Haya yalijitokeza kwenye 'unbeaten' ya Yanga

YANGA imekuwa na rekodi ya kipekee kwenye Ligi Kuu Bara ambapo tangu ilipofungwa na Azam FC bao 1-0 Aprili 25, 2021 ilicheza michezo 49 bila ya kupoteza kabla ya kutibuliwa kwenye mechi ya 50 na Ihefu Novemba 29 kwa kufungwa 2-1.

Katika muda wote huo ambayo Yanga iliandika rekodi hiyo yapo mambo ambayo yaliyojitokeza kama Mwanaspoti linavyokuelezea.


MABINGWA

Ndani ya muda huo Yanga ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuukosa kwa takribani miaka minne ambayo ilitawaliwa na wapinzani wao wakubwa Simba na kufikisha jumla ya mataji 28 tangu Ligi Kuu Bara ilipoasisiwa 1965.


YAIFIKIA ARSENAL

Hili ni jambo litakaloendelea kukumbukwa kwa mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa kuifikia rekodi ya Arsenal ya England ya kucheza michezo 49 bila ya kupoteza iliyotokea msimu wa 2003/2004 kuanzia Mei 7, 2003 hadi Oktoba 16, 2004.


MICHEZO ILIYOSHINDA

Katika kipindi hicho Yanga ilishinda michezo 37, sare 12 na kufungwa mmoja tu ikifunga mabao 84 na kuruhusu 20.


CLEAN SHEET 34

‘Clean Sheet’ hizo 34 ni (2-0) v JKT Tanzania (Mei 19, 2021), (1-0) v Simba (Julai 3, 2021), (2-0) v Ihefu (Julai 15, 2021), (1-0) v Kagera Sugar (Septemba 29, 2021).

(1-0) v Geita Gold (Oktoba 2, 2021), (2-0) v KMC (Oktoba 19, 2021), (2-0) v Azam FC (Oktoba 30, 2021), (2-0) v Mbeya Kwanza (Novemba 30, 2021), (4-0) v Dodoma Jiji (Desemba 31, 2021), (2-0) v Coastal Union (Januari 16, 2022).

(1-0) v Polisi Tanzania (Januari 23, 2022), (2-0) v Mtibwa Sugar (Februari 23, 2022), (3-0) v Kagera Sugar (Februari 27, 2022), (1-0) v Geita Gold (Machi 6, 2022), (2-0) v KMC (Machi 19, 2022), (2-0) v Dodoma Jiji (Mei 15, 2022).

(4-0) v Mbeya Kwanza (Mei 20, 2022), (3-0) v Coastal Union (Juni 15, 2022), (2-0) v Polisi Tanzania (Juni 22, 2022), (1-0) v Mtibwa Sugar (Juni 29, 2022), (2-0) v Coastal Union (Agosti 20, 2022) na (3-0) v Mtibwa Sugar (Septemba 13, 2022).

(1-0) v KMC (Oktoba 26, 2022), (1-0) v Geita Gold (Oktoba 29, 2022), (1-0) v Kagera Sugar (Novemba 13, 2022), (2-0) v Dodoma Jiji (Novemba 22, 2022), (2-0) v Mbeya City (Novemba 26, 2022), (0-0) v Namungo (Mei 15, 2021).

(0-0) v Dodoma Jiji (Julai 18, 2021), (0-0) v Simba (Desemba 11, 2021), (0-0) v Mbeya City (Februari 5, 2022), (0-0) v Simba (Aprili 30, 2022), (0-0) v Ruvu Shooting (Mei 4, 2022) na (0-0) v Tanzania Prisons (Mei 9, 2022).


REKODI YA UGENINI

Kabla ya kufungwa 2-1 na Ihefu Novemba 29, Yanga ilicheza jumla ya michezo 27 ugenini bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Coastal Union mabao 2-1 Machi 4, 2021 ambapo kati ya hiyo ilishinda 19 na sare minane.


SIMBA MAKOCHA SITA

Wakati Yanga ikiendelea kutamba na kocha wake mkuu, Nasreddine Nabi kwa upande wa wapinzani wao Simba hali imekuwa ni tofauti kabisa kwani kwa kipindi hicho imebadilisha jumla ya makocha sita kwenye benchi lake la ufundi.

Ilianza na Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes Da Rosa, Pablo Franco Martin, Zoran Maki na sasa Juma Mgunda.


HERSI RAIS MPYA

Julai 9, mwaka huu Injinia Hersi Said alitangazwa rasmi kuwa Rais mpya wa klabu hiyo baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ikiwa ni mabadiliko ya mfumo wa kiuendeshaji ikitoka kuwa chini ya wanachama hadi kuendeshwa kama kampuni.


HAT-TRICK TANO (5)

Kwa msimu wa 2021/22 ni wachezaji watatu tu waliofunga hat-trick ambao ni Jeremiah Juma (Tanzania Prisons) v Namungo (Novemba 27, 2021), Shiza Kichuya (Namungo) v Mtibwa Sugar (Juni 26, 2022) na Idris Mbombo (Azam FC) v Biashara United (Juni 29, 2022).

Msimu huu pekee wakati mzunguko wa kwanza ukimalizika tayari zimefungwa mbili akianza Fiston Mayele (Yanga) v Singida Big Star (Novemba 17, 2022) na John Bocco (Simba) aliyeifunga Ruvu Shooting Novemba 19, mwaka huu.


DTB YAPEWA JINA JIPYA

Baada ya kupanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu huu uongozi wa DTB ulibalisha jina la timu hiyo na kuiita Singida Big Stars.

Jina hilo lilibadilishwa Mei 30, mwaka jana baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship na pointi 66.


NDOTO YA STARS QATAR YAFIFIA

Moja ya ndoto kubwa ya Watanzania ni kuona timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ nayo inashiriki katika fainali hizo kubwa na za kusisimua zaidi Duniani.

Katika hatua za kufuzu Stars ilishindwa kupenya raundi ya mwisho ya mtoano baada ya kushindwa kuongoza Kundi ‘J’lililokuwa na timu za DR Congo, Benin na Madagascar kufuatia kumaliza nafasi ya tatu na pointi zake nane.

Kundi hilo Stars ilishinda michezo miwili (3-2) v Madagascar, (1-0) v Benin, sare miwili (1-1) v DR Congo, (1-1) v Madagascar na kufungwa miwili (1-0) v Madagascar, (3-0) v DR Congo na kuifanya Congo kusonga mbele kwa pointi 11.


MANARA AFUNGIWA

Julai 21 mwaka huu aliyekuwa Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara alifungiwa kutojihusisha na masuala ya soka ndani, nje ya nchi kwa miaka miwili na faini ya Sh20 milioni kwa kosa la kumtolea maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Wallace Karia.

Manara alikutana na adhabu hiyo baada ya kufanya hivyo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) uliozikutanisha Yanga dhidi ya Coastal Union uliochezwa Julai 2, 2022 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.


YATINGA MAKUNDI AFRIKA

Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Club African kwa jumla ya bao 1-0 lililofungwa na Stephane Aziz KI ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi kuitoa timu ya Uarabuni.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Yanga ililazimishwa suluhu.

Klabu hiyo kongwe nchini ilifika hatua hiyo baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan na kuangukia Shirikisho ilipofuzu kwa mara ya tatu ndani ya miaka sita baada ya kufanya hivyo 2016 na 2018.