HISIA ZANGU: Carlinhos, sura ya kitoto maamuzi ya kiume

KUNA mambo mawili inawezekana yaliwalemaza wachezaji wetu utotoni. Kitu cha kwanza ni ule mchezo wa ‘Gombania goli’. Nadhani ni wakati mwafaka wa kuwaambia watoto wetu waachane na mpira wa Gombani goli.

Kwamba mnakuwa wengi halafu kunakuwa na golikipa mmoja tu, wachezaji wengine wote wanakuwa maadui zako. Unawapiga chenga kadri uwezavyo kwa ajili ya kwenda kufunga. Kila aliye mbele yako inabidi umpunguze.

Huu mchezo hauna malengo. Kwa Afrika umeimarisha ujanja mwingi wa wachezaji wetu. Unaibuka kuwa na akili nyingine ya kukaa na mpira. Lakini nadhani unapunguza uwezo wa vijana kuchukua maamuzi yako kwa manufaa ya wenzako.

Katika mchezo huu kitu cha msingi kinachokosekana ni kupiga pasi murua kwa ajili ya wenzako. Wewe unakuwa peke yako na hakuna wa kukusaidia kukamilisha mpango wako. Mnaweza kuwa watu 13, lakini wewe hauna wa kumpasia wala wa kumsaidia ili atimize lengo lake.

Labda inawezekana mchezaji anayeitwa Carlinhos wa Yanga hakufanya michezo hii utotoni. Majuzi aliibuka kuwa shujaa wa Yanga katika pambano dhidi ya Biashara United pale Uwanja wa Taifa. Watu walimsifu kwa pasi muhimu za mara kwa mara.

Binafsi namlinganisha na Kelvin de Bruyne wa Manchester City. Hawana muda wa kukaa na mpira bila ya sababu. Lakini pia wanapenda kucheza soka la matokeo. Kwamba wakiwa na mpira wanataka kitu fulani kifanyike kwa harakaharaka bila ya kupoteza muda.

Hivi ndivyo Carlinhos anavyowafundisha viungo wa Yanga na viungo wa timu nyingine za Tanzania. Anacheza mpira wa matokeo. Viungo wetu wengi wanapenda kucheza ile staili ya Gombania goli. Na kuna wengine wanapenda kucheza soka la ‘Hangaisha bwege’. Ukiwaambia wacheze soka la msingi huwa wanashindwa.

Carlinhos huwa anacheza soka la msingi. Ukiniuliza ni mchezaji gani ambaye amechangia Yanga kupwaya nitakuambia ni huyu hapa Muangola. Akiwepo uwanjani anacheza soka la msingi. Hatazami nyuma wala hazunguki sana. Anataka mpira uende sehemu sahihi kwa haraka sana, hasa maeneo ya mbele.

Pale Yanga naamini kuna viungo wetu wengi wakiongozwa na Fei Toto wamemzidi kipaji, lakini hawachezi kwa malengo. Hawachezi kwa ajili ya kutoa maamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Hili ndio tatizo letu kubwa. Hii ndio tofauti kubwa kati yake na wengineo.

Bahati mbaya sio yeye tu, wachezaji wengi wa kigeni wanaotamba Tanzania sio kwamba wana vipaji vikubwa sana, hapana, isipokuwa ni wazuri katika kufanya maamuzi

katika wakati sahihi. Wakati wa kupiga atapiga, wakati wa kutoa pasi atatoa pasi, wakati wa kupiga pasi fupi atapiga pasi fupi, wakati wa


kupiga pasi ndefu atapiga. Jambo la pili achilia mbali Gombania goli inayofanywa na vijana wetu hadi wanapokuwa wachezaji wakubwa ni kwamba tukiwa tunatazama soka kwa sasa tuanze kubadilika. Kwanini bado tunawashangilia wachezaji ambao wanageuka na mpira kwa umaridadi huku wakirudi katika lango lao?

Tumezalisha viungo wengi wenye tabia hizi kwa sababu wanapofanya hivi bila ya umuhimu wowote bado tunawashangilia sana. Kiungo badala ya kujikita kusaka pasi mpenyezo unakuta anageuka anamzungusha mchezaji wa timu pinzani huku akienda nyuma na jukwaa linasimama kushangilia.

Huyu Carlinhos, huku akiwa na sura ya kitoto lakini bado ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga wanaocheza mpira wa kikubwa. Bahati mbaya mashabiki wameanza kuwa na uelewa na mpira na ndio maana walau wapo wanaojitokeza kumpa sifa.

Zamani asingekuwa maarufu hata miongoni mwa Wanayanga kwa sababu aina yake ya soka sio maarufu kwetu. Watanzania wanapenda wachezaji ambao wanapiga tobo na kanzu uwanjani. Hasa wachezaji wa nafasi yake.

Huku kwetu hata De Bruyne asingekuwa mchezaji maarufu kuliko Haruna Niyonzima. Aina zao za soka zinapokelewa tofauti na mashabiki wa soka nchini. Hata hivyo aina hii ya De Bruyne ndiyo ambayo inakubalika zaidi katika soka la kisasa.

Mpira umekuwa mchezo wa takwimu zaidi. Umeondoka katika kuwa mchezo wa mbwembwe kuelekea katika mchezo wa takwimu. Wachezaji mahiri duniani wanahukumiwa kwa takwimu zao maridadi na sio chenga zao. Hiki ndicho ambacho Carlinhos anawafundisha wachezaji wetu wazawa waliopo Yanga na wale ambao wanacheza timu nyingine.

Wakati mwingine hata wachezaji wa nafasi nyingine uwanjani huwa wanaathirika na tabia hizi. Mfano mzuri ni namna Yanga hawa hawa walichelewa kujua umuhimu wa nahodha wao wa zamani, Nadir Haroub Cannavaro. Zamani watu walikuwa wanataka Cannavaro acheze kama Victor Costa. Kwamba aweze kutuliza mpira vyema, kupiga chenga na kufanya mambo mengine kama vile yeye ni kiungo. Hata hivyo baadaye wakagundua kwamba kazi ya msingi ya mlinzi ni kulihami lango. Hata wakati mwingine akina Pep Guardiola huwa wanaponzwa pale ambapo wanamsajili mchezaji kwa sababu ya umuhimu wake wa kukaa sana na mpira na kusogea nao mbele badala ya kujali sifa ya kwanza ambayo ni kulihami lango.

Matokeo yake ndio wakaenda kusajili walinzi kama akina John Stones ambao walishindwa kufanya kazi ya kwanza ya mlinzi huku wakiiweza kazi ya pili ambayo haikuwa msingi mkuu wa mchezaji husika. Tanzania tumejaza wachezaji wengi ambao wanafanya kazi ya pili badala ya kufanya kazi ya kwanza.

Majuzi kuna rafiki mmoja aliniuliza swali. Simba ikiachana na Ibrahim Ajibu iende kwa mchezaji gani mzuri wa ndani anayecheza kama kiungo mshambuliaji? Sikuwa na jibu sahihi. Labda waende kwa Lucas Kikoti wa Namungo. Vinginevyo ni swali gumu kwa sababu wachezaji wetu wameshindwa kujipambanua vema katika nafasi zao. Wengi ndio hawa hawa ambao hata takwimu zao uwanja ni sio bora. Wana vipaji lakini hawana takwimu bora.