tayari Kylian Mbappe ameshatwaa Kombe la Dunia. Kama angekuwa Tanzania sasa hivi Mbappe angekuwa ndio kwanza anahaha katika timu za vijana kusaka uzoefu kabla ya kwenda kuharibika katika timu za wakubwa za Simba na Yanga.

Hata hivyo, tayari Mbappe alishacheza mechi nyingi za vijana akiwa na Monaco kama hivi ambavyo Kelvin John anafanya kwa sasa. Na jaribu pia kufikiria. Tayari Kelvin amepandishwa katika kikosi cha kwanza cha Genk. Angekuwa Tanzania angekuwa katika kikosi cha kwanza cha timu gani kubwa? Tuwaandalie vijana mechi nyingi. Ni suluhisho zuri katika soka letu. Vijana wetu wanafanya zaidi mazoezi kuliko kucheza mechi. Uwekezaji tunaoufanya kwa kina Kapombe unatumia nguvu nyingi kuliko inavyopaswa. Wachezaji kama kina Israel Mwenda walipaswa kuwa uwanjani wanashindana na sio kuonekana kama makinda.

Mchezaji kama Bukayo Saka tayari ana uzoefu wa kutosha katika umri wa miaka 20 tu. Huu ni ukweli ambao inabidi tuumeze. Wachezaji wetu wanachelewa sana kukomaa kwa sababu ya mfumo duni ambao tumewawekea. Wengine wanafika juu wakiwa wamechoka tayari.