Fei wa Kagera hatofautiani na Nyoni

New Content Item (1)
New Content Item (1)

ANZIBAR imejaliwa kuwa na vipaji vingi vya soka licha ya kuwa kwa upande wao halina fedha na wengi wanacheza kwa kujifurahisha.

Ukitaka kupata wachezaji bora na mahiri wanaocheza eneo la kiungo unaambiwa vuka maji nenda visiwani kwani hautajuta na hii ni kutokana na sasa wengi wao kuja Bara kutafuta maisha na kuonyesha ubora wa hali ya huu.

Ukitaja viungo bora wazawa wanaocheza Ligi Kuu Bara idadi kubwa ni mastaa kutoka Zanzibar, na kwa sasa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiye anayeimbwa sana kutokana na ubora alionao. Ukiachana na Fei Toto anayekipiga Azam FC kuna Mudathir Yahya anayecheza Yanga amekuwa akiibwa kutokana na ubora anaouonyesha, basi unaambiwa sio hao tu kuna viungo wengine imara zaidi kutoka Zanzibar hawatajwi sana kutokana na kucheza timu ambazo hazina mashabiki wengi.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na kiungo wa Kagera Sugar, Feisal Hilal Nassor aliyezungumza mambo mbalimbali akimtaja pia Awesu Awesu ‘Rasta’ kuwa ndiye kiungo aliyemshawishi kuwekeza kwenye soka.


NI AWESU

Awesu Awesu ni kiungo ambaye amewahi kukipiga Azam FC, Kagera Sugar na sasa anacheza kwa umahiri KMC akicheza vyema eneo la kiungo mkabaji na kuna wakati alitajwa kujiunga na Yanga ili aweze kuwa msaidizi ya Khalid Aucho.

“Awesu hazungumzwi sana, lakini naamini kwa sababu hachezi timu zenye ushawishi mkubwa wa mashabiki wengi, kwani ndiye kiungo wangu bora na ndiye aliyenifanya nipende mchezo wa mpira na huwa najifunza vitu kutoka kwake,” anasema Feisal.

“Ni kiungo mbunifu na anatumia zaidi akili sio nguvu awapo na umiliki wa mpira. Uwanjani ni mwepesi wa kutoa pasi hakai na mpira mguuni kumfanyia madhambi sio rahisi sana, lakini ni mchezaji ambaye ana mpira wa kukera akikutana na viungo wanaotumia nguvu kwani mpira wake wa akili unawapa shida.”


MUNGU KWANZA

Soka limekuwa likitajwa baadhi ya wachezaji kuamini kuwa bora kufanya ndumba ili watoboe, matukio ambayo kwa kiasi yamesheheni Ligi Kuu Bara, lakini yamekuwa yakifika mbali zaidi kwa kuwahusisha hadi mashabiki.

Kiungo huyo wa Kagera anadai haamini katika ndumba. “Mimi ni muumini wa masuala ya dini na mazoezi kwenye majukumu yangu ya soka, na ndio maana mara yangu ya kwanza kucheza soka la ushindani niliposajiliwa pesa yangu niliyoipata niliitoa sadaka msikitini ili kumuomba Mungu anifanikishie malengo yangu,” anasema Feisal.

“Soka ndio ajira yangu nimewekeza huku naamini katika kumuamini Mungu ili niweze kufanikisha mipango yangu.  Namshukuru amekuwa pamoja nami haniachi kwa lolote. Nafurahia kazi yangu.”


HADI BEKI YUMO

Nafasi ya wachezaji viraka kwenye soka Bara sio kubwa sana kwani ni wachache wanaoaminika na kupewa nafasi ya kucheza nafasi nyingi uwanjani kama ilivyo kwa Erasto Nyoni ambaye anakipiga Namungo FC kwa sasa, lakini Feisal anasema pia yupo bora maeneo mengi uwanjani. “Wengi wamezoea kuniona nikicheza eneo la kiungo, lakini mimi ni bora maeneo mengi uwanjani na nimekuwa nikipewa nafasi ya kucheza maeneo mengine mbali na kiungo na nimekuwa nikifanya vizuri.

“Naweza kucheza beki namba mbili, beki ya kati na mshambuliaji wa mwisho,” anasema kiungo huyo ambaye alipita New Power na Taifa ya Jangombe kabla ya kutua Kagera Sugar.


LIGI ZENJI KITONGA

Wachezaji wazawa Bara wamekuwa na safari ndefu kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu tofauti na wale wanaotoka Zanzibar ambao wao kucheza ni kawaida kutokana na vipaji vyao na nafasi kuwa kubwa kwao kupata timu.

“Zanzibar kuna viwanja vingi, muda wa kufanya mazoezi kwa timu ni ambao vijana wengi wanakuwa wametoka kazini, hivyo kujumuika viwanjani kufanya mazoezi na timu ambazo zinacheza ligi ukionyesha uwezo wewe kucheza ligi ni suala la kawaida,” anasema

“Hata usipocheza nao mazoezini, lakini ukionwa na viongozi au makocha ni rahisi kukujumuisha kikosini na unacheza kwa ubora kutokana na kipaji, na Zanzibar vipaji ni vingi changamoto ni malipo tu.”


MAPINDUZI CUP

Ukifuatilia mastaa wengi kutoka Zanzibar waliopata nafasi ya kucheza Bara ni kutokana na kuonyesha uwezo kwenye michuano ya Mapinduzi Cup inayofanyika kila mwaka kama anavyodai Feisal.

“Ligi yetu imepata nafasi ya kuonekana, ni fursa kwetu tofauti na miaka ya nyuma ambayo ili wachezaji wa Zanzibar waonekane, basi hadi michuano ya Mapinduzi Cup ambayo kwa asilimia kubwa imetoa mwanya kwetu kucheza soka la Bara,” anasema.

“Muda wa mashindano hayo ukifika wachezaji wanakuwa tofauti na walivyozoeleka wanacheza kwa kujituma ili kujitengenezea ulaji kwa kupata nafasi ya kucheza Bara ambapo ndio kumekuwa na malipo mazuri tofauti na Zanzibar unaweza ukacheza na usilipwe.”


SOKA AKILI

Kila mchezaji ana aina yake ya uchezaji kwani kuna wale ambao wanapenda mchezo wa nguvu na kuparamiana na wapo wale ambao wanacheza kishua uwanjani kama Clatous Chama ambaye amekuwa hapendi kugusana akihofia kuumia, basi hata Feisal ipo hivyo. “Napenda kucheza soka la akili sio nguvu. Ukitaka nilale na viatu nikutane na wachezaji ambao wanatumia nguvu uwanjani huwa wananipa kazi ya ziada kufanya ili niweze kuipambania timu yangu. Lakini nikikutana na wanaotumia akili mchezo kwangu unakuwa ni burudani,” anasema kiungo huyo anayemtaja Neymar JR wa Al Hilal ya Saudi Arabia kuwa miongoni mwa mastaa wanaomvutia kutokana na aina yake ya uchezaji.


MHILU FUNDI, ILA BASI TU

Akimzungumzia staa wa zamani wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu, Feisal anasema jamaa ni fundi sana.

“Tanzania Bara kuna washambuliaji wengi bora, lakini nimepata bahati ya kucheza na wengi ila navutiwa zaidi na Yusuf Mhilu ambaye kwa sasa anakipiga Geita Gold, ni mchezaji mzuri naamini amekosa kocha sahihi ambaye anajua namna ya kumtumia,” anasema.

“Mhilu ana mwili mzuri wa uchezaji hasa eneo analocheza. Ana nguvu na ana jicho la kuona goli, lakini kwa sasa amekuwa hana makali kama zamani nafikiri akipata kocha akamjenga kisaikolojia atamsaidia na atakuja kuwa bora eneo hilo na bado ana muda wa kucheza kwani ana umri mdogo,” anasema Feisal, kiungo ambaye hajawahi kuonyeshwa kadi nyekundu.


JERAHA LA PENZI

Hakuna mkate mgumu kwa chai, hivyo ndivyo unaweza kusema licha ya Feisal kuwa mgumu uwanjani akipambana na viungo wa timu pinzani, lakini kuna eneo aliwezwa na kuyumba kidogo kiufundi.

“Nilishawahi kuumizwa kwenye mahusiano (ya mapenzi). Kulikuwa na ugomvi kati yangu na mpenzi wangu nikajikuta natoka hadi kwenye mstari kwenye kazi yangu ya soka. Namshukuru Mungu nilikubali na kuamua kusimamia soka ambalo ndilo linaendesha maisha yangu,” anasema.

“Mapenzi yanauma kila mmoja huwa anapitia nyakati kama hizi.”