Gundu, nyota Simba, Yanga walioshuka daraja

KUNA mastaa ambao waliwika wakiwa na Simba na Yanga na baadhi walitegemewa timu ya Taifa Stars, msimu ulioisha wamekumbana na changamoto nzito ya kushindwa kuzibeba timu walizozitumikia msimu wa 2020/2021 hadi zimeshuka daraja.

Mwanaspoti linakuletea kikosi cha mastaa hao, ambao timu zao za JKT Tanzania, Ihefu, Gwambina na Mwadui zimeshuka daraja, licha ya wao kuonyesha viwango vya juu ambavyo havijaweza kusaidia kuzuia changamoto hiyo.


Deogratius Munishi ‘Dida’ - Ihefu

Jina la kipa Deogratisu Munishi ‘Dida’ ni kubwa katika jamii ya wanasoka, amezichezea timu ambazo nitamanio la wachezaji wengi ambao bado hawajaonja raha yake, Simba, Yanga na Azam FC pamoja na Taifa Stars.

Baada ya kuachana na Simba, amekuwa na bahati mbaya ya kushuka na timu anazozitumikia alianza na Lipuli ya Iringa na sasa msimu huu kashuka na Ihefu.


William Lucian ‘Gallas’ - Mwadui FC

Jina la utani la Gallas alipewa akiwa anaichezea Simba, limetokana na beki namba mbili wa timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu za Arsenal, Chelsea na Spurs zinazoshiriki Ligi Kuu England. William msimu huu uliomalizika hivi karibuni haukuwa mzuri kwake kwani ameshuka na Mwadui FC, licha ya kiwango chake kuwa juu.


Paul Ngelema - JKT Tanzania

Mchezaji wa zamani wa Simba, Paul Ngalema alikuwa na wakati mgumu msimu huu baada ya kushindwa kuisaidia timu yake ya JKT Tanzania kusalia Ligi Kuu Bara.


Novart Lufunga - Gwambina

Aliyekuwa beki namba wa kati wa Simba, Novart Lufunga ni kati ya mastaa waliokumbwa na changamoto ya timu aliyoichezea msimu huu kushuka ambayo ni Gwambina FC.


Joram Mgeveke - Mwadui FC

Ni beki wa kati wa zamani wa Simba ambaye msimu uliomalizika aliichezea Mwadui akiwa kama nahodha lakini akashindwa kuiokoa timu hiyo na janga la kushuka daraja.


Jabir Aziz - JKT Tanzania

Japokuwa alikuwa ni panga pangua kikosi cha kwanza cha kocha Mohammed Abdallah ‘Bares’ kiwango chake hakijazuia JKT Tanzania kushuka daraja kwa staa huyo wa zamani wa Simba.


Mrisho Ngassa - Gwambina

Ngassa ambaye alitamba na Yanga na Simba na alipata nafasi ya kucheza Free State ya Afrika Kusini, huu msimu haukuwa mzuri kwa upande wake baada ya kushuka na Gwambina FC.


Mwinyi Kazimoto - JKT Tanzania

Aliyekuwa kiungo mkabaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto hakuwa na msimu mzuri, kwanza hajamalizia mechi kutokana na kusumbuliwa na majeraha, kama haitoshi timu yake ya JKT Tanzania imeshuka daraja.


Raphael Daud - Ihefu

Baada ya kuachwa Yanga akaibukia Ihefu kupitia usajili wa dirisha dogo, hata hivyo haukuwa msimu mzuri kwake baada ya timu hiyo kushuka daraja chini ya kocha Zuber Katwila.


Paul Nonga - Gwambina FC

Licha ya kwamba amemaliza na mabao sita, straika wa zamani wa Yanga hakuwa na bahati ya kuisaidia timu yake ya Gwambina kusalia ligi kuu.


Danny Lyanga - JKT Tanzania

Staa wa zamani wa Simba, Danny Lyanga pamoja na kujipinda kufunga mabao10 msimu uliomalizika hakuiweza kuisaidia timu yake ya JKT Tanzania imeshuka daraja.

Wakati wachezaji wa akiba ni mastaa wa zamani wa Simba, Uhuru Seleman (Mwadui), Kigi Makasi (JKT Tanzania), wakati mastaa wa Yanga ni Juma Mahadhi (Ihefu)na Gustapha Saimon (Mwadui FC).