Hawa saizi yetu...Simba, Yanga mipango

Hawa saizi yetu...Simba, Yanga mipango

Muktasari:

  • UKIONDOA Kipanga ya Zanzibar, hakuna sababu ya utetezi utakaoeleweka kwa klabu za Simba, Yanga na Azam kama zitazingua kwenye mechi zao za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika zitakazopigwa mapema mwezi ujao.

UKIONDOA Kipanga ya Zanzibar, hakuna sababu ya utetezi utakaoeleweka kwa klabu za Simba, Yanga na Azam kama zitazingua kwenye mechi zao za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika zitakazopigwa mapema mwezi ujao. Hii ni kutokana na wapinzani ambao watakutana nao kutokuwa tishio kwao kulinganisha na Kipanga ambao uzoefu, ubora wa vikosi na hali ya uchumi inaitofautisha na Club African ya Tunisia wanaokutana nao kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itaumana na Al Hilal Omdurman ya Sudan wakati Simba itavaana na Primiero de Agosto ya Angola, wakati Azam itavaana na Al Akhdar ya Libya katika Kombe la Shirikisho kama Kipanga.

Mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na zile za Kombe la Shirikisho zitachezwa kati ya Oktoba 7 hadi 9 na michezo ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 14 hadi 16 mwaka huu na hata chini ni ubora na uimara wa vikosi vya wapinzani wa timu hizo za Tanzania.


AL HILAL

Yanga itaanzia nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Al Hilal iliyoanzishwa mwaka 1930 na wiki moja baadaye itakuwa, huko Sudan kwenye Uwanja wa Al Hilal jijini Omdurman. Al Hilal ilipenya kuingia katika raundi ya pili baada ya kuitoa St. George ya Ethiopia kwa faida ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa matokeo ya jumla ya 2-2, ikianza kwa kufungwa mabao 2-1 ugenini na kisha ikashinda bao 1-0 nyumbani.


UBORA WAO

Chini ya kocha Florent Ibenge (pichani), Al Hilal imekuwa ikipendelea zaidi kushambulia kutokea pembeni mwa uwanja ikiwatumia zaidi Mohamed Abdelrahman na Makabi Lilepo ambao wana kasi na uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kumiliki mpira huku mshambuliaji wa kati wakipendelea kumtumia Waleed Bakhet.

Silaha yao kubwa ni kushambulia katika dakika zote za mchezo jambo ambalo limewafanya wawe na wastani mzuri wa kufunga bao katika kila mchezo.

Wachezaji tishio katika kikosi cha Al Hilal ni Lilepo, Abdelrahman, Claude Singone, Abdul Ajagun na Abdelrazig Omer


UDHAIFU WAO

Tabia ya kupenda kushambulia imekuwa ikiwagharimu Al Hilal katika safu yao ya ulinzi iliyo na hulka ya kuachia mianya inayotumiwa vyema na wapinzani wao kufumania nyavu zao.

Takwimu zinaonyesha katika mechi 10 zilizopita za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11 ikiwa ni wastani wa bao 1.1 katika kila mechi. Ikikutana na timu inayomudu kushambulia vyema kwa kushtukiza, imekuwa ikikutana na wakati mgumu kutokana na uchache wa wachezaji wake inapozuia.


KIKOSI

Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com, thamani ya kikosi cha Al Hilal ni Euro 2.75 milioni (Sh 6.3 bilioni) na mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi ni Abdul Ajagun aliyenaswa na timu hiyo kutoka Cape Town City ya Afrika Kusini kwa ada ya Yuro 575,000 (Sh 1.3 bilioni).


PRIMIERO DE AGOSTO

Ni miongoni mwa timu kongwe za Angola ikiwa imeanzishwa 1977 ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi la Angola ikitumia Uwanja wa FranÁa Ndalu uliopo jijini Luanda ambao unaingiza mashabiki 20,000.

Imekuwa ikitumia jezi nyekundu zenye michirizi yenye rangi nyeusi na bukta nyeusi wanapokuwa nyumbani na ugenini wanavaa jezi nyeupe zenye michirizi ya rangi nyeusi.

Wametinga raundi ya pili baada ya kuitoa Red Arrows kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1, ikishinda bao 1-0 ugenini na kisha kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.


MAKALI YAO

De Agosto ni timu yenye kundi kubwa la wachezaji wanaopenda kumiliki mpira kutokana na ufundi iliyonayo na imekuwa ikipendelea kupiga pasi nyingi fupifupi za harakaharaka pindi inapojenga mashambulizi. Ni hatari katika kufunga kwa kutumia mipira ya krosi na mara nyingi imekuwa ikikabia wapinzani kuanzia mstari wa mbele, kwa lengo la kuwalazimisha wafanye makosa, kisha iwaadhibu.


UDHAIFU WAO

Safu ya ulinzi ya de Agosto imekuwa na udhaifu wa kujisahau na hushindwa kuhimili mashambulizi hasa inapokutana na washambuliaji wajanja wa kutumia nafasi na kudhihirisha hilo, katika mechi 10 za kimataifa zilizopita, imefungwa mabao 11 ikiwa ni wastani wa bao 1.1 kwa mechi.

Haina washambuliaji wanaojua kutumia vyema nafasi na kuthibitisha hilo, imefunga mabao nane tu katika mechi zao 10 za mwisho za kimataifa.


KIKOSI

Mtandao wa www.transfermarkt.com unabainisha kuwa kikosi cha Primiero de Agosto iliyo chini ya kocha Srdjan Vasiljevic kutoka Serbia kina thamani ya Euro 2.25 milioni (Sh 5.1 bilioni).

Simba imepata bahati kubwa ya kukutana na Agosto katika kipindi ambacho nyota hatari wa timu hiyo, Ambrosini AntÛnio CabaÁa ‘Zini’ (20), ambaye amepelekwa kwa mkopo katika timu ya AEK Athens inayoshiriki Ligi Kuu ya Ugiriki aliyehusika na mabao yote mawili yaliyofungwa na de Agosto dhidi ya Red Arrows, akifunga moja na kupiga pasi moja ya bao.

Ukiondoa Zini, wachezaji wengine hatari katika kikosi cha de Agosto ni Mawiya Jiresse, Camilo Mbule Ngongue, Manuel Keliano, Dago Tshibamba na Domingo Cuxixima.

Tshibamba ndiye mchezaji ghali zaidi katika kikosi chao akiwa amenunuliwa kwa ada ya Euro 400,000 (Sh 914 milioni).


AL AKHDAR

Itakutana na Azam katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na itaanzia nyumbani kabla ya mchezo wa marudiano kupigwa katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Ilifuzu raundi ya pili baada ya kuitoa Al Khartoum ya Sudan kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 ambao waliupata katika mchezo wa kwanza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Benina Martyrs uliopo jijini Benghazi, Libya.

Hii ni mara ya tatu inashiriki mashindano ya Klabu kwa Afrika na mbili zilizopita waliishia hatua za mwanzoni. Inanolewa na kocha raia wa Bahrain, Samir Chammam


UDHAIFU NA UIMARA

Ni timu inayofahamu vyema kujilinda hasa inapokuwa ugenini lakini ni hodari wa kushambulia kwa kushtukiza ikiwatumia zaidi washambuliaji na viungo wake wenye kasi.

Lakini ina matumizi mazuri ya nafasi za mabao ambayo imekuwa ikitengeneza na kuthibitisha hilo, katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti imefunga mabao tisa, huku ikiruhusu mabao mawili.

Kama ilivyo kwa timu nyingi kutoka Kaskazini mwa Afrika, Al Akhdar imekuwa na tabia ya kupoteza muda hasa pale inapokuwa inaongoza au ina matokeo ambayo yana faida kwa upande wao. Udhaifu wao ni kutokuwa na mabeki wazuri wa pembeni ambao sio imara sana pindi ikutanapo na mawinga na washambuliaji wenye kasi na wajanja wa kuchezea mpira.


KIKOSI

Kikosi cha Akhdar kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com kina thamani ya Euro 1.95 milioni (Sh 4.5 bilioni) na mchezaji ghali zaidi ni winga wa Angola, Ary Paper aliyenunuliwa kutokea Ismaily ya Misri kwa dau la Euro 400,000 (Sh 914 milioni).


CLUB AFRICAIN

Ni kati ya timu zenye mafanikio makubwa Tunisia, ikiwa imetwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja, ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara 13, pia Kombe la Chama cha Soka Tunisia mara 13. Ilianzishwa mwaka 1920 jijini Tunis na imekuwa ikitumia Uwanja wa Olympique de RadËs unaoingiza idadi ya mashabiki 60,000. Inaongozwa na kocha raia wa Ufaransa, Bertrand Marchand


KIKOSI

Thamani ya kikosi cha Club Africain kwa taarifa za mtandao wa www.transfermarkt.com ni Euro 9.25 milioni (Sh21 bilioni) na mchezaji ghali zaidi ni beki wa kati mwenye uraia wa Tunisia na Ufaransa, Nader Ghandri mwenye thamani ya Euro 650,000 (Sh1.5 bilioni).