Hesabu za vidole! Makocha sita shakani kushuka daraja Ligi Kuu
Muktasari:
- Hadi sasa zimechezwa raundi 21, zimebaki mechi tisa kwa kila timu kuhitimisha msimu huu ambapo Yanga imeendelea kukaa kileleni na pointi 51 ikiiacha Simba kwa pointi tano ikiwa nafasi ya pili na pointi 46.
LIGI Kuu imefikia patamu kwa kila timu kuanza hesabu za vidole katika kufikia malengo ya msimu huu haswa kwenye kuwania ubingwa, nafasi nne na kukwepa aibu ya kushuka daraja.
Hadi sasa zimechezwa raundi 21, zimebaki mechi tisa kwa kila timu kuhitimisha msimu huu ambapo Yanga imeendelea kukaa kileleni na pointi 51 ikiiacha Simba kwa pointi tano ikiwa nafasi ya pili na pointi 46.
Azam iliyowahi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2013-2014, wamekaza katika nafasi ya tatu kwa pointi 43, huku ikikabiliwa na upinzani mkali kwa timu zilizo nyuma yake, JKT Tanzania pointi 32, Singida Black Stars (32), TRA United (30) na Pamba Jiji (29).
Pamoja na mtifuano huo, inafanya makocha kuanza hesabu za vidole kwa mechi zilizobaki kuhakikisha wanafanya kweli ili kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, wakati timu zinazowania nafasi nne za juu zikipamba moto, huko mkiani kwenye kukwepa kushuka daraja moto unaonekana kuwaka zaidi na kufanya makocha wake kuwa kwenye hatari ya kuikimbia Ligi Kuu msimu ujao.
Mwanaspoti inakuletea orodha ya baadhi ya makocha walio katika hatari ya kushuka daraja na timu zao msimu huu kutokana na mwenendo wa matokeo ulivyo na presha kubwa inayoendelea ndani na nje ya uwanja.
NNE BORA
Pamoja na ugumu ulivyo hadi sasa kwa timu za kuwania ubingwa na za kupambania kushuka daraja zinao uwezo wa kumaliza nafasi nne za juu iwapo kila timu itashinda mechi zake wakiwamo KMC wanaoburuza mkia kwa pointi tisa.
Kwa hesabu ya haraka kwa kutumia vidole, kama KMC itashinda michezo yake tisa iliyobaki itafikisha pointi 36 ambazo zinaweza kufikisha nafasi ya nne na kuishusha JKT Tanzania, japokuwa kwa uhalisia kutoboa kwake ni ngumu.
Kwa sasa timu zenye matumaini ya kumaliza nafasi nne za juu mbali na Yanga na Simba ni Azam FC, JKT Tanzania, TRA United, Pamba Jiji, Singida Black Stars na Dodoma Jiji huku Namungo, Mashujaa na Mtibwa Sugar zikisubiri lolote.
KUSHUKA DARAJA
Kwa hesabu za wadau na mashabiki wa soka wanaiona KMC safari yake ligi kuu kama inaenda mwishoni baada ya michezo michezo 21, huku ikisaka mwenzake wa kwenda naye Championship.
Pamoja na hayo, takribani timu nane haziko salama sana kutokana na utofauti wa pointi uliopo na lolote linaweza kuwakuta iwapo mipango haitawekwa sawa na viongozi husika nje ya uwanja.
Timu kama Namungo yenye pointi 23 sawa na Mtibwa Sugar na Coastal Union iliyokusanya pointi 22 sawa na Fountain Gate, zinawindwa vibaya sana na walio chini yao ambao ni Mbeya City yenye pointi 21 na Tanzania Prisons pointi 14.
Kwa mantiki hiyo, wastani huo wa pointi kwa timu hizo, yeyote atakayezembea anaweza kujikuta akiachwa na kujikuta akishuka daraja kutokana na ushindani wa Ligi Kuu ulivyo kwa sasa na uchu wa pointi tatu kwa timu zote.
Ikumbukwe timu mbili za mkiani zitashuka daraja moja kwa moja, huku zile za nafasi ya 11, 12, 13 na 14 zikikutana mchujo wa kwanza ‘play off’ kisha mbili zitakazopoteza zikicheza na zile za Championship zitakazofuzu hatua ya awali play off.
JUMA MGUNDA
Kocha huyu mwenye wasifu mkubwa kwenye soka la Tanzania wengi wakimuita ‘Guardiola Mnene’ bado hayuko salama na chama lake kutokana na pointi za Namungo kuweza kufikiwa na timu yoyote ya chini yake.
Mgunda aliyewahi kuzinoa Coastal Union na Simba kwa mafanikio, presha yake kwa sasa si nyepesi katika kuinusuru timu hiyo pekee ya ukanda wa Kusini mwa tanzania akiwa na hesabu kali kwa michezo 10 iliyobaki.
Namungo yenye pointi 23 inahitaji japo pointi 10 au zaidi ili kujiweka kwenye hesabu rasmi za kubaki Ligi Kuu, vinginevyo tunaweza kumsikia kocha huyo mwenye akili nyingi uwanjani akishuka daraja na wauaji hao wa Kusini.
JAMHURI KIHWELO ‘JULIO’
Kocha huyo asiyeishiwa maneno nje na ndani ya uwanja, hali yake si nzuri sana na kama atazingua anaweza kujikuta Championship.
Mashujaa ambayo iliweka rekodi ya kupanda Ligi Kuu kupitia play off kwa kuwaondoa Mbeya City iliyokuwa Ligi Kuu, imekusanya pointi 25 ambapo kwa matokeo hayo si rafiki sana kujihakikishia kuwa salama.
Julio ambaye tayari amejiapiza kuibakiza timu hiyo Ligi Kuu akidai kuachana na soka iwapo Mashujaa itashuka daraja, kibarua chake ni kigumu katika kusaka pointi kuanzia 10 na kuendelea ili abaki kwenye soka.
Kocha huyo amekabidhiwa kikosi hicho akichukua mikoba ya Salum Mayanga, ambapo anahitaji kuonesha uzoefu na uwezo wake kwenye mpira lakini kuthibitisha imani yake kwa viongozi waliompa kazi.
YUSUPH CHIPO
Kocha huyu raia wa Kenya si mgeni katika Ligi Kuu, lakini Mtibwa haiko salama katika vita ya kukwepa kushuka daraja na iwapo hatajipanga kimbinu na kiufundi anaweza kuirudisha Mtibwa Sugar Championship.
Chipo aliyewahi kuzinoa timu za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United (zamani Tabora United) anakabiliana na mzigo mzito wa mechi tisa kuamua hatma yake ya kulinda heshima binafsi na Taifa lake la Kenya lakini zaidi Mtibwa Sugar.
FIKIRI ELIAS
Licha ya kurejea kwa kasi mpya katika kikosi cha Coastal Union, Kocha Elias ana mtihani mzito katika kuinusuru timu hiyo kongwe nchini katika vita ya kushuka daraja msimu huu.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa AFC ya Arusha na KenGold ya Mbeya kwa nyakati tofauti, pointi 22 ilizokusanya timu yake hazimruhusu kunywa glasi ya maji kwa utulivu kutokana na hali ilivyo.
Mechi tisa zilizobaki kwake ni kama mtego kuweza kuutegua vyema kuhakikisha anashinda japo mitano tu ili kujihakikishia kuwa salama Ligi Kuu msimu ujao na kutowarejesha mashabiki kwenye maumivu ya msimu wa 2016/17 waliposhuka daraja.
FRED FELIX MINZIRO
Dakika 810 alizonazo kocha Minziro katika mechi tisa, si za mchezo kuipambania Fountain Gate kubaki salama Ligi Kuu kutokana na upepo ilionao kutokuwa salama kumpa uhuru na utulivu kwenye benchi la ufundi.
Minziro mwenye historia na rekodi nzuri katika kupandisha timu, amekabidhiwa kibarua kikosini humo hivi karibuni na sasa atathibitisha ubora, uwezo na uzoefu alionao tangu kucheza soka hadi sasa kulifundisha.
Vita iliyopo baina ya Fountain Gate yenye pointi 22 na timu zilizopo juu na chini yao inampa kazi ya ziada kocha huyo aliyewahi kutamba na timu za Kagera Sugar, Mbao, KMC na nyingine kuhakikisha anaishinda misukosuko hiyo.
SALUM MAYANGA
Kocha huyu asiye na mambo mengi awapo kazini, mtihani wake si mwepesi sana katika kuikinga na aibu Mbeya City ya kushuka daraja kutokana na matokeo aliyonayo kwa sasa.
Mayanga ambaye amekuwa kocha wa tatu kuifundisha timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, anasaka kulinda heshima yake kutokana mfupa mgumu alionao kwa vijana hao wa jiji la Mbeya.
Pointi 21 ilizonazo timu hiyo ni mzigo mzito kwa Kocha huyo mwenye weledi, rekodi na historia bora kwa Taifa na soka kwa ujumla kuonesha anaweza kufanya kitu na kuilinda nembo hiyo iliyowashinda watangulizi wake, Malale Hamsini na Mecky maxime.
SIKIO KAULI ZAO
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Julio anasema Mashujaa haiwezi kushuka daraja, akiahidi kuwa iwapo itatokea yuko tayari kuachana na masuala ya mpira akitambia ubora na uwezo wa nyota wake.
“Mpira wetu una mazongere mengi lakini niseme rasmi kwamba Mashujaa haiwezi kushuka daraja na iwapo ikiwa hivyo nipo tayari kuachana na mpira, nimeibadili sana timu hii” anasema Julio.
Naye Mayanga anasema Mbeya City bado ina uwezo wa kufanya vizuri akieleza kuwa njia salama ya kufanikisha hilo ni umoja, mshikamano na ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja.
“Huu siyo muda wa kutengana bali kila mmoja kwa nafasi yake atoe mchango wake, tuweke ushirikiano, umoja na mshikamano timu itabaki salama, naamini mechi zilizobaki tunaweza kubadilika” anasema Mayanga.